Na Said Mwishehe, Michuzi TV
HATIMAYE
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, imetoa maelekezo
kwa Serikali kuona umuhimu wa kusikiliza maoni
na ushauri wa wananchi
kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Serikali hususani katika eneo la Tozo za
miamala ya kielektroniki, iliyoanza kutekelezwa hivi karibuni.
Akizungumza
leo Septemba 8,2022 wakati akitoa taarifa ya kikao NEC,Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Shaka Hamdu Shaka amesema pamoja na
mambo mengine Kamati Kuu imepokea na kutafakari kuhusu hatua za kibajeti
zinazoendelea kuchukuliwa kwa lengo la kupata fedha za kutekeleza
miradi ya maendeleo kwa kasi.
“Eneo moja wapo ikiwa ni kupitia
tozo ambapo ni ukweli usiopingika Serikali imefanya mambo makubwa katika
kipindi kifupi kwa mfano ujenzi wa vituo vya afya 234, shule mpya za
sekondari 214 na maeneo mengine kadhaa yanayogusa maisha ya Watanzania
ya kila siku.
“Baada ya kutafakari na kujadiliana kwa kina Kamati
Kuu imeona umuhimu wa serikali kusikiliza maoni na ushauri wa wananchi
kuhusu utekelezaji wa bajeti hiyo, hususani katika eneo la tozo za
miamala ya kielektroniki iliyoanza kutekelezwa hivi karibuni.
“Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imeielekeza Serikali kutazama hali
halisi na kuchukua hatua stahiki kuhusu ushauri na maoni hayo ya
wananchi kuhusu tozo hizo,” amesema na kufafanua
maelekezo hayo yamezingatia ibara ya 20(b) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.
Ameeleza
Ilani inasema hivi “Kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa
gharama nafuu kwa kupanua wigo wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa
huduma za kifedha ili kuongeza huduma jumuishi za fedha nchini,
kuchochea uwekezaji wa ndani na kukidhi mahitaji halisi ya wananchi
hususan wa kipato cha chini na waishio vijijini.”
Aidha amesema
Kamati Kuu ya CCM imeelekeza Serikali kufikiria na kujielekeza kubana
matumizi, kujenga mazingira rafiki na wezeshi ili kujenga uchumi imara
unaozalisha kwa lengo la kutanua wigo wa kodi pamoja na kubuni vyanzo
vipya vya kodi ili kuwa na viwango pamoja na mfumo rafiki wa kodi kwa
kila mmoja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...