Na Janeth Raphael
Serikali kupitia ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) imewataka Waakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kufatilia na kusimamia viongozi wa elimu katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri, Kata na shule kutekeleza mikakati ya uboreshaji na usimamizi wa Elimu Nchini ili kufanikisha malengo ya serikali ya kutoa elimu bora kwa mtoto wa kitanzania.
Akitoa taarifa kuhusu uboreshaji wa huduma kwa walimu Jijini Dodoma Waziri wa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amesema ni Marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma huku akisisitiza wasimamizi wanaotoa huduma kwa walimu kutimiza wajibu wao na kutokubweteka kukaa maofisini.
“ninawaelekeza Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya Wahakikishe Wanawasimamia watendaji wanaotoa huduma kwa walimu (Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM), Maafisaelimu, Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Wathibiti Ubora wa Shule), watendaji hawa niliowataja hakikisheni mnawafuata walimu shuleni, na kutatua kero na malalamiko yao kwa wakati.
Marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma. Narudia tena mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini. Pia Mwalimu akiandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa” amesisitiza
Aidha Mh. Bashungwa amewataka watendaji Tume ya Utumishi wa Walimu, wahakikishe wanaziwezesha Kamati za Tume ngazi ya Wilaya kuwapandisha walimu madaraja, na kuwarekebishia vyeo kwa wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
“Ninamwelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu, kupitia na kuchambua upandaji madaraja wa kila mwalimu, kwa lengo la kubaini stahiki halali ya daraja la mwalimu, na kuchukua hatua stahiki za kuwapandisha madaraja walimu, watakaobainika kucheleweshewa stahiki zao za madaraja” amewaelekeza
Katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zaidi ya walimu 157,923 (laki moja hamsini na saba elfu,mia tisa ishirini na tatu)wamepandishwa madaraja, wamerekebishiwa Muundo wa Utumishi na kulipwa mishahara kulingana na madaraja mapya, katika mwaka 2021 na 2022.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa akizungumza na wanahabari leo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu uboreshaji wa huduma kwa walimu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...