Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Kituo cha kuendeleza kilimo Nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kimewakutanisha wakurugenzi wa halmashauri 18 za mikoa mbalimbali nchini katika kikao kazi kilicholenga kujadili juu ya umuhimu wa kutenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu ili kuifanya nchini kujitosheleza kwa mbegu bora.
Halmashauri zilizoshiriki kikao kazi hicho ni pamoja na Butiama, Musoma, Sumbawanga, Kalambo, Nkasi, Mlele, Nsimbo, Mpanda, Simanjiro, Serengeti, Kiteto, Namtumbo, Madaba, Songea, Mbozi, Momba, Mpimbwe na Uvinza ambazo kwa tafiti zilizofanywa zimeonyesha Wilaya hizo zinavigezo vya kuzalisha mbegu kutokana na jiografia yake.
Akizungumza katika kikao hicho Meneja wa Sera wa Sagcot, Bw.Khalid Mgalamo alisema kikao hicho kimelenga kutoa elimu kwa wakurugenzi hao juu ya hali ya uzalishaji wa mbegu ulivyo hapa nchi na faida za kutenga maeneo ya uzalishaji mbegu za mazao kwa halmashauri na taifa kwa ujumla.
“Tafiti zinaonyesha tunaagiza mbegu za mazao nje ya nchi kwa kiasi kikubwa jambo linalopelekea hasara kwa nchi, hivyo kama kukiwa na mazalishaji wa ndani ajira zitazalishwa na pamoja na kuifanya nchi kupunguza au kuondoka na uagizaji wa mbegu nje, “ alisema Bw.Mgalamo
Alieleza kuwa nguvu kubwa ikielekezwa katika kuandaa maeneo ya kufanya kilimo cha kuzalisha mbegu kutahamasisha zaidi wawekezaji katika sekta hiyo kuja kuwekeza hapa nchini jambo litakalo pelekea ajira nyingi kuzalishwa na mapato kwa halmashauri na taifa kwa ujumla kuongezeka
“Kikao kimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na uwelewa wa pamoja juu ya faida za kutenga ardhi ya kilimo cha kuzalisha mbegu kwani kitapelekea halmashauri zetu kupata viwanda vya mbegu jambo litakalo chochea ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla,” alisema Bw.Mgalamo
Alisema Sagcot itaendelea kufanya uratibu kuhakikisha halmashauri zilizotajwa zinakwenda kuandaa ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya mbegu ambayo bila hiyo wakulima hawawezi kufanya uzalishaji wa mazao hivyo kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo nchini.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha wafanyabiashara wa mbegu Tanzania (TASTA) Bw.Baldwin Shuma alitaja mahitaji ya ardhi kwa uwekezaji wa muda mrefu kuwa ni hekta 35,000 na mahitaji ya muda mfupi ni hekta 17,610 ili kuweza kuzalisha mbegu na kuifanya nchi kujitosheleza kwa mbegu.
“Tunamakampuni ambayo yapotayari kuja kuwekeza kwenye sekta ya uzalishaji mbegu na kujenga viwanda vya kuchakata mbegu hapa nchini lakini changamoto kubwa imekuwa ni upatikanaji wa ardhi, hivyo kupitia kikao kazi hiki tunauhakika sasa halmashauri zetu zitaweka kipaumbele ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye kilimo,” alisema Bw.Shuma
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Bi.Patricia Kabaka alishukuru Sagcot kwa kuandaa kikao kazi hicho kwani kimeweza kuwaongezea maarifa zaidi hususani katika umuhimu wa kutenga ardhi kwa ajili ya kilimo na kuahidi watakwenda kufanyia kazi kwani ni fursa kwao katika kuengeza wawekezaji na uchumi wa Wilaya kukua.
“Nilijua Sagcot inafanya kazi katika mikoa ya nyanda za juu kusini tu, kupitia kikao hiki nimeelewa kuwa taasisi hii inafanya kazi kuhakikisha mageuzi kwenye sekta ya kilimo yanafikiwa nchi nzima,” alisema Bi.Kabaka
Kikao kazi hicho kimeratibiwa na Kituo cha kuendeleza kilimo Nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kwa udhamini wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...