Na Mwandishi wetu , NCAA.

Serikali imeboresha uratatibu wa kuandikisha wananchi wanaohama kwa hiari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwaandikisha katika ngazi ya kijiji wanapoishi tofauti na utaratibu wa awali ambapo timu moja iliyokuwa imeundwa na Serikali ilikuwa ikipita maeneo ya vijiji vyote ndani ya Hifadhi.

Kauli hiyo imetolewa na Serikali kupitia Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mangwala wakati akiaga kundi la nane lenye kaya 25, wananchi 132 na mifugo 259 wanaohamia kijiji cha Msomera Mkoani Tanga.

“Mwitikio kwa wanaojiandikisha umeongezeka sana, Serikali imeboresha utaratibu na kuanzia wiki ijayo tumepanua wigo kwa wananchi kupiga simu kwa mtendaji wa kijiji ambae atamuandikisha sehemu alipo, hii ni tofauti na ilivyokuwa awali kwa timu moja kuzungukia maeneo mbalimbali ndani ya eneo” Mangwala.

Mhe. Mangwala ameongeza kuwa baada ya mwananchi kuandikishwa na mtendaji wa kijiji, taarifa zitaunganishwa ngazi ya kata, tarafa hadi wilayani na baada ya hapo timu maalum itapita kwa ajili ya kufanya uthaminishaji wa nyumba na mali za mwananchi anayehama kwa ajili ya taratibu nyingine za Kiserikali.

“Ni imani ya Serikali kuwa maboresho tuliyoweka yataendana na kasi ya wananchi wanaotaka kujiandikisha kuhama kwa hiari ndani ya eneo la hifadhi na serikali yao imejipanga kuwahudumia kwa kufuata misingi ya haki, utu na kuwapatia huduma mbalimbali za kijamii wanakoenda” amesisitiza Mhe. Mangwala.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Needpeace Wambuya ameeleza kuwa Serikali kupitia NCAA inaendelea kuratibu zoezi hilo kwa umakini na itawahamisha wananchi hao kwa awamu ili kuhakikisha mtu anayehama anapata huduma za msingi anakohamia ikiwemo nyumba, mashamba ya kulima, malisho ya mifugo, majosho na huduma mbalimbali za kijamii.

Aidha amefafanua kuwa katika kuongeza ufanisi wa zoezi na kupunguza gharama za kuhamisha wananchi hao magari ya Serikali ndio yanayotumika kwa sehemu kubwa katika kusafirisha wananchi na mali zao.

Serikali inaendelea kuboresha maisha ya wananchi wanaohama katika hifadhi ya Ngorongoro kwenda eneo la Msomera lililoandaliwa kwa kuhakikisha kuwa huduma zilizokuwa zikikosekana Ngorongoro zinapatikana katika Kijiji hicho kwa kupata huduma stahiki kama watanzania wengine.

Hadi kufikia tarehe 8 septemba, 2022 zaidi ya kaya 183, zenye wananchi 926 na mifugo zaidi ya 5,300 zimekwishahamia Kijiji cha Msomera.




 




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...