Na Yeremias Ngerangera, Namtumbo
VIJIJI na shule wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma vimekamilisha ujenzi wa vyoo bora katika vijiji 15 na shule zake kwa awamu ya kwanza na ya pili ya mradi toka kuanzishwa kwake mwaka2013.
Akiongea kwenye moja ya mafunzo ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujenga vyoo bora, afisa afya wa kata ya Rwinga, Agrey Mwasansu alisema kuwa kila kaya inatakiwa iwe na vyoo bora ili kuepuka ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na kutokuwa na vyoo bora katika kaya .
Bwana Masasu aliwataka wananchi kujenga vyoo hivyo kwa lengo la kupunguza ugonjwa wa kuharisha ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na kukosa vyoo bora vya kutumia kwenye kaya .
Mwansasu aliwataka wananchi wa kijiji cha Rwinga kwenda kujionea baadhi ya vyoo vilivyojengwa na baadhi ya vijiji majirani vya Mgombasi,Likuyu, Litola na Namabengo kwa ajili ya kujiridhisha.
Mwenyekiti wa kijiji cha Rwinga bwana Musa Kambako aliwataka wananchi waliohudhuria mafunzo hayo kuitikia wito wa serikali wa kujenga vyoo bora ili kujinusuru na homa ya kuharisha .
Naye afisa elimu msingi wa wilaya hiyo bwana Loberto Mbilinyi alisema kuwa kupitia mradi wa SWASH shule 6 kati ya shule 10 zilizoingizwa kwenye mpango zimekamilisha ujenzi wa vyoo bora.
Alitaja shule ya msingi Mgombasi,Msindo ,Hanga zilikamilisha awamu ya kwanza ya mpango na shule ya msingi Mfuate,Kanjele na Njuga zilikamilisha ujenzi wake awamu ya pili ya mpango na awamu hii ya tatu mpango umeelekezwa ujenzi wa vyoo kwenye shule ya msingi Suluti,Kidugalo,Namanguli na Litete.
Mektides Chiwango mratibu wa mpango wa SWASH halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa shule za msingi alisema kuwa mradi huo unatekelezwa vizuri kwa kuwa wananchi na kamati za shule zinaonesha kushirikiana kwa kuzitumia fedha za mradi vizuri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...