Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MGANGA Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method amemtaka Afisa Lishe kushirikiana na viongozi wa kata pamoja na mitaa kuendelea kutoa elimu kwa wamama wajawazito pamoja na wananchi wote kujua umuhimu wa kuwahi kliniki kwaajili ya kujua maendeleo ya kiafya pamoja na kutumia vyakula vyenye lishe ili kuondoa udumavu na utapiamlo mkali.
Mganga Mkuu aliyasema hayo katika kikao cha tathimini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya kata robo ya kwanza (Julai – Septemba) 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Dkt. Method alisema kuwa suala la lishe bora ni jambo la muhimu ambalo kila mwananchi anatakiwa kulijua kwa sababu wajawazito wengi wamekuwa hawahudhurii hospitali. Alisema kuwa wajawazito wengi hawatumii vyakula vya lishe kitu ambacho kinawaletea matatizo wakati wa kujifungua. “Kinamama wote wanatakiwa wapatiwe elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa lishe pamoja na kwenda kliniki wakati wote wa ujauzito ili kuondokana na haya matatizo.
Wajawazito wamekuwa wakipoteza damu nyingi au kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Inatakiwa kama wataalamu wa afya tuhakikishe jambao hili la kutoa elimu katika kata na mitaa yetu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Hata kama mama atajifungua salama kama hatumii lishe bora basi mtoto atakuwa na utapiamlo mkali pamoja na udumavu” alisema Dkt. Method.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma, alisema kuwa katika kuhakikisha tatizo la utapiamlo linakuwa historia katika Jiji la Dodoma, uongozi wa kata na mitaa kwa kushirikiana na wahudumu wa ngazi ya jamii waendelee kufanya ufuatiliaji wa watoto walioibuliwa na utapiamlo mkali kwenye mitaa. Aidha, aliwataka kuhakikisha siku ya afya na lishe inafanyika kwa kila mtaa.
“Tunatakiwa kuondoa tatizo la utapiamlo mkali kwa watoto wetu kwa kuhakikisha watendaji wanasimamia vema uwepo wa program za uzalishaji wa chakula kwa wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo kwenye kata. Pia katika vituo vyote vya afya kunatakiwa kuwepo namba za watendaji wa kata ili kupata taarifa za watoto wenye utapiamlo hii itasaidia kujua jinsi gani ya kutatua tatizo hili. Lakini pia chumvi ambayo inatumika inatakiwa kupimwa ili kujua kama ina madini joto ndipo itumike” alisema Semeni.
Katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisisitiza kuwa kila kilichojadiliwa kifanyiwe kazi ili kuokoa jamii. Jambo la lishe lipewe kipaumbele kwa sababu wengi wao wamekuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu lishe. “Jambo hili tulisifanyie mzaa kabisa wengi wamekuwa wakipoteza maisha au watoto kuwa na udumavu pamoja na utapiamlo mkali kwa kutokuwa na elimu ya kutosha. Kwahiyo, tushirikiane sote katika jambo hili,” alisema Shekimweri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...