Na Dennis Gondwe, DODOMA
WATENDAJI wa kata katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuhakikisha utaratibu wa chakula kwa wanafunzi unafanikiwa kwa kiasi kikubwa ili kuwasaidia watoto kuondokana udumavu na kupandisha kiwango cha usikivu utakaowapelekea kufaulu vizuri wanapokuwa shuleni.
Agizo hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akisaini Mkataba wa utendaji kazi ya usimamizi wa shughuli za lishe na maafisa watendaji kata 41 wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya jiji hilo.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa lengo la mikataba hiyo ni kuboresha suala la hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii. “Lazima twende kwa kina zaidi ili chakula kipatikane kwa wanafunzi. Watendaji wote mtambue majukumu yenu na muongeze nguvu kwasababu mtoto akiwa na njaa hawezi kusoma wala kuelewa kile kinachofundishwa darasani. Kuna umuhimu hata wazazi kuelimishwa juu ya watoto wao hata kupata kifungua kinywa kabla hawajaenda shuleni ili apate nguvu, lakini kuna baadhi ya shule zimefanikiwa katika jambo hili. Kwahiyo, wale ambao hawajafanikiwa mnatakiwa kujifunza kwa wenzenu ni njia gani wamezitumia,” alisema Mafuru.
Akiongelea mtakata wa utendaji kazi ya usimamizi wa shughuli za lishe, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alisema kuwa unalenga kutatua changamoto ya lishe katika Jiji la Dodoma. “Mkataba huu unaosainiwa ni wa miaka minane hivyo, watendaji wa kata mnatakiwa kuhamasisha jamii kushiriki katika mpango wa utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni na kuwatambua wadau wa lishe wote waliopo kwenye kata na kuhakikisha wanawasilisha taarifa zao kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata,” alisema Juma.
Kiongelea nafasi ya madiwani katika utekelezaji wa masuala ya lishe, alisema kuwa madiwani wote wanatakiwa kuhakikisha wananchi wanatambua umuhumu wa kushiriki katika siku ya afya na lishe. Alisema kuwa siku hiyo inalenga kutoa elimu zaidi juu lishe bora kwa watoto kwasababu wanafunzi wengi wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na kukosa lishe.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa maafisa watendaji wa kata wanapokwenda kuwasainisha maafisa watendaji wa mitaa ni vizuri kualika na viongozi wengine katika tukio hilo. Uwepo wa viongozi wengine katika mitaa utawasaidia kuwa mashahidi na kurahisisha utekelezaji wa masuala ya lishe katika mitaa na kutoa matokeo yaliyokusudiwa, alisema.
Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru (katikati) akisaini Mkataba wa Lishe na Afisa Mtendaji Kata ya Madukani Tunu Dachi (kulia). Kushoto ni Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Andrew Method akifuatilia kwa umakini mkubwa tukio hilo
Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru akiagiza kutolewa chakula katika shule zote jijini Dodoma
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...