Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MBOGO Maji!!! Ihefu SC wameharibu rekodi ya Young Africans SC ya kutofungwa (Unbeaten) michezo 49, baada ya kuifunga timu hiyo mabao 2-1 katika uwanja wa Highland Estate, Mbarali mjini Mbeya ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC PL) msimu wa 2022-2023.
Mabao ya Ihefu SC yaliyoharibu rekodi hiyo ya Wananchi yamefungwa na Kiungo Never Tigere kwenye dakika ya 38’ ikiwa ni bao la kusawazisha katika mchezo huo, wakati bao la kwanza la Young Africans SC likifungwa dakika ya 8’ na Mlinzi wa timu hiyo, Yannick Litombo Bangala.
Mbogo Maji walienda mapumziko katika dimba lao la nyumbani kwa sare ya bao 1-1. Kipindi cha pili, Ihefu SC walirudi uwanjani kwa kasi na kupata bao la ushindi kwenye dakika ya 61’ kupitia kwa Mlinzi wao, Lenny Kissu ambaye aliunganisha ‘Krosi’ safi ya ‘kona’ ya Never Tigere.
Mara ya mwisho, Wananchi kupoteza mchezo, ilikuwa Aprili 26, 2021 ambapo walifungwa bao 1-0 na Azam FC kwenye dimba Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, bao lililofungwa na Mshambuliaji, Prince Dube.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...