MAONI NA USHAURI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA,
BIASHARA NA MAZINGIRA KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA
UWEKEZAJI TANZANIA WA MWAKA 2022
__________________________
1.0 UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99 (5) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020, naomba kuwasilisha Maoni ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira,
kuhusu Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 97 (1) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Viwanda, Biashara na Mazingira, iliupokea Muswada huu Mwezi
Septemba, 2022 baada ya kusomwa Bungeni mara ya kwanza tarehe 23
Septemba, 2022 ili iufanyie kazi, na tarehe 18 Oktoba, 2022, Waziri wa
Uwekezaji, Viwanda na Biashara alifika mbele ya Kamati na kutoa
maelezo kuhusu Malengo na Madhumuni ya Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, dhana ya Sheria ya Uwekezaji siyo dhana ngeni
katika mizania ya Sheria na Uwekezaji hapa Tanzania na nchi nyingine.
Nchi nyingi za Afrika kama vile Kenya, Rwanda na Afrika Kusini tayari
wana hii Sheria. Kwa nchi ya Kenya Sheria hii ilitungwa Mwaka 2004 na
inaitwa Investment Promotion Act Na.6 ya Mwaka 2004 ambayo
ilifanyiwa marekebisho mwaka 2021. Kwa nchi ya Rwanda Sheria
ilitungwa mwaka 2021na inaitwa Investment, Promotion and
Facilitation Act Na. 6 ya mwaka 2021.
Kwa nchi ya Afrika Kusini Sheria ilitungwa Mwaka 2015 na inaitwa
Protection of Investment Act, Na. 22 ya Mwaka 2015. Uingereza
2
Sheria hii ilitungwa tarehe 4 Januari, 2022 na inaitwa National Security
and Investment Act ya mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 97 (2) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni, 2020, Kamati ilitoa
matangazo katika vyombo vya habari na kuwaalika Wadau mbalimbali ili
waweze kufika mbele ya Kamati na kutoa Maoni yao kuhusu Muswada
huu.
Aidha, Wadau walifika mbele ya Kamati tarehe 19 Oktoba, 2022 na kutoa
maoni yao ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika Uchambuzi
wa Muswada huu.
2.0 MALENGO NA MADHUMUNI YA MUSWADA
Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza kutungwa kwa Sheria
ya Uwekezaji Tanzania Na. 9 ya mwaka 2022. Sheria inayopendekezwa
ina Madhumuni ya kuweka masharti ya Mazingira bora kwa Wawekezaji
Tanzania, kuweka Mfumo wa Kitaasisi kwa ajili ya Uratibu na Usimamizi
wa Uwekezaji nchini na kufuta Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka
1997.
Mheshimiwa Spika, utafiti unaonesha kuwa nchi nyingi duniani na zile
zinazotuzunguka zimefanya mapitio ya Sheria za Uwekezaji ili kuweka
mazingira bora na shindani kwa Wawekezaji ikiwa ni pamoja na
kuzingatia mabadiliko ya haraka katika Mifumo ya Kiuchumi duniani.
Mapitio hayo yamewezesha kuboresha utoaji wa huduma na uratibu kwa
Wawekezaji. Vile vile mapitio hayo yameimarisha utendaji wa Taasisi
zinazohusika na Uwekezaji katika nchi hizo katika kutoa Huduma Mahala
3
Pamoja kwa Ufanisi (True One Stop Centre) na kuzingatia ushiriki katika
uchumi wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020, Sura ya Pili
Ibara ya 22 Ukurasa wa 18-19 (a) - (L) Serikali iliwaahidi Wananchi
kuboresha mazingira ya Uwekezaji. Kwa kutaja mambo machache
Chama kiliahidi: -
(a) Kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa kuendeleza
Uwekezaji na kuvutia Wawekezaji wa ndani na nje kwa kushirikisha
Sekta Binafsi;
(b) Kuimarisha upatikanaji wa Ardhi ya Uwekezaji kwa kuhimiza
Mamlaka za Serikali kujenga maeneo ya Uwekezaji, kulipa fidia na
kuweka miundombinu ya Msingi ili kufanikisha Uwekezaji; na
(c) Kupitia upya taratibu za utoaji vibali vya ujenzi ili kuhakikisha
kwamba vibali hivyo vinatolewa ndani ya siku saba za kazi.
Aidha, kutokana na hamasa ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza na kufungua mipaka
ya uwekezaji nchini, nidhahiri kwamba Muswada huu unalenga kuweka
Mfumo Madhubuti na Endelevu ambao utaondoa vikwazo na dosari
zilizokuwa kikwazo kwa Wawekezaji nchini na hivyo kuwavutia
Wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Spika, Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Kuu
Tano zifuatazo: -
2.1 Sehemu ya Kwanza ya Muswada
Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kwanza ya Muswada inajumuisha
masharti ya utangulizi ikiwa ni pamoja na Jina la Sheria
inayopendekezwa, matumizi na tafsiri ya misamiati na maneno
mbalimbali yaliyotumika katika Muswada unaopendekezwa.
4
2.2 Sehemu ya Pili ya Muswada
Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Pili ya Muswada inaweka Mfumo
wa Kitasisi wa Uratibu na Uwezeshaji wa Wawekezaji nchini,
kuendelea kuwepo kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, kuenedelea
kuwepo kwa Kamati ya Taifa ya Uwekezaji, inaweka masharti
yatakayokiwezesha Kituo kuanzisha Mfumo Unganishi wa
Kielektroniki, Uanzishaji wa Bodi, Muundo na Majukumu yake,
Vyanzo vya fedha vya Kituo na Utaratibu wa utunzaji na ukaguzi
wa hesabu;
2.3 Sehemu ya Tatu ya Muswada
Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tatu ya Muswada inaweka
masharti mbalimbali ya Uwekezaji. Ikiwemo kuzitaka Tasisi za
Serikali kushirikiana na Kituo katika kutoa huduma kwa
Wawekezaji kupitia Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja. Aidha,
sehemu hii inaweka utaratibu wa maombi ya cheti cha Vivutio,
muda wa uhai wa cheti hicho na vivutio anavyoweza kupata
Mwekezaji. Vile vile sehemu hii inabainisha kuwa vivutio
vinavyosimamiwa na Sheria nyingine yoyote vitatolewa kwa mujibu
wa taratibu zilizoainishwa katika Sheria hizo;
2.4 Sehemu ya Nne ya Muswada
Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nne ya Muswada inahusu Haki
na Wajibu wa Serikali na Wawekezaji. Serikali inapewa haki ya
kusimamia shughuli za Uwekezaji ili kuhakikisha kuwa
zinaendeshwa kwa kuzingatia Misingi ya Sera na Sheria za nchi.
Kwa upande wa Wawekezaji wanatakiwa kutii Sheria za nchi,
kuendesha shughuli zao kwa namna inayolinda walaji, mazingira
5
na Usawa wa Kijinsia na kutoa taarifa kwa Mamlaka mbalimbali za
Serikali pale zitakapohitajika;
2.5 Sehemu ya Tano ya Muswada
Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tano ya Muswada inaainisha
masharti ya jumla yanayojumuisha makosa mbalimbali
yanayohusiana na masuala ya Uwekezaji na adhabu zake pamoja
na Mamlaka ya Waziri kutunga Kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora
wa Sheria inayopendekezwa. Shemu hii pia inafuta Sheria ya
Uwekezaji Tanzania ya mwaka 1997 pamoja na kuweka masharti
ya mpito kwa ajili ya masuala mbalimbali yaliyokuwa
yanasimamiwa na Sheria inayopendekezwa kufutwa. Miongoni
mwa masharti hayo ni kuendelea kutambuliwa kwa vivutio
vilivyotolewa na Mikataba iliyoingiwa na Wawekezaji chini ya
Sheria inayopendekezwa kufutwa.
3.0 UCHAMBUZI WA JUMLA WA MUSWADA
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Kanuni ya 24 (2) (a), (b), na (d) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020, Kamati ilifanya
uchambuzi wa kina wa Muswada huu wa Sheria kwa kupitia Vifungu
vyote 37 vya Muswada na kujiridhisha na Malengo na Madhumuni ya
Sheria inayotungwa katika Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilipokea maelezo ya Waziri wa Uwekezaji,
Viwanda na Biashara tarehe 18/10/2022 ambaye aliieleza Kamati
kinagaubaga kuhusu Malengo na Madhumuni ya Sheria hii.
Mheshimiwa Spika, ili kukidhi matakwa ya Kanuni ya 97 (2) ya Kanuni
6
za Kudumu za Bunge Toleo la Juni, 2020, tarehe 19 Oktoba, 2022,
Kamati ilikutana na kupokea maoni ya Wadau mbalimbali kutoka katika
Sekta ya Umma, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia na Mitandao ya Kijamii ili
kusikiliza na kupokea maoni yao kwa lengo la kuisaidia Kamati katika
uchambuzi wa kitaalamu wa Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea maoni mbalimbali ya Wadau
Kamati ilijipa muda wa kupitia na kuchambua maoni ya Wadau kwa kina
ili kujiridhisha na maudhui yake. Maoni ya Wadau kwa kiasi kikubwa
yameisaidia Kamati katika kufanya Uchambuzi wa Muswada na
hatimaye kutoa maoni kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 21/10/2022 Kamati ilikutana na mtoa hoja,
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili kushauriana naye kuhusu
hoja mbalimbali za msingi ambazo Kamati iliziona kutokana na
uchambuzi uliofanyika. Yapo maeneo ambayo Kamati ilikubaliana na
Serikali na Serikali ilikubali kuchukua Mapendekezo ya Kamati. Yapo
pia maeneo ambayo Serikali ilihitaji muda zaidi kwa ajili ya kufanya
majadiliano ya ndani na kuandaa jedwali la marekebisho.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Wadau waliochangia katika Muswada
huu wamekubaliana na Malengo na Madhumuni ya Muswada na
kuipongeza Serikali kwa hatua hii ya kutunga Sheria ya Uwekezaji
Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa
Muswada huu kwa kupitia Kifungu kwa Kifungu na baada ya kupokea na
kuchambua Madhumuni na Malengo ya Muswada huu Kamati iliona
kwamba kwa maslahi ya Sekta ya Uwekezaji Tanzania kuna haja ya
kuvifanyia maboresho Vifungu 37 vya Muswada huu kwa kutazama
7
mazingira tuliyonayo hapa Tanzania na kwa kutazama pia Sheria za
namna hii zilivyo katika nchi nyingine (International Comparative
Perspective).
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Vifungu vilikuwa na makosa ya Sarufi,
maana na mpangilio, tayari vimeingizwa katika jedwali la marekebisho la
Serikali. Kwa mfano, katika Ibara ya 2 (5) ya Muswada sentensi ‘’Bila
kujali Kifungu cha (1) Kituo kitawasaidia Wawekezaji wote, Kamati
imeshauri isomeke ‘‘Kituo Kitawahudumia’’. Serikali imeyapokea
mapendekezo ya Kamati na kuyajumuisha katika jedwali la
marekebisho.
Mheshimiwa Spika, Vifungu ambavyo vilihitaji kuboreshwa zaidi ni
kama ifuatavyo: - Kifungu cha 1 kuhusu Jina la Sheria, Kifungu cha Pili
kuhusu Matumizi, Kifungu cha 3 kuhusu tafsiri ya neno mtaji, Kifungu
cha 4, kuhusu kuendelea kuwepo kwa Kituo cha Uwekezaji, Kifungu cha
5 kuhusu malengo ya Kituo, Kifungu cha 6 Kuhusu majukumu ya Kituo,
Kifungu cha 9 kuhusu uanzishwaji wa Bodi, Kifungu cha 13 kuhusu
Maafisa na Wafanyakazi wengine wa Kituo, Kifungu cha 14 kuhusu
Ukomo wa Uwajibikaji kwa Wajumbe wa Bodi na Wafanyakazi, Kifungu
cha 18 kuhusu Kituo cha Huduma Mahala Pamoja, Kifungu cha 19
kuhusu Maombi ya Cheti na Usajili, Kifungu cha 20 kuhusu Uhai na
kufutwa kwa cheti cha vivutio, Kifungu cha 21 kuhusu Uratibu wa
uanzishwaji wa Taasisi za kibiashara, Kifungu cha 22 kuhusu Manufaa,
Kifungu cha 23 kuhusu manufaa kwa Uwekezaji wa Kimkakati au
Uwekezaji Maalum wa Kimkakati, Kifungu cha 26 kuhusu Wajibu wa
Mwekezaji, Kifungu cha 27 kuhusu Dhamana dhidi ya kurekebishwa au
kubadilishwa kwa manufaa, Kifungu cha 33 kuhusu Utatuzi wa
migogoro, Kifungu cha 34 kuhusu makosa na adhabu.
Aidha, Kamati inapendekeza kiongezwe Kifungu kimpya cha 38
8
kuhusu namna Sheria itakavyo wasaidia, kuwawezesha na
kuwalinda Wawekezaji Wazawa.
Mheshimiwa Spika, baada ya majadiliano ya kina kati ya Kamati na
Serikali, pande zote mbili zilikubaliana kufanya marekebisho kwa ajili ya
kuboresha Vifungu vyote vilivyokuwa na utata ili viwe bora zaidi.
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba
maoni na mapendekezo ya Kamati katika Muswada huu yamezingatia
Uchambuzi wa Kitaalamu wa Muswada huu uliofanywa na Kamati kwa
kushirikiana na Wadau mbalimbali waliotoa maoni yao kwenye Kamati.
4.0 MAONI NA USHAURI WA KAMATI
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali Kamati ilifanya Uchambuzi
wa Muswada Kifungu kwa Kifungu hatua hiyo iliwezesha kutolewa kwa
Maoni na Ushauri kwa Serikali kuhusu maboresho ya Vifungu vya
Muswada kama ifuatavyo: -
Maoni ya Jumla
Mheshimiwa Spika, Kamati ina maoni na mapendekezo ya jumla
yafuatayo: -
Hadhi ya Kituo cha Uwekezaji ilivyo kwa sasa haiwezeshi Mfumo
madhubuti wa Kitaasisi kwa ajili ya Uratibu na Uwezeshaji wa Uwekezaji
nchini, kwa sababu hiyo, Kamati inapendekeza Kituo cha uwekezaji
kipewe Mamlaka kamili badala ya kuendelea kuwa Wakala wa Serikali,
lengo ni kukipa nguvu ya utekelezaji wa majukumu yake;
Kamati inapendekeza kuwa baada ya Sheria hii kutungwa na Bunge
‘‘itafsiriwe katika Lugha ya Kiingereza ndani ya siku 30. Sababu ni
9
uhalisia wa Uwekezaji ambao kutokana na vivutio katika Muswada huu
Wawekezaji wengi wanatarajiwa kutoka mataifa mbalimbali.
Maoni na Ushauri wa Kamati kuhusu Vifungu vya Muswada
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 1 kuhusu Jina, Kamati inashauri
Jina la Sheria lisomeke ‘‘Sheria ya kuvutia na kulinda Uwekezaji
Tanzania ya mwaka 2022’’.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 3 cha Tafasiri, Kamati inashauri
kuongezeke Maneno ‘‘Ardhi’’ na ‘‘Hakimiliki’’ (Intellectual Property
Right) kwenye tafsiri ya neno ‘‘Mtaji’’.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 4 Kamati inashauri maelezo ya
pembeni yasomeke ‘‘Uwepo wa Kituo na Malengo’’.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 5 (1) Kamati inashauri Kifungu
hiki sasa kisomeke 4 (4). Lengo ni kuweka mpangilio mzuri wa Vifungu
vya Muswada.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 5 Kamati inashauri maelezo ya
pembeni yasomeke ‘‘Kamati ya Taifa ya Uwekezaji’’.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 5 (2) Kamati inashauri Kifungu
hiki sasa kisomeke 5(1), Kifungu cha 5(4) kisomeke 5(2), Kifungu cha
5(3) kibaki kilivyo na Kifungu cha 5(5) kisomeke 5(4) Lengo ni kuweka
mpangilio mzuri wa Vifungu vya Muswada.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Uwekezaji
katika Kifungu cha 5 (2), Kamati inashauri kwamba aongezwe ‘‘Waziri
10
mwenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki’’. Sababu ni kwamba Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki ndiye mwenye dhamana ya kusimamia Sera ya
Mambo ya Nje ambayo imejikita kwenye Diplomasia ya Uchumi. Huyu pia
ndiye msimamizi wa Mabalozi walioko nje ya nchi wanaohamasisha na
kuwavutia Wawekezaji wa Nje kuja kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu neno kitawasidia katika Kifungu cha 6 (1) (f),
Kamati inashauri lisomeke ‘‘kitawahudumia’’ Lengo ni kuleta maana nzuri
ya jukumu la Kituo.
Mheshimimwa Spika, katika Kifungu cha 9 (2) kuhusu Wajumbe wa Bodi
ya Kituo, Kamati inashauri kwamba Uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya
Kituo cha Uwekezaji uzingatie uwiano wa Kijinsia. Lengo ni kuona
kuwa uwakilishi wa Wanaume na Wanawake katika Wajumbe wa Bodi. Hii
itasaidia pia kujenga uwezo wa Wanawake katika nafasi za Uongozi na
Usimamizi bora wa utekelezaji wa Sheria hii kwa jicho la kutazama
makundi yote katika Jamii.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 9 (4) (b) (c) kuhusu muda wa
Wajumbe wa Bodi kushika nafasi zao, Kamati inapendekeza kwamba
muda wa Wajumbe kushika nafasi zao iwe miaka mitatu kwa Makundi
yote isipokuwa Mwenyekiti wa Bodi ibaki miaka Minne. Sababu ni
kuondoa tofauti kati ya Wajumbe kutoka Serikalini na wa Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kufuta kwa maelezo ya
Utangulizi Aya ya 13 kwa kufuta maneno ‘‘Sekretarieti’’ badala yake
yatumike maneno ‘‘Maafisa na Wafanyakazi wengine wa Kituo’’ ili
kuendana na maelezo ya Kifungu cha 13 cha Muswada huu.
11
Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kufuta kwa maelezo ya
Utangulizi Aya ya 14 kwa kufuta maneno ‘‘Ukomo wa uwajibikaji’’ na
badala yake yatumike maneno ‘‘Kinga dhidi ya madai kwa Wajumbe wa
Bodi na Wafanyakazi’’ ambapo pia yatatumika kwenye maelezo ya
pembeni ya Kifungu cha 14 cha Muswada.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 18(4) kuhusu muda wa utoaji wa
Leseni, Kamati inapendekeza muda wa Utoaji wa Leseni au Idhini uwe
siku 7 za kazi kama ilivyobainishwa kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2020 Sura ya Pili Ibara ya 22 (L) Ukurasa wa 19 wa Ilani.
Sababu ni kuwavutia Wawekezaji na kuondoa urasimu.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 20 (1) (a) na (b) kuhusu uhai na
kufutwa kwa cheti cha vivutio, Kamati inashauri Muswada utoe tafsiri ya
maana ya vivutio vya kifedha na visivyo vya kifedha ili vijulikane kwa
urahisi na Wawekezaji wa ndani na wa kigeni, Wasomi na wasio wasomi.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 22 (2) (d) na (e) kuhusu
manufaa, Kamati ilitoa maoni kuwa Muswada ufafanue utofauti wa magari
hayo na endapo gari la mwekezaji mwenye cheti cha vivutio lisilotumika
moja kwa moja kwenye mradi na lenye injini isiyozidi uwezo wa cc. 3000
lina sifa ya kupata vivutio. Baada ya kushauriana na Serikali, Serikali
ilikubali kwamba kinachoelezwa kwenye Aya ya (d) tayari kimejumuishwa
katika Aya ya (e), hivyo ilikubali kuondoa Aya (d) ili kuondoa
mkanganyiko kama inavyoonekana kwenye Jedwali la marekebisho ya
Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 26 kuhusu Wajibu wa
Mwekezaji, Kamati inashauri kiongezwe Kifungu (g) mara baada ya
Kifungu (f) kitakachosomeka (g) ‘‘kutunza taarifa za ukaguzi wa hesabu
12
na fedha za kila mwaka na kuwasilisha taarifa hizo Kituoni’’ na (h)
‘‘kutekeleza Mradi kwa mujibu wa Mpango Kazi uliokubaliwa wakati
wa maombi ya vivutio vya Uwekezaji’’.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 33 (1) kuhusu Utatuzi wa
migogoro, Kamati inashauri kuongeza maneno ‘‘ndani ya siku 60’’
katikati ya neno majadiliano na ili. Sababu ni kuweka ukomo wa muda
wa majadiliano.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 34 (1) Kamati inashauri
isomeke faini isiyopungua Milioni Tano na isiyozidi Milioni Kumi au
kifungo kisichopungua miezi sita au kisichozidi mwaka mmoja au
vyote kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha 34 (2), Kamati inashauri
kuongeza maneno ‘‘au mwajiriwa wa Wizara, Idara au Taasisi ya
Umma’’ katikati ya neno Kituo na neno ambaye.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliaarifu Bunge lako Tukufu kwamba
Serikali imekubali mapendekezo mengi ya Kamati na kuyaweka katika
jedwali la marekebisho lililowasilishwa katika Bunge hili. Serikali pia
imetoa maelezo ya ziada na ufafanuzi katika maeneo ya Muswada
ambayo Kamati ilihitaji ufafanuzi.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini kwamba uchambuzi wa Kitaalamu
uliofanywa katika Muswada huu utasaidia kupatikana kwa Sheria bora ya
kusimamia Sekta ya Uwekezaji nchini na kufungua ukurasa mpya kwa
Wawekezaji nchiniTanzania.
Kamati inapendekeza Serikali iongeze Kifungu cha 38 katika Muswada
kitakachoelezea namna ya kuwasaidia, kuwawezesha, na kuwalinda,
Wawekezaji Wazawa.
13
5.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana wewe kwa kutoa kibali ili
Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira iweze kuufanyia kazi
Muswada huu na kuipa fursa ya kuwasilisha maoni yake mbele ya Bunge
lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Waziri wa Uwekezaji,
Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashantu Kijaji (Mb), pamoja na Naibu
Waziri Mhe. Kigahe Exaud Silaoneka (Mb) kwa ushirikiano wao wakati
wa kuwasilisha maelezo ya Muswada huu na kutolea ufafanuzi wa hoja
mbalimbali zilizoibuliwa na Wajumbe wa Kamati.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru kwa dhati Wadau wote
walioshiriki na kutoa maoni yao katika Muswada huu ambayo kwa kiasi
kikubwa yamezingatiwa na Kamati. Naomba kutambua mchango wa
Wadau wafuatao: -
• Baraza la Kilimo Tanzania (ACT);
• Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS);
• Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS);
• Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC);
• Shirikisho la Wafanyabiashara na Wawekezaji Tanzania (Tanzania
Trade and Investment Coalition - TATIC),
• IResolve
• Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (Tanzania Private Sector
Foundation), na;
• Umoja wa Makampuni ya Simu Tanzania (TAMNOA).
14
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa naomba niwashukuru
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na
Mazingira kwa weledi na umahiri wao waliouonyesha wakati wa
kuchambua Muswada huu na hatimaye kutoa maoni na ushauri wa
msingi wa kuuboresha Muswada huu.
Naomba Majina yao yaingizwe kwenye Kumbukumbu ya Taarifa
Rasmi za Bunge (HANSARD).
1. Mhe. David Mwakiposa Kihenzile, Mb - Mwenyekiti
2. Mhe. Eric James Shigongo, Mb – Makamu Mwenyekiti
3. Mhe. Hawa Chakoma Mchafu, Mb - Mjumbe
4. Mhe. Martha Nehemia Gwau, Mb - Mjumbe
5. Mhe. Daudi Silanga Njalu, Mb - Mjumbe
6. Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Mb - Mjumbe
7. Mhe. Usonge Hamad Juma, Mb - Mjumbe
8. Mhe. Cecil David Mwambe, Mb - Mjumbe
9. Mhe. Eng. Ezra John Chiwelesa, Mb – Mjumbe
10. Mhe. Lucy John Sabu, Mb – Mjumbe
11. Mhe. Haji Makame Mlenge, Mb – Mjumbe
12. Mhe. Antipas Zeno Mgungusi, Mb – Mjumbe
13. Mhe. Askofu Josephat M. Gwajima, Mb – Mjumbe
14. Mhe. Daimu Iddi Mpakate, Mb – Mjumbe
15. Mhe. Issa Ally Mchungahela, Mb –Mjumbe
16. Mhe. Boniphace Mwita Getere, Mb -Mjumbe
17. Mhe. Maryam Omar Said, Mb, -Mjumbe
18. Mhe. Deodatus Philip Mwanyika, Mb - Mjumbe
19. Mhe. Zulfa Mmaka Omary, Mb –Mjumbe
20. Mhe. Jumanne Kibera Kishimba, Mb -Mjumbe
15
21. Mhe. Nancy Hassan Nyarusi, Mb – Mjumbe
22. Mhe. Shamsia Azizi Mtamba, Mb – Mjumbe
23. Mhe. Dkt. James Kimea Alfred, Mb - Mjumbe
24. Mhe. Salim Hassan Turky Toufiq, Mb - Mjumbe
25. Mhe. Kavejuru Eliadory Felix, Mb
26. Mhe. Hamis, Mohamed Mwinjuma mb, - Mjumbe
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa lakini si kwa umuhimu, namshukuru
Katibu wa Bunge Ndg. Nenelwa Mwihambi, ndc, kwa Uongozi thabiti
ambao umerahisisha utendaji kazi wa Kamati. Aidha, namshukuru
Mkurugenzi wa Idara ya Kamati za Bunge Ndg. Athuman Hussein, ndc,
Mkurugenzi Msaidizi Ndg. Michael Chikokoto, ndc, Makatibu wa Kamati
waliofanikisha kazi hii ambao ni Ndg. Angelina Langisi Sanga, na Ndg.
Nyamwanja C. Chilemeji, Wanasheria wa Bunge Ndg. Praisegod Zakaria
Lukio, Ndg. Evelyne Shibandiko, na Ndg. Nesta Kawamala na Msaidizi wa
Kamati Ndg. Modesta Kipiko kwa kuiwezesha Kamati kufanya kazi yake
kwa weledi mkubwa na kuhakikisha taarifa hii inakamlika kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
David M. Kihenzile (Mb),
MWENYEKITI, KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA. 01 Novemba, 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...