Na Said Mwishehe, Michuzi TV

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja imesema Tanzania ni nchi mojawapo iliyoko kwenye mpango wa kuresha uoto wa asili hekta milioni 5.2 wakati mpango wa Bara zima la Afrika ni kurejesha hekta za uoto wa asilimi milioni 100 ifikapo mwaka 2030.

Hivyo ameshauri ili kufikia lengo ambalo nchi yetu imejiwekea ni vema kila Mkoa nchini ukaweka mkakati wa kurejesha ukijani kwa kupanda miti kila mkoa na isiwe Mkoa wa Dodoma tu ambako kuna Kampeni ya Dodoma ya Kijani huku akifafanua ili kufanikisha lengo hilo jamii inatakiwa kushirikiana.

Akizungumza leo Novemba 22, mwaka 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa Warsha iliyowakutanisha wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya uhifadhi wakiongozwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) walipokutana kujadili na kuweka mikakati itakayowezesha kurejesha uoto wa asili(AFRI100).

“Lengo ni kurudisha uoto wa asili takribani hekta milioni 100 na Tanzania tumeweka ahadi ya kurejesha uoto wa asili hekta milioni 5.2 , sasa bila kuungana pamoja, bila kufanya jitihada mbalimbali , bila kuelimisha jamii hatutaweza kuzifikia hizi jithihada ambazo tumejiwekea kufikisha malengo.Lakini mimi naomba pamoja na kuwa na mabolozi wa mazingira tuweke mabalozi wengine kila mkoa ambao watakuwa wanatupa mrejesho wa kazi zilizofanyika.

“Na tuwe na mpango tutakaokuwa tunaujadili na kupeana taarifa kila wakati kwamba sasa hivi tumerejesha uoto wa asili kwa asilimia kadhaa.Ijapokuwa kwamba uoto wa asili utarejeshwa kwa mbinu mbalimbali hata wale wanaopanda maua, miti kando ya nyumba zao wote ni kundi linalojumuishwa katika jitihada hizi, sio miti tu ya TFS bali miti yote inayoonesha jitihada kurejesha uoto wa asili,”amesema Naibu Waziri Mary Masanja aliyekuwa mgeni rasmi kwenye Warsha hiyo.

Amesema kuna suala la mikoko, upandaji wa miti ya maua , majani ya asili ambazo zote hizo ni tijitahada za kurejesha uoto wa asili huku akitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Finland kupitia Ubalozi wake nchini wamekuwa na kampeni ya panda miti kibiashara kwa muda mrefu.

“Kamishna wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ameeleza kwa kirefu hatua ambazo tunaendelea kuzichukua na unapoangalia utabaini kumbe nchi yetu imeanza siku nyingi na kwamba baada ya kuona mabadiliko ya tabianchi yamejitokeza hatua mbalimbali zilianza kuchukuliwa kwa lengo la kurejesha uoto wa asili,”amesema Masanja.

Aidha Serikali imekuwa na jitihada mbalimbali za kuokoa maeneo ambayo yamevamiwa na leo hii kuna tarifa nzuri zikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameongoza mawaziri nane wa kistekta kwenda kuzunguka mkoa kwa mkoa kuokoa maeneo yaliyoharibika au kuvamiwa na wananchi.

“Kwa hiyo zote ni jitihada za kuhakikisha tunarudisha uoto wa asili ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.Lakini tumekuwa na Dodoma ya Kijani , kwanini iwe Dodoma peke yake, kwanini isiwe kila mkoa ?Tuwe na mkoa wa kijani na ndio Dodoma tumeanza.Kupitia kikao hiki nielekeze kila mkoa uwe na jitihada za kuwa na kijani yake, mfano Singida ya kijani, Kagera ya kijani.Kila mkoa uoneshe unajitihada gani kurudisha uoto wa asili na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.”

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Profesa Dos Santos Silayo amesema leo wamekutana kwenye mkutano huo mahususi kwa lengo la kuweka mikakati ya kufuatilia, kuratibu pamoja na kutoa taarifa kwamba shughuli zinazofanyika katika kurejesha uoto wa asili katika nchi yetu.

“Mtakumbuka kumekuwa na changamoto mbalimbali za kimazingira duniani zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na tangu mwaka 1979 ambapo dunia ilianza kubaini kwamba kuna ongezeko la joto duniani na kuanza kuchukua hatua kwa kufanya jitihada mbalimbali .Miaka 10 iliyopita katika jitihada za kuhakikisha maeneo ya ardhi yaliyoharibika yanarejeshewa uoto wake wa asili basi palifanyika mkutano mkubwa pale Born Ujerumani…

“Ambapo dunia kwa pamoja ilitangaza mkakati uliopewa jina Born Challenge uliweka azimio ifikapo mwaka 2030 basi Dunia iwe imefanya jitihada za kurejesha uoto takribani hekta milioni 350 duniani kote ambazo aidha zinaweza kupote au zimeharibika zirejeshewe uoto wake. Afrika ikachukua jukumu sehemu ya hiyo.

“Ahadi ambayo yenyewe itahakikisha katika nchi zake 54 itarejesha uoto huo kwa takribani hekta milioni 100 na ndipo ilipozaliwa neno AFRI100 yaani Afrika 100 , miaka ni hekta ambazo bara la Afrika limeweka azimio la kufikia sasa baada ya kufikia azimio hilo ikazitaka nchi wanachama na zenyewe ziweke maazimio na malengo yao ya kiasi gani kila nchi itachangia kufikia hekta milioni 100,”amesema .

Profesa Silayo amesema kwamba Tanzania ikapokea maelekezo na ikaweka lengo la kurejesha hekta milioni 5.2 kwa nchi nzima ifikapo 2030. “Lakini hadi sasa nchi za Afrika 32 zimeshaweka malengo yake na kwa ujumla wake zimeshafikia lengo la hekta milioni 128 kwa hiyo bado nchi takribani 22 hazijaweka malengo.

“Sasa lengo la Serikali ni nini katika hili? Tunataka kurejesha uto na kuzuai uharibifu wa maeneo ya misitu yanayoweza kuharibika iwapo hatutachukua hatua katika malengo haya tunafanya shughuli mbalimbali ikiwemo maeneo ya uoto kutoharibiwa,”amesema Profesa Silayo wakati wa warsha hiyo.


Mwandishi Ally Thabit (kulia) ambaye anachangamoto ya kutoona akiandika maelezo ya ufafanuzi aliyokuwa akipewa na Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos Silayo (katikati) baada ya kumalizika kwa warsha iliyowakutanisha wadau wa uhifadhi Novemba 22 mwaka 2022.

Ally alitaka kufahamu namna gani TFS na Serikali inaweka mkakati wa kuhakikisha watu wenye changamoto ya kutoona wanashiriki kwenye mikakati ya kurejesha uoto wa asili.Kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa TAFORI Dk. Revocatus Mushumbuzi wakifuatilia namna ambavyo mwandishi huyo anaandika kwa kutumia nukta nundu.



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja akiwa makini kufuatilia majadiliano yaliyokuwa yakiendelea kwenye Warsha iliyowakutanisha wadau wa uhifadhi nchini ambao pamoja na mambo mengine wameweka mkakati wa kurejesha uoto wa asili ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali ya Tanzania kurejesha uoto hekta milioni 5.2 ifikapo mwaka 2030.


Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa warsha hiyo.(PICHA NA SAID MWISHEHE-MICHUZI TV)


Mdau wa uhifadhi kutoka Community Forest Pemba Rahima Hamad Ali akiwa miongoni mwa wadau walioshiriki warsha hiyo akifuatilia majadiliano


Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo akizungumza kwenye warsha ya wadau wa uhifadhi iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.


Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos Silayo (kulia) akipitia maelezo kabla ya kwenda kuzungumza na wadau wa uhifadhi.Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja.


Wadau wa uhifadhi nchini wakiwa kwenye warsha hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.Mgeni rasmi kwenye warsha hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja(wan ne kulia) akiwa na viongozi wa taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa uhifadhi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa warsha iliyowakutanisha kujadili na kuweka mikakati ya kurejesha uoto wa asili nchini ambapo lengo la nchi ni kurejesha uoto hekta milioni 5.2.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja akizungumza kwenye warsha ya wadau wa uhifadhi iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa mikoa yote nchini kuanzisha kampeni ya kuwa ya kijani kwa kupanda miti ya aina mbalimbali kama mkakati mmojapo wa kurejesha uoto wa asili.


Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii Mary Masanja(watatu kushoto) ,Kamishna wa Uhifadhi-TFS Profesa Dos Santos Silayo (wa pili kulia) , Mkurugenzi wa TAFORI Dk.Revocatus Mushumbuzi wa kwanza kulia wakifuatilia warsha iliyowakutanisha wadau wa uhifadhi kujadili na kuweka mikakati ya kuresha uoto wa asili nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...