Haikuwa rahisi. Hivi ndivyo unaweza kusema baada ya utumishi uliotukuka wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Agnes Kijazi ambaye ametumikia nafasi hiyo tangu mwaka 2010.

Kwa sasa amestaafu, ama kwa hakika amefanikiwa kuibadilisha taswira ya TMA kutoka Wakala hadi Mamlaka na kutoka kutokuaminika na jamii katika masuala ya utabiri wa hali ya hewa hadi wakati huu ambapo jamii imekuwa ikizungumza na kufuatilia kwa karibu mamlaka hiyo kwa ajili ya masuala mbalimbali.

Utabiri wa hali ya hewa umekuwa ukitumika katika masuala mengi ikiwemo kilimo, uvuvi, usafiri wa anga, sekta za ujenzi na wananchi katika kazi zao mbalimbali.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho ni kuongezeka kwa matumizi ya huduma za hali ya hewa nchini na kuaminika kwa utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na TMA na hivyo kuongezeka kwa wadau wanaofuatilia na kutumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Dk. Kijazi anasema katika kipindi hicho wamefanikiwa kutekeleza programu za Shirika la Hali ya Hewa Duniani na wadau wengine wa maendeleo ambazo zimechangia katika kuboresha huduma za hali ya hewa ikiwa pamoja na kuboresha miundombinu ya hali ya hewa, kujenga uwezo kwa wataalam na watumiaji wa huduma za hali ya hewa.

Pia anasema kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kumechangia kuboresha huduma za hali ya hewa nchini kutokana na mamlaka hiyo kushiriki katika masuala ya kimataifa ya maamuzi ya hali ya hewa.

Dk. Kijazi anaeleza kuwa kitendo cha kununua rada saba na vifaa vya kisasa vya hali ya hewa kumeimarisha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa nchini.

"Tumeongeza uwezo wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kudahili wanafunzi kutokana na kukamilika kwa ukarabati wa miundombinu ya chuo na kuboreshwa kwa mazingira ya utoaji wa huduma kutokana na kukamilika kwa ukarabati wa vituo 15 vya hali ya hewa," anasema Dk. Kijazi.

Anaongeza kuwa; "wameongeza usahihi wa utabiri kutokana na jitihada za kusomesha wataalam wa hali ya hewa, matumizi ya vifaa vya kisasa vya kuandaa utabiri pamoja na kuongezeka kwa vituo vya kupima hali ya hewa."

"Tumefanikiwa kuongeza watumiaji wa huduma za hali ya hewa katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu baada ya Mamlaka kuongeza huduma zake kutoka bandari moja iliyopo Dar es Salaam na kuzifikia bandari nyingine sita zilizopo Zanzibar, Pemba, Tanga, Mwanza, Kigoma na Itungi," ameeleza.

Mafanikio mengine ni kuimarika kwa maandalizi ya utabiri wa maeneo madogo madogo kutokana na ununuzi wa kompyuta maalum yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa, uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa kuanza kufanyika nchini kupitia karakana ya TMA iliyopo JNIA hivyo kupunguza gharama za kuhakiki vifaa nje ya nchi.

TMA pia imefanikiwa kupata cheti cha ubora wa utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga (ISO 9001:2015), kuongezeka kwa vituo vya kupima hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe kutoka vituo saba mwaka 2010 hadi vituo 57 mwaka 2022.

Mkurugenzi huyo pia anasema idadi ya sekta zinazotumia huduma za hali ya hewa zimeongezeka na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Vilevile anasema wamefanikiwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato kutoka vinne hadi tisa na kwamba walifanya tafiti 33 zilizohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuzichapisha kwenye majarida ya kimataifa ya tafiti za kisayansi.

"Mafanikio mengine ni kuongezeka na kuendelea kutumiwa kwa data za muda mrefu za hali ya hewa na sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo ujenzi, kilimo na nishati," anaongeza.

Pia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imesaidia kuunda mifumo mbalimbali iliyorahisisha shughuli za uendeshaji na utoaji wa huduma pamoja na tovuti mbili za kutangaza shughuli za mamlaka hiyo.

TMA imekuwa ikifanya kazi zake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya maendeleo wa mwaka 2025, Mipango ya Taifa ya maendeleo ya miaka mitano, Ilani za Uchaguzi za Chama cha Mapinduzi (CCM), Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) na yale ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Dk. Kijazi anasema dira ya maendeleo inakusudia kuifanya Tanzania kuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo ili kufikia kipato cha kati, viwango vya juu vya viwanda, ushindani na maisha bora hivyo, TMA imechangia katika utekelezaji huo.

TMA imeboresha miundombinu ya hali ya hewa kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kufikia viwango vya kimataifa (ISO 9001:2015) na hivyo kukidhi matakwa ya huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga.

Mamlaka hiyo pia imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta mbalimbali ambazo zimekuwa ni kichocheo cha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ikiwemo miradi ya kimkakati ya reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHP).

"TMA imekuwa ikitoa huduma za utabiri na taarifa mahususi za hali ya hewa kwa wakandarasi wanaoendelea na shughuli za ujenzi katika miradi hiyo," anasema.

Anasema katika Mpango wa maendeleo endelevu hususan lengo namba 13 ambalo linahusisha kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, linatarajia kuwa ifikapo mwaka 2030 mataifa yatakuwa yameimarisha uwezo wao wa kukabiliana na athari zinazosababishwa na hali ya mbaya ya hewa pamoja na majanga ya asili hivyo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kujumuisha masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi katika sera na mipango ya taifa.

Katika kutekeleza hilo, TMA imeimarisha miundombinu ya hali ya hewa, kufanya tafiti za sayansi ya hali ya hewa, kushiriki katika shughuli za Jopo la Kimataifa linalosimamia sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa (IPCC) na kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

Hata hivyo, anasema pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto kadhaa ambazo zinakwamisha malengo ya TMA ikiwemo kuchelewa kukamilika kwa utengenezaji wa mitambo na vifaa vya hali ya hewa kutokana na athari za UVIKO -19.

Pia baadhi ya wadau wanatajwa kutokuwa tayari kuchangia huduma za hali ya hewa upungufu wa vifaa na mitambo ya hali ya hewa kwa ajili ya shughuli za uangazi hususan katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ambayo yanasababisha mabadilikoya mifumo ya hali ya hewa na upungufu wa wafanyakazi na kuongezeka kwa kasi ya kuhama kwa watumishi kutafuta maslahi bora.

Dk. Kijazi anasema wanaendelea kufuatilia wakandarasi wanaotengeneza rada na vifaa vya hali ya hewa ili vikamilike na kuwasili nchini, kuongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa na kuimarisha uangazi wa hali ya hewa katika Bahari na Maziwa Makuu.

"TMA itaendelea kuimarisha usalama wa abiria wa kwenye maji, shughuli za uvuvi pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali zikiwemo upakuaji wa mizigo bandarini na uvunaji wa gesi asilia, kuhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia sheria namba 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake," anasisitiza.

Vilevile wataendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa, kujenga jengo la Kanda ya Mashariki na Kituo cha kufuatilia matukio ya Tsunami, kuimarisha karakana ya vifaa vya hali ya hewa na kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini na kudhibiti na kuratibu huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kwa kuhakikisha taratibu na matakwa ya kisheria yanafuatwa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...