Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MWENYEWE wanamuita Jenerali Moses Phiri ni Mshambuliaji kinara kwa sasa katika Kikosi cha Simba SC, hususani msimu huu wa mashindano wa 2022-23 tangu asajiliwe, Phiri tayari amepachika mabao 10 katika michezo 15 ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu huu kwa upande wa Kikosi hicho cha Simba.

Baada ya kufika mabao 10 katika mbio za kuwania Kiatu cha dhahabu, Phiri tayari amemfikia Mshambuliaji kinara wa Yanga SC, Fiston Mayele ambaye na yeye ana mabao 10 wakiwa sawa sawa katika orodha ya upachikaji mabao.

Tangu asajiliwe na Simba SC msimu huu, Moses Phiri amekuwa Mchezaji hatari pindi afikapo katika lango la mpinzani, hilo amelithibitisha katika mchezo dhidi ya Coastal Union FC katika uwanja wa CCM Mkwakwani mjini Tanga, ambapo Wekundu wa Msimbazi walipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji wa uwanja huo, Wagosi wa Kaya.

Phiri ameweka kimyani mabao mawili peke yake katika mchezo uliokuwa wa ushindani muda wote wa dakika 90’. Phiri alifunga bao lake la tisa msimu huu na bao la kwanza kwenye mchezo huo kwenye dakika ya 53’ baada ya kupokea ‘pasi’ safi ya Master Clatous Chota Chama.

Moses Phiri alimpiga chenga safi Mlinzi wa kati wa Coastal Union, Khatibu Ally Kombo (Hero) na kuweka wavuni mpira huo. Katika dakika ya 61’ Phiri tena aliandika bao lake la 10 msimu huu na bao la pili kwa Simba SC dhidi ya Coastal baada ya kupiga ‘Penalti’ safi.

Katika mchezo huo, bao la tatu la Simba SC lilifungwa na Master Chama dakika ya 88’ baada ya Phiri kuanzisha shambulizi la hatari, lililomkuta Mshambuliaji John Bocco ambaye aligongesha mwamba mpira alioupiga kwa kichwa ambapo ulimkuta Chama katika eneo la wazi na kupachika wavuni mpira huo.
 
Simba SC imefikisha alama 34 katika michezo 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, na kukaa kileleni mwa msimamo wakati Yanga SC wana alama 32 katika michezo 13 na Azam FC wana alama 32 kwenye michezo 14.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...