Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA),CPA Nicodemus Mkama amesema Serikali kupitia mamlaka hiyo ina jukumu la kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia shughuli za maendeleo.

Mkama amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Faida (Faida Fund) ambayo ni sehemu ya maendeleo katika sekta ya fedha hususan masoko ya mitaji hapa nchini.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali huku Waziri, Ofisi ya Rais - Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi.

“Masoko ya mitaji ni sehemu ya mfumo wa sekta ya fedha unaowezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za muda mrefu, yaani zaidi ya mwaka mmoja, kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.

“Fedha za kugharamia shughuli za maendeleo hupatikana kwa kuuza hisa za kampuni (shares); hatifungani za kampuni (hatifungani za Serikali na vipande katika uwekezaji wa pamoja. Hapa nchini, masoko ya mitaji yanaendelezwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),”amesema Mkama.

Ameongeza kadiri Taifa letu linavyosonga mbele katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 unaolenga kujenga “Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”, mahitaji ya rasilimali fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii na uchumi, hususani miundombinu yanaongezeka.

Amefafanua ili kufanikisha azma hiyo kunahitajika uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya fedha, ikiwa ni pamoja na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja kama Faida Fund. Aidha, uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya mitaji unachangia utekelezaji wa Sera za Ukwasi katika Uchumi.

Pia kuongezeka kwa akiba hapa nchini; kupanuka kwa uwekezaji unaoleta ongezeko la ajira; Mapato kwa njia ya kodi kwa Serikali na kuinua kipato cha watanzania kwa ujumla huku akifafanua Oktoba 17 2022, (CMSA ilidhinisha Waraka wa Matarajio na Mkataba wa kuendesha Mfuko wa Faida.

“Idhini ilitolewa na CMSA baada ya Watumishi Housing Investments kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya uanzishaji na uendeshaji wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.

“Faida Fund ni mfuko ambao umekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Uwekezaji wa Pamoja. Faida Fund ni mfuko unaoendeshwa na taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) ambaye ni Meneja wa Mfuko (Fund Manager) na Benki ya CRDB ambaye ni Mtunza Dhamana wa Mfuko (Custodian).

“Lengo kuu la Mfuko wa Faida Fund ni kuhamasisha wawekezaji wadogo, wa kati, na wakubwa kuunganisha nguvu zao na kuwekeza kwa pamoja ili kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta ya fedha.Malengo ya Mfuko wa Faida ni kuwawezesha watanzania kunufaika na uwekezaji katika masoko ya fedha.”

Akieleza zaidi amesema mauzo ya vipande katika Mfuko wa Faida Fund yalifunguliwa Novemba 1,2022 na kufungwa Desemba 31, 2022.Kiasi cha fedha Sh. bilioni 12.95 kimepatikana, ikilinganishwa na Sh. bilioni 7.5 zilizotarajiwa kupatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 173.

Aidha mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi yanayotolewa na Serikali kupitia CMSA) ambayo imeidhinisha kushusha kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji wa Mfuko wa Faida Fund kutoka Sh. milioni moja hadi Sh.10,000 na na hivyo kuwezesha ushiriki wa wawekezaji katika Mfuko wa Faida Fund, ikiwa ni pamoja na wananchi wenye vipato vya chini, kati na vikubwa, taasisi na kampuni.

Pia mazingira wezeshi yanayotolewa na Serikali yamekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 8.1 na kufikia Sh.trilioni 34.01 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022, ikilinganishwa na Sh.trilioni 31.42 kipindi kilichoishia Desemba 2021.

Thamani ya uwekezaji katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja imeongezeka kwa asilimia 63.86 na kufikia Sh. trilioni 1.22 katika kipindi kilichoishia Disemba 2022, ikilinganishwa na Sh.bilioni 744.93 katika kipindi kilichoishia Disemba 2021.

Kwa mantiki hii, leo unapozinduliwa Mfuko wa Faida Fund, Jumla ya thamani ya uwekezaji katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja itafikia Sh. trilioni 1.35, na jumla ya thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji itafikia Sh.trilioni 34.14.

  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA),CPA Nicodemus Mkama akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfuko wa Faida Fund kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...