Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Abas Kayanda (katikati), ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi katikati,akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mbio za Kilimanjaro International Marathon  2023 kwa Mkoa wa Kilimanjaro katika Ukumbi wa  Kibo Palace Hotel Moshi Mjini,kulia kwake ni Meneja Mkuu wa Mauzo wa kampuni ya TBL Group kanda ya kasikazini Neema Patrick, Katibu Tawala wa Mkoa Sara Faraji,Mkurugenzi wa kampuni ya Tigo Kanda ya kaskazini Henry Kinabo. kushoto kwa mgeni rasimi ni Kamanda wa Polisi Kilimanjaro Simon Maigwa,Mkurugenzi wa Kibo Palace Hotel, Vincent Laswai,Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Moshi Mjini Faraji Swai.
Kaimu Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Abbas Kayande akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio ndefu zijulikanazo kama Kilimanjaro International Marathon  2023 mjini Moshi hivi karibuni
Meneja Mkuu wa Mauzo wa TBL Group Kanda ya Kaskazini, Neema Patrick akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kilimanjaro International Marathon
Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo

MBIO ndefu za kimataifa za Kilimanjaro International Premium Lager Marathon kwa mwaka wa 2023 zimezinduliwa rasmi Alhamisi, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro. Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 26, 2023.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Abbas Kayande, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Klilimanjaro (RC) Nurdin Babu, amesema mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimepiga hatua kubwa katika kukuza michezo hapa nchini na kwamba maadhimisho ya miaka 21 tangu kuanzishwa kwake ni taswira halisi ya jinsi waandaaji na wadhamini wa mashindano walivyo makini katika kuhakikisha mafanikio hayo yanadumu kwa muda mrefu.

“Mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa aliagiza waandaaji wa Kilimanjaro Marathon ambapo pia yanatangaza utalii wa Tanzania kuanza kutumia jina ambalolitaonesha kuwa mbio hizi ni za kimataifa na kweli mmeitikia wito huo na sasa mashindano haya yanajulikana kama Kilimanjaro International Marathon”, amesema na kuongeza, uamuzi huo ni muhimu kwa Taifa haswa ikizingatiwa ya kuwa mashindano haya yanajulikana kimataifa linalowavutia washiriki wengi kutoka nchi nyingi duniani.

“Mbali na kushiriki mbio hizi, washiriki pia watapata fursa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kama vile kupanda Mlima Kilimanjaro, kutembelea hifadhi zetu za Taifa, mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na Zanzibar,” amesema RC Babu.

Amesema Serikali inajivunia kuhusishwa kwake na mbio za Kilimanjaro International Marathon, moja ya mashindano makubwa ya kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambayo mwaka huu inatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 12,000 kutoka zaidi ya nchi 55 duniani kote.

“Mbio za Kilimanjaro Marathon zimechangia kwa kiasi kikubwa kukuza utalii wa michezo na hii imesaidia sana Serikali katika azma yake ya kukuza sekta ya utalii nchini na sera ya Taifa ya utalii kwa ujumla”, amesema na kuongeza kuwa uongozi wa Serikali mkoani Kilimanjaro utahakikisha usalama unakuwepo mkoani humo kabla wakati na baada ya mashindano hayo.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza wadhamini wote wa mbio hizi wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager (42km), Tigo Half Marathon (21km) na Grand Malt 5km Fun Run kwa michango yao mikubwa, bila ya nyinyi pamoja na wadhamini wenza mashindano haya yasingekuwa na msisimko tunaouona sasa”, amesema, ambapo alitoa wito kwa washiriki wa Wakitanzania kujiandaa vyema na tukio hilo la kimataifa ili waweze kufanya vizuri.

Aidha Kayande alitoa pongezi zake za dhati kwa wadhamini wengine wa mashindano hayo ambao amesema ni pamoja na Simba Cement, Kilimanjaro Water, TPC Sugar, Total Energies, kampuni ya ulinzi ya GardaWorld Security, Keys Hotels Kibo Palace Hotels na CMC Automobiles.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kilimanjaro Premium Lager, Meneja Mkuu wa Mauzo wa TBL Group Kanda ya Kaskazini, Neema Patrick, amesema wanajivunia kudhamini mbio hizo kwa mwaka wa 21 mfululizo. “Jambo limetufanya kuwa moja ya wadhamini waliofadhili matukio ya michezo kwa muda mrefu na kwa mafanikio makubwa huku tukihamasisha maendeleo ya mchezo wa riadha, ukuaji wa utalii na utamaduni Mtanzania kwa ujumla”, amesema.

Ameendelea kusema kuwa mwaka huu wadhamini hao wamejipanga vyema kwa ajili ya mashindano ya 21 ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon na kwamba wametenga shilingi milioni 22,760,000 kwa ajili ya zawadi mbalimbali.

Ametoa wito kwa washiriki kujiandikisha mapema ili kuepuka msongamano wa dakika za mwisho, ambapo amesema usajili huo unafanyika kupitia tovuti www.kilimanjaromarathon.com na kupitia TigoPesa kwa kupiga *150*01#.

Aidha ametoa wito kwa washiriki wa mbio za kilomita 5 maarufu kama mbio za Burudani kujiandikisha mapema kwani idadi iliyopangwa ya washiriki ni ndogo tena.

Pia ametoa wito kwa wadhamini wenza katika mashindano hayo kujiandikisha kwa ajili ya mashindano ya ushirika ambapo watapata kukimbia kama vikundi na kwamba waandaaji watatoa muda maalum kwa ajili ya ushiriki wa vikundi ili kupata washindi katika kitengo hicho cha mashindano. “Ushiriki wa makundi kupitia wadhamini wenza ni njia moja wapo ya kutuleta wafanyakazi na wadhamini wote pamoja sambamba na kuboresha afya zetu”, amesema.

Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo amesema, “Kama wadhamini wakuu wa kitengo cha mbio za 21km, (Tigo Kili Half Marathon), tunafurahia uzinduzi toleo la 2023 la mbio hizi ambazo zimepata heshima kubwa hapa nchini na duniani kote kwa sasa”, amesema na kuongeza,

"Nichukue fursa hii kuendelea kuwahimiza wanaotarajia kushiriki kujiandikisha kupitia Tigo Pesa kwa kupiga *150*01# kisha uchague Lipa Kwa Simu ili kupata namba zako za uendeshaji kabla.

Zaidi ya hayo, amesema Tigo inafuraha kuendeleza mradi wake wa kupanda miti wakati wa msimu wa mbio hizo unaojulikana kama Tigo Green For Kili ikiwa ni jitihada na mchango wa kampuni hiyo katika kuhifadhi mazingira ynayozunguka Mlima Kilimanjaro.

Kwa upande wao waandaaji wa mbio hizo wametoa wito kwa wanaotarajia kushiriki mbio hizo kutumia muda uliosalia kujiandikisha kabla zoezi la usajili kufungwa ifikapo Februari 6, 2023. “Tunasisitiza umuhimu katika swala hili kutokana na taratibu zilizowekwa zinazohusiana na usimamizi ambao utazingatia idadi ya washiriki, ambazo ni pamoja na usambazaji wa maji, usalama wa washiriki, usalama katika njia watakazotumia na usalama wakati wa mbio hizo kwa ujumla”, imesema sehemu ya taarifa ya waandaaji wa mbio hizo.

Aidha taarifa hiyo ya waandaaji imeendelea kusema kuwa tukio hilo litatoa mchango wa hisani utakaolenga kuchangia shirika la hisani la Tumaini la Maisha (TLM) ambapo lengo kuu la mchango huo litakuwa ni kumfikia kila mtoto wa Tanzania anayeugua saratani, ili wapate ya saratani ya hali ya juu bila malipo ili waweze kuendelea na maisha yao vyema.

Mbio za Milimanjaro International Premium Lager Marathon huandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa na Executive Solutions Ltd.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...