-Azungumzia ahadi ya Waziri Bashe, migogoro ya mipaka

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

MBUNGE wa jimbo la Mvomero mkoani Morogoro Jonas Van Zeeland amewasilisha taarifa ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo yamefanyika katika jimbo hilo kutokana na mabilioni ya fedha ambayo yametolewa na Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza leo Januari 29,2023 mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo ambaye ameambatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Sophia Mjema, Mbunge huyo amesema pamoja na mambo mengine mwaka jana wamepokea fedha Sh.bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 107 lakini pia wamepokea Sh. Bilioni 1.3 kwa ajili ya vyumba 65 na vyumba hivyo vimekamilika na watoto wanasoma.

Kuhusu sekta ya afya amesema katika Kata ya Dakawa kuna ujenzi wa vituo vya afya na wameshapokea Sh.milioni 250 na wanategemea tena kupokea Sh.milioni 250 kumalizia kituo cha afya , lakini wanaendelea kumshukuru Rais Samia kwani kuna   Hospitali ya Wilaya ya Mvomero ujenzi wake unaendelea na tangu kuanza kwa ujenzi huo hadi sasa wameshapokea zaidi ya Sh.bilioni 4.3 .

“Lakini tunaendelea na ujenzi wa zaidi ya vituo vitatu na kwenye upande wa maji hapa tulipo Dakawa tuna  mradi mkubwa wa maji wa zaidi Sh.bilioni 2.3 na hivi ninavyozungumza tayari mkandarasi amepata na atakuja kuanza kazi.Aidha tulikuwa na mradi wa maji wa Sh.milioni 120 katika kijiji cha Mtakuja ambao umekamilika na kazi iliyobakia itakuwa ni kusambaza maji hapa Dakawa

“Pia tumepokea Sh.milioni 100 kwa ajili ya Kitongoji cha Sokoine na hivi karibuni kuna mwandishi wa habari alitoa video clips  inayoonesha binadamu wakinywa maji na wanyama , nikazungumza na Waziri wa Maji ameshatupa Sh.milioni 100 na hivi ninavyozungumza na wewe tumeshachimba kisima kirefu cha maji na maji yameeanza kutoka na kazi  iliyopo sasa ni kazi ya mkandarasi kuweka matanki na kusambaza maji.

“Watu wa Sokoine  tatizo la maji litakuwa historia  wakati katika upande wa barabara hapa tulipo Dakawa kuna lami ujenzi unaendelea na tumepata Sh.milioni 500 tunajenga lami kipande cha kilometa moja na hivi karubini tumepata fedha Sh.milioni 500 kwa ajili ya kujenga barabara ya kiwango cha lami kingine,”amesema na kuongeza lakini wamepata fedha nje ya bajeti zaidi ya Sh.bilioni 2 ambazo zinatumika kufungua barabara ambazo hazijawahi kutengenezwa tangu nchi ipate uhuru.

Kuhusu kilimo, Zeeland amesema kuwa asilimia 90 ya wananchi wa Dakawa wanajihusisha na kilimo cha umwagiliaji na kwenye skimu ya umwagiliaji walipokea zaidi ya Sh.bilioni 22 kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji na miundombinu hiyo imekamilika na wakulima wanafanya shughuli zao zinakwenda kama kawaida.

“Lakini tuna Skimu ya umwagiliaji iko Lubindo tulipokea zaidi ya Sh.milioni 900 na kitu lakini skimu ile imekamilika haijafunguliwa kuanza kazi.Katibu Mkuu wa Chama chetu  yapo mengine napambana nayo mwenyewe lakini hii skimu ya Lubindo naomba ikikupendeza unisaidie kupambana ili ifunguliwe.

“Skimu ile imetumia fedha nyingi karibia Sh.bilioni moja lakini inachangamoto ndogo ambazo inafanywa isifunguliwe , hivyo Katibu Mkuu unaweza kukaa na wadau wa eneo lile pamoja na viongozi walioko kutatua mgogoro uliopo.Kwa miaka mitatu wananchi wanaangalia eneo lile ambalo limekamilika lakini halijafunguliwa,”amesema Zeeland.

Ametumia nafasi hiyo kueleza katika eneo hilo la Dakawa kuna eneo lenye ukubwa wa hekta 1000 na alishamuomba fedha Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambaye aliahidi kumpatia Sh.bilioni 2 lakini fedha hizo hazijatolewa hadi sasa na inakwenda mwaka wa pili.

“Ndugu Katibu Mkuu naomba nikubebeshe huo mzigo unisaidie Skimu ya Dakawa .Pamoja na hayo kuna changamoto kwenye eneo la ardhi ambako kumekuwa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambalo limekuwepo kwa muda mrefu lakini tunaamini litakwisha.

“Tatizo lingine hapa Mvomero ni migogoro ya mipaka , kuna migogoro mikubwa sana ya mipaka inayosababisha katika baadhi ya maeneo ya vijiji watu kushindwa kufanya shughuli za kilimo lakini tumefikisha malalamiko kwa Kamishna wa ardhi mkoa na wameahidi kuja kushughulikia,”amesema.

MBUNGE wa jimbo la Mvomero mkoani Morogoro Jonas Van Zeeland  akiwasilisha taarifa ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imefanyika katika jimbo hilo kutokana na mabilioni ya fedha ambayo yametolewa na Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan mbele ya Katibu MKuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo wakati wa kikao cha shina no 18 Mikoroshini,katika kata ya Wami-Dakawa Wilayani Mvomero .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...