Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amosi Makalla ambaye ni Shabiki mkubwa wa timu ya Simba, amesema kuwa mashabiki wa timu hiyo wanaodai kiasi cha fedha Shilingi Bilioni 20 kutoka kwa Mwekezaji, wengi wao hawasaidii timu hata wakati ikipitia kipindi kigumu cha ukata wa fedha.

RC Makalla ambaye alikuwa Mgeni rasmi wa Mkutano Mkuu wa timu hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, amesema kuwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuacha kubezana ili kufikia malengo. 

“Kuna watu wanakomaa wanasema wanataka Bilioni 20 kutoka kwa Mwekezaji, wanakomaa kabisa, lakini watu hao ukiwaambia watoe hata mchango wa Shilingi Elfu tano kwenye Kundi la ‘WhatsApp’ hawatoi, ukiambiwa hata Katoni tu ya Maji wawapelekee Wachezaji, Bunju hawawezi”, amesema RC Makalla 

Makalla amesema mafanikio ya sasa yaliyopatikana katika Klabu hiyo, yalipatikana kwa ushirikiano uliotukuka baina ya viongozi wote wa Klabu sanjari na wananchama, mashabiki wote.

“Hiyo ndio maana ya Nguvu Moja ambayo ni kaulimbiu ya Klabu, na ndio inatakiwa siku zote ili kufanikiwa na kufika mbali zaidi. Nakumbuka kuna kipindi timu ilipitia wakati mgumu tulikuwa tunatembeza Bakuli kutafuta fedha, wakati huo timu ilitoka Tunduma ikifika Dar es Salaam inatakiwa kwenda Zanzibar ilibidi tuanze michango ili timu isafiri,” amesema Makalla 

Hata hivyo, Makalla amewataka wanachama wa Klabu hiyo kuchagua Viongozi wanaowataka na wenye malengo na timu ili kuhakikisha timu hiyo inafika malengo yake ya kufika mbali zaidi, ikiwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali nchini pamoja na mashindano mengine ya Kimataifa.

“Vijembe vya Kampeni viishie getini, Viongozi mkichaguliwa hakikisheni mnashirikiana sanjari na kushirikiana na wanachama, mashabiki wote wa Klabu na wananchama hakikisheni mnachagua Viongozi ambao watawapeleka kwenye mafanikio,” amesema Makalla.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...