-Spika Tulia ataja maeneo yatakayonufaika na ushirikiano huo. Wabunge, wafanyakazi wa Bunge kunufaika na mafunzo

-Utamaduni na Utalii wa Tanzania watangazwa


TANZANIA na India kupitia Mabunge ya nchi hizo wamekutana na kujadili ushirikiano baina ya Mabunge hayo pamoja na ushirikiano zaidi baina ya nchi hizo mbili kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, kilimo, maji na afya kwa manufaa ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza leo katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na ugeni ulioongozwa na Spika wa Bunge la Wananchi wa India 'Lok Sabha' Mh. Shri Om Birla Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema, wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kibunge baina ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la wawakilishi Zanzibar pamoja na Bunge la Wananchi India pamoja na fursa za uwekezaji na kiuchumi zitakazonufaisha Tanzania na India.

Kuhusiana na masuala ya Kibunge, Dkt. Tulia amesema kuwa wamejadili mahusiano yaliyopo baina ya mihimili hiyo miwili na kutumia chuo cha mafunzo cha India kwa wabunge na wafanyakazi wa Bunge nchini kupata mafunzo.

"Tumejadili juu ya mahusiano yaliyopo baina ya Mabunge kwa nchi hizi mbili pamoja na kuyainua zaidi na Spika hapa ameeleza utayari wa Bunge la Wananchi wa India kushirikiana na baraza la wawakilishi Zanzibar na Bunge la Tanzania katika eneo hilo la mafunzo.'' Amesema.

Aidha amesema India ikifahamika kama Mama wa Demokrasia ilileta ubalozi wao 1961 kabla ya kupata uhuru na wameleta mashirikiano imara katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Akifafanua sekta muhimu ambazo zimenufaika na ushirikiano huo Dkt. Tulia amesema ni pamoja na sekta za kilimo, maji, afya na teknolojia.

"Spika wa Bunge la Wananchi wa India amesisitiza matumizi ya teknolojia katika kilimo na tunaamini mazungumzo yataleta tija kwa mataifa haya mawili...Tunafahamu Tanzania Bara inatekeleza miradi mikubwa wa maji katika Miji 28 kwa thamani ya shilingi milioni 500 dola za kimarekani fedha ambazo India imeshirikiana na Tanzania ili kuweza kuzipata na visiwani Zanzibar kuna miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa kupitia ushirikiano huu, tunashukuru." Amesema.

Aidha kuhusiana na mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria na kuyapeleka katika mikoa ya Tabora, Shinyanga na maeneo jirani Spika Tulia amesema, India ilitoa fedha zaidi milioni 268 kama sehemu ya utekelezaji wa mradi huo ambao umekamilika na kuzinduliwa na Serikali.

Kuhusiana na ushirikiano baina ya Nchi hizo katika sekta ya afya Dkt. Tulia amesema wamezungumzia ushirikiano zaidi ya watanzania kwenda kutibiwa nchini India na madaktari bingwa kuja nchini katika hospitali ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa huduma na kuondoka.

"Tumejadili kwa kina kuhusu sekta ya afya tunafahamu sio watanzania pekee katika ukanda huu wanakwenda India kwa ajili ya matibabu, tumejadili kuweka mahusiano ya karibu zaidi ili teknolojia ya matibabu, madaktari zitengenezewe mazingira kwa Tanzania kuwa kitovu cha matibabu kwa Nchi jirani.' Ameeleza.

Spika Tulia amesema, katika ushirikiano wa kibiashara Tanzania imekuwa ikipeleka mazao ya chakula nchini India na wao wamekuwa wakileta bidhaa nyingi nchini kupitia usafiri wa anga ambapo Air Tanzania inaenda moja kwa moja kutoka Tanzania hadi Mumbai, India.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Wananchi wa India 'Lok Sabha' Shri Om Birla ameeleza kuwa ushirikiano wa mihimili hiyo miwili baina ya Tanzania na India ni mkubwa na wamekuwa wakishauriana na kushirikisha fursa mbalimbali ambazo zitanufaisha mataifa hayo mawili ikiwemo ya wabunge na wafanyakazi wa Bunge Tanzania kupata mafunzo kupitia chuo Chao.

Ameeleza maeneo ya kilimo, elimu, afya pamoja na uwekezaji yamejadiliwa na yatafanyiwa kazi ili kujenga uchumi imara pamoja na kudumisha mahusiano hayo.

Spika Shri amesema uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na India ni thabiti na wamejadiliana namna ya kuboresha zaidi uhusiano huo.

Kwa mara ya mwisho Tanzania ilipokea ugeni wa Bunge kutoka India takribani miaka 50 iliyopita na Leo Januari 18 Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamepokea ujumbe huo ulioongozwa na Spika wa Bunge la Wananchi wa India, Wabunge na Katibu wa Bunge hilo la Lok Sabha.

Kupitia ugeni huo Tanzania imepata fursa ya kutangaza utamaduni na vivutio vya utalii ambao Spika na wageni aliombatana nao watatembelea kivutio pendwa ulimwenguni cha Serengeti na kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya Tanzania.







Matukio mbalimbali kwenye picha baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Tulia Acksoni alipokutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Wananchi wa India Shri Om Birla leo Januari 18,2023 jijini Dar es Salaam.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Tulia Ackson ( wa pili kulia) akisalimiana na Spika wa Bunge la Wananchi la India Shri Om Birla (kushoto) baada ya kukutana katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam leo Januari 18,2023.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Tulia Ackson ( kushoto) akigonga glasi na Spika wa Bunge la Wananchi wa India Shri Om Birla (kulia) leo Januari 18,2023 baada ya kukutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo yenye lengo la kujadili masuala mbalimbali

Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson akifafanua jambo baada ya kukutana na Spika wa Bunge la Wananchi wa India Shri Om Birla leo Januari 18,2023 jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...