NA BALTAZAR MASHAKA,MULEBA

WANANCHI zaidi ya 9000 wakiwemo wafanyabiashara katika Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba,wameondokana na adha ya ukosefu wa usafiri wa uhakika baada ya Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd ya jijini Mwanza,kufungua fursa ya usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.

Kampuni hiyo imeanzisha usafiri wa boti iendayo kasi ya MV Rafiki-2 Kazi Iendelee itakayokuwa ikifanya safari kati ya Jiji la Mwanza na Kisiwa cha Goziba kilichopo ndani ya Ziwa Victoria katika Wilaya ya Muleba,mkoani Kagera.

Wakizungumza leo kabla ya boti hiyo kuanza safari,baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo wa safari ya kwanza ya kibiashara,wamesema itawaondolea adha ya kukosa usafiri wa uhakika iliyokuwa ikiwakabili muda mrefu na itawaunganisha na maeneo ya visiwa vingine.

Wamesema kukosekana kwa usafiri wa uhakika kulisafanya kuchelewa kufikisha bidhaa zao (mazao ya uvuvi) sokoni kutokana na kutumia mitumbwi ya injini kusafiri kati ya kisiwa hicho na maeneo ya nchi kavu ya Muleba,Bukoba na Jiji la Mwanza.

“Usafiri kati ya Goziba na Jiji la Mwanza ilikuwa changamoto na adha kubwa kwetu,tulipoteza muda na kuchelewa kufikisha mazao yetu sokoni kwa kutumia saa 8 hadi 12 kwenda hadi Mwanza kwa mitumbwi ya injini na kurudi kisiwani,”amesema mfanyabishara na mkazi wa Goziba,Masunguliro Mkaluka maarufu Ogopa Kuishiwa.

Ameongeza kuwa wadau hao wa usafirishaji wa abiria na mizigo kuanzisha usafiri huo wa boti ya kisasa iendayo kasi,utachochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wakisiwa hicho wakiwemo wafanyabiashara mbalimbali akiwemo wa mazao ya uvuvi.

Mmoja wa wavuvi kisiwani humo Majura Muganyizi,amesema boti hiyo itakuwa mwarobaini wa adha ya usafiri kati ya kisiwa hicho,Wilaya ya Muleba na Jiji la Mwanza kutokana kukosekana usafiri wa uhakika pia utawaepusha na majanga ya kuzama majini kwa vyombo walivyokuwa wakisafiria kwa kupigwa dhoruba na upepo mkali ziwani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Songoro Marine Transport Ltd,Major Songoro, amesema mkakati wao ni kuwahudumia kulingana na mahitaji ya wananchi wa visiwani na kuwaondolea changamoto ya kukosa usafiri wa uhakika kupitia boti hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 340 ili wafaidi matunda ya uwekezaji huo kwenye sekta ya usafiri wa majini .

Amesema kampuni hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali kwa kuhudumia maeneo ya pembezoni hasa visiwani ili kuwapa unafuu wananchi na kuwapatia fursa ya kusafirisha na kufikisha sokoni kwa wakati mazao yao ya uvuvi na mengine maeneo hali itakayowainua kiuchumi na kukuza vipato vyao hatimaye kuchangia pato la taifa.


Boti ya MV RAFIKI 2 KAZI IENDELEE ikiwa imetia nanga katika ghati la Bandari ya Mwanza Kaskazini baada ya kutoka Kisiwa cha Goziba wilayania Muleba.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...