RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa rafiki zake Morocco hasa kupitia sekta ya Utalii na uvuvi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Zakaria El Goumiri aliyefika kujitambulisha.

Alisema uchumi wa Zanzibar unategemea zaidi sekta ya Utalii na kumueleza balozi huyo kuna kila sababu ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa masuala yanayohusiana na utalii na uvuvi kwani Morocco ina uzoefu mkubwa na imepiga hatua zaidi kwenye sekta hizo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema visiwa vya Zanzibar vilivyozungukwa na Bahari ya Hindi vinaakisi sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane ya Uchumi wa buluu, hivyo alimueleza Balozi Zakaria kwamba Zanzibar inatarajia na inawakaribisha wawekezaji kutoka Morocco kuja kuangalia fursa zinazopatikana kwenye rasilimali za baharini ili wawekeze.

Akitilia mkazo kwenye eneo la uchumi wa buluu, Rais Dk. Mwinyi alisema Zanzibar inatarajia uwekezaji zaidi kwenye kilimo cha bahari ikiwemo ufugaji samaki, usindikaji pamoja na viwanda vya kusarifu samaki kwa njia na zana za kisasa ili kukuza zaidi soko la samaki.

Kuhusu uhusiano wa kidiplomasia baina ya Morocco na Tanzania hususan Zanzibar Dk. Minyi alisema pande mbili hizo zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria na uhusiano huo umekua na faida na kuibua fursa nyingi za uchumi na jamii.

Akizungumzia ujio wa Mfalme wa Morocco visiwani Zanzibar mwaka 2016, Mohammed VI, Rais Dk. Mwinyi aliisifu ziara hiyo kwani iliweka historia na kufungua ukurasa wa mafanikio baina ya nchi mbili hizo hasa alipotembalea Arusha na baadae kurudi tena Zanzibar na kufurahishwa na mandhari ya maeneo yake. Pia alieleza ujio huo uliimarisha urafiki wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi mbili hizo.

Naye, Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Zakaria El Goumiri alimueleza Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Morococo inaungamkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na iko tayari kuungamkono masuala ya jamii na uchumi.

Alisema, Morocco ina uzoefu wa fani nyingi za uchumi na jamii ikiwemo utalii, uvuvi, kilimo na uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya fedha na benki.

Balozi El Goumiri alimuhakikishia Dk. Mwinyi kwamba Morocco itaendeleza na kuimarisha uhusiano uliopo baina yao pia wataendelea kufanyakazi pamoja na kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo.

Uhusiano wa diplomasia baina ya Tanzania na Morocco ni wa kihistoria kwa mataifa mawili hayo, kushirikina kwenye masuala ya uchumi, biashara na jamii.

Morocco yenye mji mkuu wake Rabat, iko Kaskazini Magharibi mwa bara la Afrika, imezungukwa na bahari ya Mediterenia kwa upande wa Kaskazini na magharibi imezungukwa na bahari ya Atlantiki pia inapakana na Algeria upande wa Mashariki pia ina uhasama wa mipaka na taifa dogo la Jamuhuri ya kiarabu ya Saharawi kwa upande wa Magharibi mwa nchi hiyo.




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi  amekutana na Balozi wa Morocco nchini Tanzania Mhe.Zakaria El Goumiri, alipofika Ikulu  Zanzibar leo tarehe 13 Machi 2023.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...