Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo jijini Mwanza, mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Majaliwa Kassim Majaliwa amesema kwamba taasisi za umma zina nafasi kubwa ya kushirikiana na taasisi za binafsi ambazo nyingi zimejikita katika teknolojia inayowezesha kuepusha ajali.
“Shirikisheni sekta binafsi ili kupata ujuzi na kujifunza kutoka kwao, hii itawawezesha kuboresha mifumo na hivyo kulinda maisha ya wananchi wetu ambayo yamekuwa yakipotea kwa ajali,” alisema Mh Majaliwa.
Mh Waziri Mkuu aliongea hayo baada ya kupita katika banda la kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc na kujionea jinsi ambavyo mfumo wa kufuatilia magari ya kampuni na hivyo kuepusha ajali mahali pa kazi kwa miaka zaidi ya 10.
Aliongeza kwamba ili kudhibiti ajali zinazopoteza maisha ya wananchi, taasisi zina jukumu kubwa la kutafuta namna bora ya kulinda miundombinu na pia kuepusha majeruhi, “kwa miaka mitatu iliyopita (2020 – 2022) ajali nchini zilikatisha maisha ya watu 1582 na kusababisha majeruhi 4372, hili halikubaliki kabisa na tunatakiwa kulidhibiti,” aliongeza Mh Majaliwa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. Adam Malima amebainisha kuwa ni wajibu wa kisheria kwa kila mmiliki wa chombo cha moto kukatia bima chombo chake sio tu kwasababu ili asikamatwe na askari wa usalama wa barabarani bali kwa faida yake, wamiliki wengine barabarani, abiria, na watembea kwa miguu.
“Nadhani ipo haja ya kutoa elimu ya kutosha juu ya faida za bima kwenye vyombo vyetu vya usafiri. Sheria ya bima kwenye vyombo vya moto haijawekwa kwa dhumuni ili dereva asikamatwe na askari wa usalama wa barabarani, hapana. Bima ipo kwa ajili ya kukulinda, kwanza wewe dereva pindi utakapopatwa na matatizo barabarani, lakini pia ipo kwa ajili ya kuwalinda wamiliki wengine barabarani, abiria, Pamoja na watembea kwa miguu. Na ndiyo sababu zipo bima za viwango tofauti,” alisema Mh. Malima.
“Kwa kuliona hilo, ningependa kuwapongeza Vodacom Tanzania Plc ambao ni mojawapo ya wadau wakubwa wa wiki hii ya usalama barabarani kwa miaka mingi mpaka imefikia wakati hatuendi kuwaomba tena udhamini, tunajua ni sehemu ya tukio hili. Wenyewe wanatumia teknolojia yao ya mawasiliano kuwa wabunifu kwa kuja bidhaa ambazo zinabadili hali ya Maisha ya Watanzania. Kwa sasa wametuletea VODABIMA, baada ya kuona kuwa kuna changamoto kadhaa za kuzifikia huduma za bima, wao wakaamua kuitumia fursa ya mtandao mpana wa wateja walionao kuwarahisishia kuifikia huduma ya bima kwenye simu zao za mkononi. Ninaamini kila mmoja wenu hapa anamiliki simu ya mkononi, hivyo sioni sababu ya kutoanza kutumia huduma hii ambayo imekurahisishia kuendelea na shughuli zako kwa sababu itakuwezesha kukata bima popote pale ulipo bila kwenda ofisini,” alimalizia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama ambayo kitaifa inafanyika jijini Mwanza kuanzia Machi 14-17 ikiwa na kauli mbiu inayosema, ‘Tanzania Bila Ajali Inawezekana, Timiza Wajibu Wako’.
Katika jitihada za kueneza matumizi na upatikanaji wa huduma ya bima nchini, kampuni ya Vodacom Tanzania Plc imewahamasisha Watanzania kutumia VODABIMA, huduma inayopatikana kwa urahisi kupitia M-Pesa inayowawezesha kujiunga mahali na muda wowote walipo kwa kulipia kidogo kidogo mwaka mzima.
Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni alisema kuwa VODA BIMA inayopatikana kupitia huduma ya M-Pesa imekuja kufanya mapinduzi makubwa kwa kuondoa mlolongo kwa Watanzania ambao wanapatikana sehemu tofauti nchini kuzifikia huduma za bima kwa urahisi, kulipia kidogo kidogo kwa mwaka mzima, na kujulishwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno endapo inataka kuisha.
“Kupitia VODA BIMA inayopatikana kwenye M-Pesa anaweza akajiunga huduma ya bima kwa ajili ya chombo chake cha moto na kuanza kulipia kidogo kidogo kwa mwaka mzima. Pia, mteja atakuwa anajulishwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno kujua mustakabali wa bima yake kama inakaribia kuisha ili alipie. Kwa sasa huduma hii inapatikana kwa wamiliki wa vyombo vyote vya moto kama vile magari madogo na makubwa, bajaji, na pikipiki. Lengo kuu la huduma hii ni kuisaidia serikali kuhamasisha wamiliki wote wa vyombo vya moto wanakuwa na bima kwa njia rahisi, salama, na haraka popote na muda wowote kwa kulipia kidogo kidogo,” alimalizia Bw. Mbeteni
VODA BIMA inayopatikana kwenye M-Pesa ni huduma ya kibunifu ya kiteknolojia iliyozinduliwa kwa mara ya kwanza Julai 2021 na Vodacom Tanzania Plc kuwawezesha Watanzania kupata huduma za bima kwa gharama nafuu na urahisi kwa kujiunga kupitia simu zao za mkononi na kulipia pesa kidogo kidogo kwa mwaka mzima.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa (kulia) akiipongeza Vodacom Tanzania baada ya kupata maelezo ya vifaa vya kudhibiti mwendo na ajali vinavyofungwa kwenye magari ya wafanyakazi kutoka kwa Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni (kushoto), alipotembelea banda la kampuni hiyo, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kwenye viwanja vya Furahisha jijini Mwanza. Wakifuatilia maelezo hayo, wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mh. Adam Malima, na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camilius Wambura.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa (kulia) akisikiliza maelezo ya camera ya usalama zinazofungwa kwenye magari ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania kutoka kwa Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni, alipotembelea banda la kampuni hiyo, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kwenye viwanja vya Furahisha jijini Mwanza. Akifuatilia maelezo hayo, katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mh. Adam Malima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...