Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MKUU wa shule ya sekondari ya kidato cha sita ya Naisinyai ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, William Joseph Ombay amejinasibu kuwa shule hiyo ni bora na hivi karibuni itakuwa na ubora wa taaluma kama shule kongwe za Ilboru na Tabora boys.

Mwalimu Ombay ameyasema hayo kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha sita, ambapo mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise, alikuwa mgeni rasmi.

Mwalimu Ombay amesema shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2006, itakuwa kwenye viwango vikubwa hivi karibuni kutokana na taaluma inayotolewa shuleni hapo.

Amesema shule hiyo ilipanda hadhi mwaka 2023 na kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano kwa mchepuo wa sanaa kwa tahasusi ya HGK ambayo inahusisha masomo ya historia, jiografia na Kiswahili.

“Mwezi Mei wanafunzi 33 wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita kwenye shule yetu na tunatarajia matokeo bora ya ufaulu kwa wanafunzi wote,” amesema mwalimu Ombay.

Hata hivyo, mgeni rasmi wa maafali hayo, Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise amewapongeza viongozi na wanafunzi wa shule hiyo.

Mbise amesema shule ya Naisinyai ni miongoni mwa shule za za mwanzo mwanzo za kata kwenye wilaya ya Simanjiro hivyo vijana wengi wamepitia shuleni hapo katika kupata elimu.

Amesema shule ya sekondari Naisinyai ni shule bora kwa upande wa taaluma, japokuwa baadhi ya watu wanaona ipo porini hivyo wanafunzi wa shule hiyo wasijisikie unyonge.

“Mjitahidi kwenye mitihani yenu ya kidato cha sita tunatarajia mtafika chuo na baadaye muwe na faida kwa jamii, kwani mnaonyesha mtakuwa na mafanikio,” amesema Mbise.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mahafali hayo Joseph Emmanuel Zacharia na Daudi Daniel Gwandu wakisoma risala kwa mgeni rasmi wameeleza kuwa wamesoma na kupata elimu bora kwenye shule hiyo hivyo wanatarajia ufaulu mzuri.

Hata hivyo, wamemshukuru mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera kwa kuwawezesha kupitia shirika la Ted kupata kompyuta 10 na server moja hivyo kujifunza na kusoma kwa ufanisi.

“Pia tumefanikiwa kuendelea kuboresha mazingira kwa kupanda maua, miti katika maeneo yote ya shule, tumeingiza umeme wa Tanesco kenye bweni la wavulana ambao unatusaidia kuangaza maeneo ya bwenini hasa wakati wa usiku,” amesema Joseph.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...