ZAIDI ya wanafunzi 2,000 wa shule ya Msingi Kibaoni, Mahembe na maelfu ya wananchi wa kata ya Kindai, wataondokana na ajali za barabarani za mara kwa mara, baada ya serikali kujenga kivuko cha chini (Underpass), kwenye eneo la Kibaoni, katika Manispaa ya Singida.

Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Singida, mhandisi Yohannes Mbegalo, alisema ujenzi wa kivuko hicho chenye urefu wa mita 24.5, upana mita 4.6 na kimo mita 2.4, utakamilika juni 22 mwaka huu, na utagharimu Sh. Milioni 427.8/=, na hivyo kuokoa maisha ya mtu mmoja anayepoteza maisha, kila baada ya miezi mitatu.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, pamoja na wananchi, kufuatia ziara ya Mkuu huyo wa mkoa alipokwenda kuona maendeleo ya ujenzi, Mbegalo alisema kuwa, Wakala wa Barabara (TANROADs), aliamua kuchukua hatua ya kujenga kivuko cha chini cha waenda kwa miguu eneo la barabara kuu ya Dodoma – Singida ili kuwezesha waenda kwa miguu kuvuka kwa usalama.

“Hapa licha ya kuwa na shule hizi, kuna wananchi wengi na Makanisa, ambayo waumini huvuka kuwahi ibada na hatimaye hukutwa na kadhia ya kugongwa na magari, katika barabara hii ya Dodoma-Singida, eneo la Kibaoni.…,”alifafanua Mbegalo.

Baadhi ya Wazazi, akiwemo Rachel Chaka, Theophil Macarius na Diwani wa Kata ya Misuna, Hamisi Kisuke, walisema kukamilika kwa kivuko, ni nafuu kwa wanafunzi wanaopoteza maisha, kutokana na uzembe wa madereva kwa kushindwa kuzingatia alama za usalama barabarani.

Hata hivyo, wazazi hao wameiomba Serikali, kujenga kivuko kingine cha juu, karibu na eneo la Kibaoni, ambacho kitasaidia wananchi kuvuka nyakati za usiku, ili kuepuka vibaka watakaolazimika kuvizia watu watakaopita katika daraja la chini (Underpass).

“Tumeelezwa kivuko hiki kitawekewa taa na kamera ili kudhibiti wezi, lakini sisi tunaomba tujengewe pia daraja la juu ili tuwe tunapita wakati wa usiku, kwasababu hili hapa la chini sisi usiku itakuwa ni hatari, tutakabwa na vibaka,” alisema Kiranga.

Akizungumza na wanafunzi na wananchi baada ya kukagua ujenzi wa kivuko hicho, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, aliwataka kutumia kivuko hicho, ili kuepuka ajali.

Mkuu huyo wa Mkoa alimtaka Wakala wa Barabara nchini , kuhakikisha amamsimamia vyema Mkandarasi aliyepewa jukumu la ujenzi wa mradi, aweze kukamilisha mapema zaidi, ili wananchi wanufaike na kivuko hicho.

Ziara hii ya Mkuu wa mkoa katika mradi wa kivuko cha chini cha waenda kwa miguu, ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali zilizopangwa kutekelezwa katika wiki ya maadhimisho kuelekea kilele cha sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanzania na Zazibar.

Shughuli zilizotangulia kutekelezwa tangu mwanzo wa wiki, katika Manispaa ya Singida ni pamoja na usafi wa mazingida, uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa zahanati ya Isomia, uzinduzi wa wiki ya chanjo, mtahalo wa masuala ya Muungano uliohusisha wanafunzi wa shule 5 za sekondari katika manispaa ya Singida pamoja na uchangiaji damu salama.
Mwonekano wa kivuko cha chini cha waenda kwa miguu katka barabara ya Singida- dodoma eneo la kibaoni Manispaa ya Singida
Mkuu wa mkoa wa Singida Pier Serukamba ( kushoto) akiongozana na Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara ( TANROADs ) Mkoa wa Singida Mhandisi Yohannes Mbegalo pamoja na viongozi wengine wa serikali, wakati wakikagua kivuko cha chini cha waenda kwa miguu eneo la kibaoni Manispaa ya Singida


Wanafunzi wa shule za msingi Kinaoni na Mahembe wakionesha furaa baada ya kuruhusiwa kupita katika kivuko cha chini cha waenda kwa miguu. kivuko hichi kitakuwa mkombozi kwa wanafunzi hao ambao wamekuwa wahanga wa ajali za barabarani katika eneo hilo


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...