Na Janeth Raphael - Dodoma

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) pamoja na Kampuni ya DOHWA kutoka nchini Korea ya Kusini wamesaini mkataba wa usanifu na usimamizi wa Ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya uondoshaji na kutibu majitaka.

Mkataba huo umesainiwa ofisi za DUWASA jijini Dodoma na utagharimu kiasi cha dola za Marekani 5,225,000 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 12.3.

Waziri wa maji Jumaa Aweso mara baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba huo amesema lengo la makubaliano hayo na kampuni hiyo ya DOHWA ni kuendana na ongezeko la watu katika jiji la Dodoma na uzalishaji wa majitaka ambapo majitaka yasipowekewa utaratibu mzuri hupelekea kugeuka na kuwa uchafuzi wa mazingira.

"Asilimia 80% ya majisafi yanatumika na binadamu katika matumizi ya kila siku na hugeuka kuwa majitaka na tujiulize yanakwenda wapi kama si kuchafua mazingira" - Waziri Aweso.

Wakazi wa Dodoma asilimia 20 pekee wanapata huduma ya kuondoa majitaka katika kaya 14 kati ya 41 kupitia mtandao wa DUWASA, ambapo ufanisi wake hauendani na ongezeko la kasi ya watu katika Jiji hilo na uzalishaji wa majitaka.

Hata hivyo Waziri Aweso amesema kuwa Wizara yake haijafanya uwekezaji wa kutosha katika eneo la uondoshaji wa majitaka.

Awali Mkurugenzi Mtendaji DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo unalenga kuhusisha usanifu na ujenzi wa mabwawa mapya makubwa 16 yenye uwezo wa kutibu lita za maji milioni 20 kwa siku, usanifu na ujenzi wa bomba kubwa kwa kilomita 107.5, kubadilisha mabomba chakavu kilomita 2.6 na kukarabati kilomita 2.1 za mtandao wa majitaka.

Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 49 kuanzia tarehe ya utiaji saini ambapo awamu ya kwanza mhandisi mshauri atafanya kwa muda wa miezi 13 kusanifu mradi na awamu nyingine itatumia miezi 36 katika ujenzi wa mradi huo.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...