Na Said Mwishehe, Michuzi TV- Simiyu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, amesema Chama kitaishauri serikali iwasikilize wananchi kuhusu usafiri wa bodaboda kubeba abiria zaidi ya mmoja.
Akizungumza jana baada ya kupokelewa wilayani Bariadi mkoani Simiyu akitokea Mkoa wa Mara, Kinana pamoja na mambo mengine alisema upo umuhimu wa kuangaliwa upya kwa sheria ya usafiri wa bodaboda ambayo kwa sasa inakataza kubeba abiria zaidi ya mmoja.
“CCM inakwenda kuzungumza na serikali kuiangalia sheria ya kuzuia usafiri wa pikipiki (bodaboda) kuruhusiwa kubeba abiria zaidi ya mmoja,” alisema Kinana alipokuwa akizungumza na wananchi waliojitokeza kumlaki alipongia wilayani humo.
Awali akiwa mkoani Mara, Kinana alieleza kwa kina kuhusu suala bodaboda kubeba abiria zaidi ya mmoja. “Sasa msije mkasema amekuja Makamu Mwenyekiti amesema tupakie watu wanne, watano kwenye bodaboda.
“Kupakia watu wawili mtu na rafiki yake ukimsimamisha mwambie sheria hairuhusu lakini kwa sasa nenda, sio unamchukua mwenye pikipiki na abiria unawapeleka kituo cha Polisi. Kuna mambo nimeyaona yako Tanzania peke yake.
“Nenda India wanatumia bodaboda sana, wanakaa watu watatu kuna shida gani? Wanaosafiri wanapata unafuu, mwenye pikipiki anapata fedha wewe inakuhangaisha nini? Kuna nchi nyingine Thailand kila bodaboda ina watu watatu wanne na haisimamishwi.
“Kuna nchi ya Vietnam asilimia 70 ya usafiri ni pikipiki, unakuta mtu anapikipiki amempakia mkewe nyuma na mtoto mbele lakini sijaona anasimamishwa, hapa ni mgogoro,” alisema.
Pia, Kinana alizungumzia sheria ambazo zimekuwa kero kwa wananchi ambapo amewaomba madiwani wanapotengeneza sheria za halmashauri na serikali za mitaa watengeneze sheria rafiki kwa wananchi.
“Msijifungie mahali, mnatafuta mapato halafu mnatunga sheria hamna habari kwamba sheria hiyo inakwenda kuumiza watu, na kabla hamjatunga sheria ninyi mnatoka kwenye kata zenu nendeni na rasimu ya sheria.
“Mkakae na wananchi wenu muwaambie mnataka kutunga sheria hii na wakisema sheria hii ni mbovu hatuitaki, achaneni nayo. Wakiwa na mabadiliko yazingatieni kwa sababu mnatunga sheria kwa ajili yao.
“Inakuaje sheria kwa ajili yao, lakini hata ile nafasi ya kuwauliza hakuna, haiwezekani lakini katika kusimamia sheria kuna sheria, kuna kanuni na kuna utaratibu,” alisema.
Aliongeza kuwa, jambo lingine ambalo ni lazima liende na utekelezaji wa sheria ni busara, “wakimkamata mtu ni kumweka ndani kwani hawajui kusamehe.”
Akitoa mfano mwingine alisema kuwa nchi ilipiga marufuku masi kusafiri usiku kwa miaka 35, kabla ya hapo mtu ilikuwa ruhusa na ilirahisisha mambo mengi.
“Mtu anasafiri usiku akifika anafanya shughuli zake mchana kutwa na kisha usiku anapanda basi tena anasafiri usiku mzima.Nashukuru na naipongeza serikali na wabunge kwa kutoa kauli sasa mabasi yatakuwa yanasafiri usiku,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...