Na Mwandishi Wetu
Baadhi ya vijana wakike ambao ni wahanga wa utoaji mimba usio salama na madaktari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wameshauri kuwepo na huduma hiyo kwa wanawake ambao watapewa mimba kwa njia za kubakwa na kwa wale ambapo watapata kutoka kwa ndugu zao wa damu.
Easter John mkazi wa Buzuruga mkoani Mwanza alisema akiwa na umri wa miaka 16 alipata ujauzito kwa kubakwa na Mjomba wake aliyewatembelea nyumbani kwao wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.“
Baada ya kupima na kubaini kuwa nimepata ujauzito nililazimika kusafiri kutoka nyumbani Buzuruga hadi Wilaya ya Sengerema kwa ajili ya kutoa mimba hiyo, nilikwenda hospitali lakini nilikataliwa kupewa huduma hiyo ambapo niliamua kutoa mimba kwa kutumia dawa za kienyeji kwa sababu sikutaka kubeba mtoto niliyepewa na mjomba wangu na mbaya zaidi kwa kubakwa. Nakumbuka nilipoteza damu nyingi nikiwa nimejificha kwenye nyumba ndugu yangu hadi hali ilipozidi kuwa mbaya.
Hatimaye nilifikishwa hospitalini ambako nilipata matibabu bora zaidi ingawa walitoa mfuko wa uzazi kwa sababu ulikuwa umeoza. Vinginevyo, ningeweza kupoteza maisha yangu," alieleza binti huyo kwa uchungu Easter ambaye alikuwa mwanafunzi wa sekondari wakati huo anahitimisha:
“Ninapendekeza kuwekwa kwa huduma hii kwa maana kama mimi ambao tulipata mimba kutokana na matukio tofauti ikiwa ni pamoja na kubakwa.”
Binti mwingine, Amina Ismail kutoka jijini Mwanza amesema kuwa yeye akiwa na umri wa miaka 17 alipata mimba baada ya kubakwa na mwendesha bodaboda aliyekuwa akimpeleka shuleni kila siku.
"Baada ya kubakwa na kupata ujauzito, nilikwenda kutoa ujauzito huo kwa njia ya kienyeji, lakini baada ya hapo nilitoka damu nyingi na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi," alisema.
Amesisitiza: “Kwa hiyo, baadhi yetu tulipata mimba katika umri wa ujana ama kwa kubakwa, au kutoka kwa ndugu zetu. Kwa hivyo, ninaishauri serikali iweze kutoa huduma hizi kwa wasichana kama sisi ambao tunapatiwa mimba bila hiari yetu.”
Kwa upande wake Elizabeth Masanja kutoka Kahama Mkoani Sinyanga alisema yeye alipata ujauzito baada ya kubakwa na mwanafunzi mwenzake ambaye alimlazimisha kufanya tendo la ndoa bila yeye mwenyewe kutaka:
“Awali ya yote napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa wote walioshiriki kunisaidia kurudisha maisha yangu baada ya kutoa ujauzito huo kwa kutumia dawa za kienyeji.”
Kwa upande wao, baadhi ya Madaktari kutoka Kanda ya Ziwa walisema wanawake watatu kati ya watano wanaolazwa hospitalini kwa matatizo ya utoaji mimba ni wenye umri chini ya miaka 20 na wengi wao walipata matatizo ya utoaji mimba usio salama.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Buzuruga cha jijini Mwanza, Dkt. Mahube Richard amesema kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu. zaidi ya wanawake 90 walilazwa katika kituo hicho kutokana na matatizo yanayohusiana na utokaji wa mimba.
Dkt. Mahube ametoa wito kwa serikali kutoa nafasi kwa wanawake waliobakwa kutoa mimba walizopewa na ndugu zao wa damu wakiwemo wajomba, baba, Kaka na wapwa zao.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Nyankumbu mkoani Geita, Dkt. Irene Temba amesema ipo haja kwa wanawake waliopewa mimba na ndugu wa damu na kwa ubakaji kupewa fursa ya kutoa mimba salama katika vituo vya afya.
"Tunaruhusiwa kisheria ikiwa ni kuokoa maisha ya mwanamke, na sio vinginevyo, lakini serikali inaweza kuongeza kwa wale waliopata ujauzito kwa ubakaji au unyanyasaji wa kijinsia au kutoka kwa nduu zao ," Dk Irene amesema.
Naye Mkurugenzi wa Kanda wa Mtandao wa Kimataifa wa Wanawake wa Haki za Uzazi Afrika (WGNRR AFRICA), Nondo Ejano alisema:“Utoaji mimba usio salama unachangia hadi asilimia 19 ya vifo vya uzazi nchini Tanzania huku huduma ya afya kwa ajili ya kudhibiti matatizo ya utoaji mimba usio salama inagharimu mfumo wa afya wa serikali bilioni 10.4 kwa mwaka.
Gharama hizi za kibinadamu na za kifedha zinaweza kuepukika kwa kiasi kikubwa na, hii inaweza kutoa rasilimali kutumika mahali pengine.Tathmini ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonyesha kuwa ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (VAWC) uliotokea nchini Tanzania mwaka 2022 upo kwa kiwango cha juu sana.
Tafiti iliyofanywa na Taasisi ya Guttmacher Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS) ya mwaka 2015/16 ilisema kuwa inakadiriwa kuwa, mimba 405,000 zilitolewa ndani ya mwaka 2013 nchini. Idadi hii ni kiwango cha utoaji wa mimba 36 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri kati ya miaka 15-49 na uwiano wa utoaji mimba 21 kwa kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai.Tafiti iliongezea kuwa utoaji mimba usio salama unachangia zaidi ya theluthi moja ya wanaolazwa mahospitalini kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba na takribani robo moja ya vifo vya uzazi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...