Na Mwandishi wetu
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeshiriki kwenye Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara na Viwanda (Sabasaba) huku wadau wengi wakitembelea banda la WCF kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Akizungumza kuhusu Maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema wadau wengi walijitokeza kupata uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko.
"Wadau wengi wamejitokeza kutembelea banda letu kuanzia waajiri, waajiriwa na wananchi kwa ujumla jambo linaloonesha hamasa ya wadau kutaka kufahamu kuhusu haki yao ya fidia kisheria endapo wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi", alisema Dkt. Mduma na kuongeza:
"Kauli mbiu ya maonesho haya ni Tanzania - Mahali Sahihi kwa Uwekezaji na Biashara ambayo inaakisi malengo ya Mfuko ya kulinda nguvukazi ya Taifa na kuchochea tija kwa sekta za umma na binafsi kupitia uwekezaji na biashara. Tunajivunia kuwa moja ya Taasisi ambazo zinalenga kutimiza kwa vitendo kaulimbiu ya mwaka huu".
Dkt. Mduma anatanabaisha kuwa hadi sasa asilimia 86 ya huduma zote za WCF zinapatikana kwa njia ya mtandao hivyo kuwaondolea waajiri adha ya upotevu wa muda na kuwapa fursa ya kujikita katika uzalishaji mali.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la WCF mmoja wa wadau, Bi. Zakia Kimaro alisema amefurahishwa na uwepo wa WCF katika maonesho haya kwa sababu wananchi wengi wamepata fursa ya kujifunza huduma zitolewazo.
"Uwepo wa taasisi ya WCF unatupa nafasi ya kujifunza huduma ambazo ni haki yetu kisheria. Pia nitoe kongole kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma zake kwa njia ya mtandao. Taasisi nyingine za umma zinapaswa kujifunza kupitia WCF".
Maonesho ya Kimataifa ya Biashara na Viwanda yamefanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Juni 2023 hadi kufikia kilele tarehe 13 Julai 2023 ambapo Mgeni Rasmi katika Sherehe za ufungaji alikua ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...