Na Hamida Kamchalla, TANGA.

TAASISI ya Afyachek ya jijini Dar es salaam inatarajia kufanya zoezi la upimaji wa afya kwa hiyari kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga kuanzia tarehe 21 hadi 25 mwezi huu.

Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za jiji la Tanga, Mratibu mkuu wa Afyachek Isaac Maro amesema lengo la kuweka kambi mkoani hapa ni kutaka kuwajengea wananchi tabia ya kupima afya kwa hiyari mara kwa mara.

"Watanzania tuna tabia ya kutopima afya zetu, hivyo tunatumia garama kubwa sana kujitibu, Afyachek tumekuja Tanga kufanya zoezi la upimaji wa afya bure na tunatarajia kupima watu 5000," amesema.

Naye Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema magonjwa yatayopimwa ni yanayoambukizwa na yasiyoambukizwa na endapo mtu atakutwa na ugonjwa atapatiwa tiba lakini kwa wale ambao watakuwa na magonjwa kama yatahitaji upasuaji watapatiwa tiba watakapokuja madaktari bingwa.

Ametaja magonjwa yasiyoambukizwa kuwa ni shinikizo la damu, kisukari, saratani ambapo watapima (mlango wa kizazi, matiti na tezi dume), pamoja na macho lakini pia ameyataja magonjwa ya kuambukizwa kuwa ni virusi vya ukimwi, kifua kikuu na malaria.

"Takwimu inaonesha wapo watu laki mbili ambao hawajajitambua afya zao katika upimaji wa vvu, tunawashauri na kuwahamasisha watu kupima na kama watu wote ambao wana maambukizi wangekuwa wanafuata masharti ya kumeza dawa tunaweza kuutokomeza kabisa" amesema.

Hata hivyo Waziri ameipongeza na kuishukuru benki ya CRDB kwa kujitolea kufadhili huduma za afya katika mpango huo wa Afyachek lakini pia katika huduma nyinginezo

"Niwapongeze sana sana wadau wetu wakubwa CRDB, benki yetu kwa kujitolea na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kufadhili huduma zinazowasaidia wananchi" amebainisha.

"Sasa, nitoe wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga kujitokeza, wilaya zote kujitokeza kuja kupima katika viwanja vya shule ya sekondari ya Usagara, lengo ni watu 5000 lakini hata tukipata zaidi itakuwa vizuri" amesisitiza.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akiongea na waandishi wa habari, katikati ni Mratibu mkuu wa Afyachek Dkt. Isaac Maro akifuatiwa na Mganga mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeyo.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...