Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar Shaibu Ibrahim Mohamed amewataka walimu wa lugha ya kiswahili kuunda umoja utakaowawezesha kutatua matatizo na kupata fursa za ajira ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo ameitoa Baraza la Kiswahili Mwanakwerekwe wakati alipokua akifunga mafunzo ya lugha ya kiswahili kwa wageni .
Amesema endapo kutakua na umoja utakaowashirikisha walimu wote wa lugha hiyo wataweza kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza katika kutafuta soko la ajira ulimwenguni.
"Tutumie fursa hizi kuhakisha tunalifanikisha suala la umoja wetu wa kiswahili ili kufikia lengo la kuitangaza lugha hii",alisisitiza.
Aidha amefahamisha kuwa katika kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kukua zaidi Baraza la Kiswahili limekuwa likitoa mafunzo mara kwa mara kuwapatia walimu hao ili kuweza kujua mbinu bora za kuzitumia kufundishia hasa kwa wageni ambao wanahitaji kuijua lugha hiyo.
Aidha Mkurugenzi huyo Alilipongeza baraza la kiswahili kwa kutoa mafunzo hayo kwani yatawawezesha walimu kupata maarifa zaidi na mbinu za kuitumia katika kufundishia lugha hiyo.
"Naamini kuwa mafunzo hayo ni chachu ya kuimarisha lugha yetu kwa wageni kwani safari hii kumekuwa na mwamko mkubwa hivyo muwe mabalozi wazuri wa kuitangaza lugha yetu",alihimiza Mkurugenzi.
Aidha amewashukuru wakufunzi kwa kushiriki mafunzo hayo na kuwataka kushirikiana na Bakiza ili kuimarisha zaidi kiswahili kwani kuna wageni wengi wanaohitaji kujifunza.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kiswahili kinaendelea kutumika duniani ni kuendeleza kutoa mafunzo na kuhakikisha wanatafuta fursa mbalimbali ili kuendeleza mafunzo hayo.
Akisoma risala katika ufungaji wa mafunzo hayo Mwalimu Abdalla Ali Abdalla amesema mafunzo hayo ni kutekeleza sera ya Rais Mwinyi katika kuhakikisha vijana wanapata elimu na kupata ajira.
Akitaja changamoto zinazowakabili Mwalimu Abdalla ameeleza kuwa ukosefu wa ufadhili katika mafunzo kama hayo kumekuwa kukiwakosesha wengne fursa ya kushiriki.
Aidha amelitaka Baraza la Vijana kuwaunga mkono katika kupambana katika kutafuta fursa za ajira na kuepuka uvumi wa baadhi ya watu wanaosema kua kiswahili hakina ajira jambo ambalo ni upotoshaji wa jamii.
Nae Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Dkt Mwanahija Ali Juma amefahamisha kuwa baraza limeshawapatia mafunzo ya Kiswahili kwa wageni walimu 175 kwa awamu tatu tofauti.
"Sasa kiswahili kina hadhi kuwa duniani kwani ni lugha inayotumika rasmi ikiwemo umoja wa Afrika hivyo kwa umuhimu huu tutajitayarisha katika kupata wafadhili ili kukiimarisha zaidi..,"alifahamisha Katibu.
Aidha amewapongeza washiriki kwa utulivu na usikivu wao na kuwataka kununua vitabu vya kiswahili ili kujisomea na kupata ujuzi zaidi.
Hivi karibuni kulifunguliwa mafunzo ya kiswahili kwa wageni yaliyowashirikisha takribani walimu mia moja wa lugha ya Kiswahili kutoka maeneo mbalimbali Nchini .
MAELEZO YA PICHA Wanafunzi wa Mafunzo ya mbinu za kusomesha lugha ya kiswahili kwa wageni wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo yaliyofanyika Ofisi za Baraza la Kiswahili Mwanakwerekwe ZANZIBAR.PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO ZANZIBAR.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...