Mama Kinara Bhoke Mokhe akitoa elimu kuhusu Masuala ya VVU


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Imeelezwa kuwa Afua ya Mama Kinara iliyoanzishwa katika Hospitali ya mji wa Tarime Mkoani Mara ili kuhakikisha akina mama wajawazito na wanaonyonyesha walio na Virusi vya UKIMWI na watoto wao wanabaki katika matunzo na matibabu ya VVU imekuwa matokeo chanya katika kuboresha utumiaji wa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.


Mama Kinara ni mama anayejitolea ambaye yuko tayari kusaidia ufuatiliaji wa karibu wa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha kuhusu huduma za matumizi ya dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs), katika nyumba zao na jamii.


Akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea Hospitali ya Mji wa Tarime ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) nchini Tanzania , Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto Hospitali ya Mji wa Tarime, Elizabeth Burure amesema walianzisha Huduma ya Mama Kinara ili kuhakikisha elimu ya VVU inafika kwa jamii.


“Tulianzisha Mpango wa Mama Kinara ili kuhakikisha wamamama wajawazito na wanaonyonyesha walio na VVU na watoto wao wanabaki katika matunzo na matibabu ya VVU, kuhakikisha ufuasi mzuri wa ART/ARVs na dawa kinga kwa watoto na kufikia lengo la upimaji wa mapema kwa wototo waliozaliwa na mama mwenye VVU kwa 100%. Mama Kinara (akina mama wanaoishi na VVU) walipewa jukumu la kufuatilia watoro katika huduma (MISSAP) na utoaji wa huduma za kisaikolojia (PSS)”,ameeleza Elizabeth.


Amesema wamekuwa wakitumia mpango wa Mama Kinara kwa ajili kuwafuatilia akina mama wanaoishi na maambukizi ya VVU ili waendelee na huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Elizabeth amesema Mpango wa Mama Kinara ulianzishwa baada ya PEPFAR kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kubaini kukosekana kwa ufuasi mzuri kwenye kwa matibabu ya ART kwa wamama wajawazito na wanaonyonyesha inahusishwa na kuongeza hatari ya maambukizo ya VVU kwa watoto wao.

Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto Hospitali ya Mji wa Tarime, Elizabeth Burure


“Kupitia ripoti za ukaguzi wa upimaji wa awali kwa watoto (EID) zilizotayarishwa kwa misingi ya kila robo mwaka, tulibaini kukosekana kwa mwendelezo wa huduma za ART miongoni mwa wamama wajawazito na wanaonyonyesha, hii ilikuwa sababu kuu ya hatari kwa watoto wachanga walioambukizwa VVU.
“Lakini pia tulianzisha Afua ya Mama Kinara baada ya kubaini kuwa, kuna ukosefu wa usaidizi wa kijamii, unyanyapaa, na uhusiano mbaya ndani ya familia na jamii pamoja na kuchelewa katika huduma za upimaji wa watoto (EID)”,ameeleza Elizabeth.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Huduma za Kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto Hospitali ya Mji wa Tarime, Calorine Anatoly amesema mpango wa Mama Kinara umesaidia kupunguza athari kubwa ya kisaikolojia ya ubaguzi na unyanyapaa.
“Mama Kinara ni mama Mwenye VVU na anatumia dawa za ARVs vizuri, ni mama mwenye moyo wa kujituma katika kuwaelimisha akina mama kuhusu masuala ya VVU. Mama Kinara amekuwa msaada mkubwa wa kuibua changamoto zinazowakabili akina mama wanaoishi na VVU na kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanawake wanaotumia dawa za ARVs”,amesema Calorine.

Msimamizi wa Huduma za Kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto Hospitali ya Mji wa Tarime, Calorine Anatoly.


“Katika mpango wa Mama Kinara, tunawatumia akina mama waliofunzwa na kupewa majukumu muhimu ya kufuatilia wateja kuhusu huduma za ART na kutoa elimu na huduma za kisaikolojia na kijamii. Mama Kinara anatoa ushauri endelevu juu ya vipengele muhimu kama vile unywaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs), njia salama za kujifungua na njia sahihi za unyonyeshaji wa watoto wachanga pamoja na umuhimu wa upimaji mapema wa wototo (EID”,amesema.


Amebainisha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni 2023 wamefanikiwa kuwafikia akina mama 940 na baada ya kuwafanyia kipimo cha kwanza, akina mama wajawazito 19 wamebainika kuwa na maambukizi ya VVU kupitia Mama Kinara.


“Utekelezaji wa Mpango wa Mama Kinara umetoa matokeo mazuri na kuleta mabadiliko chanya kwenye kituo. Kituo kimefanikiwa kufikia malengo katika upimaji wa wingi wa VVU kwa asilimia 97%,wamama wajawazito waliopimwa na kukutwa kiwango cha chini kabisa cha VVU (<50cp) asilimia 98% na upimmaji wa mapema kwa watoto umeongezeka kufikia 100%. Kila watoto wachanga wamepata huduma bora na kwa wakati. Tuwashukuru sana mama vinara kwa bidii wanazofanya”, ameongeza Calorine.


Kwa upande wake, Mama Kinara ,Hawa Hamis (siyo jina halisi) mkazi wa Tarime ambaye anaishi na maambukizi ya VVU tangu mwaka 2009 amesema amekuwa akitoa elimu ya ufuasi mzuri wa dawa kwa akina mama wanaoishi na maambukizi na kuwapa elimu namna ya kuwakinga watoto wasipate maambukizi ya VVU.

“Kuwa na maambukizi ya VVU siyo mwisho wa Maisha, ukiwa mfuasi mzuri wa dawa utaishi marefu”,amesema Hawa (pichani).


Naye Bhoke Mokhe (32) ambaye pia ni mama kinara anayetumia muda mwingi kutoa elimu ya VVU kwa akina mama ameishukuru PEPFAR pamoja na serikali ya Tanzania kwa kuwapatia mafunzo na kuwawezesha kuwafikia akina mama wengi zaidi kwani lengo ni kuhakikisha watoto wanazaliwa bila maambukizi ya VVU.

 

Bhoke Mokhe


Hospitali ya Mji wa Tarime ilianzishwa mwaka 1956 kama zahanati na kupandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya mwaka 1970. Ni hospitali ya rufaa ambapo pia ina kituo cha matunzo na matibabu na inatoa huduma za kina za VVU ikiwa ni pamoja na HTS, huduma za VVU na Kifua Kikuu, huduma za dawa za VVU (ART) kwa watoto na watu wazima, uchunguzi na usimamizi wa magonjwa ya zinaa (STI), huduma za kupima VVU kwa familia (mume/mke na watoto), na Virusi vya Ukimwi (HVL) na imekuwa ikipata msaada wa PEPFAR kupitia CDC.


Katika Mkoa wa Mara, kuna vituo vya afya 358, ambapo vituo vya afya 107 vinasaidiwa kupitia PEPFAR kutoa huduma za matunzo na matibabu pamoja na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).


Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI - The U.S. President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) kupitia Kupitia Kituo cha udhibiti na uzuiaji wa Magonjwa cha nchini Marekani (CDC) kwa kushirikiana Amref Health Africa Tanzania na Wizara ya Afya inatoa huduma kamili za VVU ili kufikia udhibiti wa janga la VVU na kufikia lengo la 95-95-95 ifikapo 2030 ambapo Mpango huu unasaidia Wizara ya Afya (MoH) kufikia lengo la kitaifa la kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) hadi chini ya asilimia nne (<4%) ifikapo mwaka 2026.Malengo ya PEPFAR ni kuongeza idadi ya wajawazito na wanaonyonyesha wanaojua hali zao za mammbukizi ya VVU, kuongeza idadi ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha walio na VVU wanaopata dawa za kurefusha maisha (ARVs), kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matunzo na matibabu kwa akina mama na watoto wachanga wanaoishi na VVU na kuboresha maisha ya watoto walio zaliwa na mama mwenye VVU na wale watoto tayari wana maambukizi ya VVU.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...