Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Mchezo wa Fainali ya Ngao ya Jamii utachezwa baina ya Yanga SC dhidi ya Simba SC kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, mchezo huo utapigwa Agosti 13, 2023 majira ya saa 1:00 Usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Simba SC imeifuata Yanga SC kwenye mchezo huo baada ya kuifunga Singida Big Stars kwa jumla ya mikwaju ya panalti 4-2 kwenye uwanja huo wa Mkwakwani, baada ya timu hizo kutoa sare ya 0-0 kwenye dakika 90’ za mchezo huo wa Nusu Fainali ya pili.

Kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti, Singida Big Stars walianza kupiga mkwaju wao kupitia kwa Aziz Andambwile na kupanguliwa na Golikipa wa Simba SC, Ally Salim. Baada ya kukosa Singida, walifuata Simba SC kupiga mkwaju wa kwanza kupitia kwa Luís Miquissone ambaye aliweka wavuni mkwaju huo.

Penalti ya pili ya Singida ilipigwa na kuwekwa wavuni na Mshambuliaji wa timu hiyo, Tchakei Marouf. Kwa upande wa Simba SC, Saido Ntibazonkiza alifunga mkwaju wa pili na kumuacha Golikipa wa Singida, Beno Kakolanya hana la kufanya.

Singida Big Stars walikosa mkwaju wa tatu, kupitia kwa Yusuph Kagoma ambaye alipaisha juu mpira alioupiga kuelekea kwa Ally Salim. Mzamiru Yassin alifunga mkwaju wa tatu kwa upande wa Simba SC.

Duke Abuya alifunga mkwaju wa nne wa penati kwa upande wa Singida na kumuacha Ally Salim ‘hoi bin taaban.’ Simba SC walipiga penalti ya ushindi kupitia kwa Moses Phiri ambaye alifunga mkwaju huo wa penalti wanne ambao uliipeleka katika Fainali Klabu ya Simba.

Yanga SC ni timu ya kwanza kutinga Fainali ya mashindano hayo, baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC, kwenye uwanja huo wa Mkwakwani, shukrani kwa mabao ya Stephane Aziz Ki dakika 84’ na Clement Mzize aliyefunga bao la pili kwenye dakika ya 88’.

Agosti 13, 2023 majira ya saa 9 alasiri, Azam FC watacheza dhidi ya Singida Big Stars, mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wakati majira ya 1:00 usiku utapigwa mchezo wa Fainali baina ya Watani wa Jadi Yanga SC dhidi ya Simba SC. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...