Na: Calvin Gwabara - Tanga
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na watafiti kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) wanafanya majaribio ya matumzi ya wadudu rafiki kupambana na Viwavijeshi vamizi kwenye mahindi.
Akizungumza na Mwandishi wetu Mkuu wa Mradi huo wa Utafiti Prof. Gration Rwegasira kutoka SUA amesema baada ya utafiti na majaribio ya maabara na baadae ngazi ya kitalu nyumba wamebaini kuwa wadudu aina ya Trichogramma mwanzae na Telenomous remus wameonesha uwezo
mkubwa katika kupambana na viwavijeshi vamizi.
‘’Katika utafiti wetu tukabaini wadudu hao aina mbili ambao ni nyigu wadogo sana wenye uwezo wa kuwadhibiti Viwavijeshi vamizi na wao wanauwezo wa kushambulia mayai ya kiwavijeshi na sio kiwavijeshi mwenyewe na hivyo kwakuwa wanashambulia mayai yao wanasababisha
kutoongezeka na kupotea kwa viwavijeshi kwa kuwa hawazaliani shambani‘’alieleza Prof. Rwegasira.
Aliongeza ‘’Kwa kuwa tunatambua hatua ambayo inaathiri zaidi mazao ya wakulima ni Kiwavi kwa hiyo mayai yasipoanguliwa maana yake kiwavi hatoanguliwa na h
ivyo kuwa tumemsaidia mkulima kumaliza wadudu hao hatari kwenye mazao ya mkulima bila kutumia viuatilifu ambavyo vina sumu‘’.
Prof. Rwegasira amesema hivi sasa wapo katika hatua ya tatu ambayo ni kuwapandikiza wadudu hao kwenye mashamba ya wakulima yaliyolimwa Mahindi kwenye Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro na Muheza mkoani Tanga ili kuona namna ambavyo wanafanya kazi kwenye mashamba halisi
yenye wadudu aina ya Viwavijeshi Vamizi.
‘’Leo tumeweka kwenye mashamba haya lakini tutarudi kuweka tena baada ya wiki mbili na hii inatakiwa ifanyike mahindi yakishafikisha wiki tatu hadi nne baada ya kupandwa maana majani yatakuwa matatu hadi manne na ndio wakati ambao Viwavijeshi Vamizi wanakuja kutaga mayai yao kwenye mimea kwa hiyo wakifika na kutaga wadudu hao rafiki wanashambulia mayai yote shambani”, alieleza Prof. Rwegasira.
Aidha amesema wadudu hao rafiki wanatumia mayai ya Viwavijeshi Vamizi kuweza kuzaana hivyo ndio maana wanayatafuta mayai hayo na kudunga sindano na kuweka mayai yao ndani ya yai la kiwavijeshi vamizi na kwa namna hiyo wanamaliza kizazi cha Viwavijeshi vamizi kwenye shamba la mkulima na kubaki wao ambao hawana madhara.
Amesema utafiti huu ukikamilika utawasaidia wakulima kuondokana na matumizi ysiyofaa ya viuatilifu vyenye viambata sumu ambavyo ni hatari kwa afya zao na mazingira na zaidi sana hawa wadudu rafiki
watampunguzia Mkulima gharama za uzalishaji mazao ya chakula hasa mahindi na kuleta tija kwenye kipato cha kaya na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkulima Salehe Alfan Ally mkazi wa Dumila Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro amepongeza utafiti huo ambao utasaidia kulinda mazao yao kwa kuwa matumizi ya madawa wengi hawayawezi maana ni ghari na mwisho wa siku wanapata hasara wakati wa kuvuna.
‘’Awali tulizoea kulima mahindi bila kupulizia dawa tukawa tunapulizia dawa kwenye mashamba ya nyanya tu lakini toka mwaka 2017 walipokuja wadudu hawa Viwavijeshi Vamizi hali ya maisha yetu yamekuwa magumu unapata hasara maana sio wote wanamudu kununua madawa kupulizia
kila baada ya wiki mbili hadi tunapovuna na bado hawatoweki‘’ alieleza Bw. Salehe.
Aliongeza kuwa ‘’Yani inafika mahali tunaamua tu kuacha wadudu wale na kile kinachobaki ndicho tunachopeleka nyumbani kama mavuno ya mwaka na unakuta muda mwingine unapata gunia moja au mbili kwenye shamba la mahindi la ekari moja na unakuta mahindi yenyewe ni yale madogo
\madogo sana ambayo yameliwa hadi magunzi yamejikunja‘’.
Nae Afisa Kilimo Mwandamizi kutoka Kata ya Mlingano wilayani Muheza mkoani Tanga Bw. Jimmy Mhina amewapongeza watafiti hao wa SUA na TPHPA kwa kuja na ubunifu huo wa matumizi ya wadudu rafiki katika kukabiliana na Viwavijeshi Vamizi na kuomba jitihada hizo za majaribio zifanikiwe kwenye mashamba ili kumtua mkulima mzigo wa hasara
zinazosababishwa na wadudu hao hatari kwenye mazao.
‘’Wakulima wengi wanashindwa kununua mfano mbolea na hata mbegu bora sasa ujio wa wadudu hawa unawalazimisha gharama ya kununua Viuatilifu ambavyo ni ghali na hivyo wengi wao hawapigi dawa
wanahudumia shamba na kusubiri kile watakachobakisha wadudu hao ndio apeleke kwenye familia kwa kweli wanapata tabu na kuongeza umasikini kwa wakulima wetu‘’ alifafanua bw. Mhina.
Viwavijeshi Vamizi kutoka Amerika viliingia nchini mwaka 2017 kwenye mikoa michache lakini kufikia mwaka 2019 viliripotiwa kwenye mikoa yote ya Tanzania na kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ambao ndio wafadhili wa utafiti huo wanasema Viwavijeshi
Mdudu rafiki aina ya Telenomus remus,akitoboa na kutaga mayai yake kwenye mayai ya Kiwavijeshi Vamizi.
Mdudu rafiki aina ya Trichogramma mwanzae akitoboa na kutaga mayai yake kwenye mayai ya Kiwavijeshi. Vamizi
Mtafifti Mkuu kutoka SUA Prof.Gratian Rwegasira na wataalamu kutoka TPHPA wakiwa kwenye zoezi la kuweka wadudu hao rafiki kwenye mashamba ya wakulima Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro na Muheza mkoani Tanga.
Mtafifti Mkuu kutoka SUA Prof.Gratian Rwegasira na wataalamu kutoka TPHPA wakiwa kwenye zoezi la kuweka wadudu hao rafiki kwenye mashamba ya wakulima
Picha ya karibu ya namna Kiwavijeshi vamzi anavyoshambulia zao la Mahindi.
Sehemu ya picha anayoonesha wadudu hao rafiki wakiwa kwenye maabara kwenye Maabara za TPHPA kibaha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...