Na mwandishi wetu Dodoma.


Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeeleza kuridhishwa na ujenzi wa mradi wa maji katika kata ya Nzuguni wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 7.6 kwa siku ambao utaongeza upatikani wa maji kwa asilimia 11 na kupunguza makali ya mgao uliopo sasa.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi Job Masima, ameyasema hayo Agosti 3,2023,jijini Dodoma wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kutoa maelekezo kwa Mamlaka hiyo.

Balozi Masima, amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua maendeleo ya ujenzi wa maradi huo muhimu katika kupunguza uhaba wa maji jijini Dodoma.
"Huu ni mradi muhimu sana na mkubwa ambao utabadilisha sura ya upatikanaji wa maji katika jiji la Dodoma na mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi huu hivyo Bodi imeona ni vizuri kuja kuona maendeleo na tumeridhika na maendeleo ya mradi huu"amesema Balozi Masima

Aidha, amesema kwa namna mradi walivyouona ni matumaini yao kuwa utakamilika ndani ya mwezi huu na kuzinduliwa mapema mwezi Septemba 2023, ili kutoa ahuweni kwa wananchi kupata huduma ya maji ya uhakika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema mradi huo hivi sasa umefikia asilimia 76 ya ujenzi na kwa mujibu wa mkataba unapaswa kukamilika ndani ya mwezi huu.

"Mradi huu unaouwezo wa kuzalisha maji kiasi cha lita milioni 7.6 kwa siku hali ambayo inakwenda kuongeza kiasi cha upatikanaji maji katika jiji la Dodoma kwa asilimia 11"amesema Mhandisi Joseph

Pia, amesema uwezo wa uzalishaji maji kwa sasa katika jiji la Dodoma ni lita milioni 68 kwa siku hivyo kukamilika kwa maradi huo kutaongeza hadi kufikia zaidi ya lita milioni 75 kwa siku.

"Matenki ambayo yatatumika kuhifadhia maji tayari tumeshaagiza kutoka China moja litakuwa la lita milioni tatu na jingine lita 500,000 na maji yatakayopatikana hapa yatakuwa kwa ajili ya wakazi wa Nzuguni na ziada itakwenda katika maeneo mengine na kuongeza muda wa utoaji huduma"amesema

Kadhalika, Mkurugenzi huyo amesema mara baada ya mradi huo kukamilika wataingiza maji hayo katika mtandao ulipo ili kila mwenye bomba apate maji.
"Awali watu walikuwa na mabomba lakini hawana maji hivyo baada ya kusambaza maji katika mtandao uliopo tutapanua mtandao ili kuwafikiwa watu wote kwani awali tusingefanya hivyo kwakuwa hatukua na maji ya kutosha lakini hivi sasa tunayo yanaotosheleza mahitaji katika eneo hili la Nzunguni"amesema Joseph.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...