Na Muhidin Amri
Tunduru

BAADHI ya wakazi wa mji wa Tunduru wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameipongeza Serikali kupitia wakala wa Barabara za mijini na vijijini(Tarura) wilayani humo kwa kazi nzuri ya kujenga na kukamilisha mradi wa ujenzi wa Barabara za mitaa kwa kiwango cha lami.


Wamesema, Barabara za lami zilizojengwa kwa viwango bora katika mitaa yao zimesaidia sana kupendeza mji wa Tunduru na kuongeza  thamani ya maeneo yao,kuondoa changamoto ya usafiri na kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na wilaya ya Tunduru .


Sharifa Athuman alisema kabla ya ujenzi  huo,Barabara nyingi za mitaa katika mji wa Tunduru zilikuwa mbovu na hazikupitika kirahisi hususani kipindi cha masika,hivyo kusababisha wananchi kushindwa kufika kwa wakati pale wanapohitaji kwenda maeneo mengine.


Alisema,baada ya kujengwa kwa Barabara za lami mitaa yao imekuwa kimbilio kubwa kwa wageni wanaotafuta maeneo kwa ajili ya kujenga nyumba za kuishi na wengine  kuhitaji vyumba vya kupanga tofauti na hapo nyuma ambapo nyumba nyingi zilikaliwa na wenyeji.


Aidha alieleza kuwa,Barabara hizo zilizojengwa sambamba na kufungwa taa zimesaidia kuimarisha ulinzi na kukomesha matukio ya uharifu na waharifu ambao walitumia kuwepo kwa giza nyakati za usiku kutekeleza  vitendo viovu.


“tunamshukuru sana Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kutujengea Barabara za mitaa yetu kwa kiwango cha lami,kabla ya lami maeneo haya yalikuwa maficho makubwa ya vibaka ambao kwa sasa wamekimbilia maeneo mengine”alisema Sharifa.

Zuber Mtonyole alisema,ujenzi wa Barabara za lami katika mji wa Tunduru umeondoa adha ya mashimo barabarani na kupunguza maambukizi ya magonjwa ikiwemo kifua na mafua kutokana na kuwepo kwa vumbi kubwa lililoingia hadi ndani ya nyumba zao.


Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia Tarura kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara nyingine zilizobaki  katika mitaa yao ili ziweze kuchochea maendeleo na kuvutia wawekezaji wengi.

Kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Mhandisi Julius Msolwa alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023  Tarura  imetekeleza mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami  ya Misufini-Extended yenye urefu wa kilomita 1.7 kwa gharama ya Sh.milioni 769.


Alisema ujenzi wa barabara  hiyo ulianza mwezi Novemba 2022 na kukamilika mwezi Juni 2023 na sasa imekamilika na kuanza kutumika kwa wananchi kusafiri na kusafilisha bidhaa zao kwenda katika maeneo mbalimbali ya mji wa Tunduru kwa ajili ya kufuata masoko.


Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Tarura inatarajia  kutekeleza mradi mwingine wa Barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 2.6 ambao utaanza mwezi oktoba na sasa upo kwenye hatua ya manunuzi.

Msolwa alisema,serikali inatoa fedha kwa ajili ya kujenga Barabara na kuboresha miundombinu yake,hata hivyo changamoto kubwa katika wilaya hiyo ni wananchi kugeuza mitaro kama dampo na baadhi ya madereva kuzidisha uzito wa magari yao zaidi ya tani 10.
MWISHO.

Uwekezaji wa alama za barabarani katika barabara ya lami ya Misufini-Extended wilayani Tunduru ikiendelea kwa ajili ya kudhibiti uzito wa magari na matumizi yasiyozingatia sheria ili kuiwezesha barabara hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.

Barabara ya Misufini-Extended yenye urefu wa kilomita 1.7 iliyojengwa na wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilayani Tunduru ikiwa imefikia asilimia 99 ya ujenzi wake na kuanza kutumika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...