-Benki zajipanga kutengeneza fursa za masoko na Teknolojia

- Watanzania wakumbushwa kuweka akiba ya chakula 

SERIKALI imewataka watanzania kutumia kongamano la Afrika la Mifumo ya Chakula la mwaka 2023 kama fursa katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji pamoja na mazao huku taasisi za kifedha zikiwemo benki zikiahidi kupiga kambi katika kongamano hilo litakalofanyika nchini kuanzia Agosti tano hadi nane mwaka huu kutafuta fursa za masoko na Teknolojia kutoka mataifa mbalimbali.

Hayo yameeelezwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Gerald Mweli  leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano uliowakutanisha wahariri na waandishi wa vyombo vya habari na taasisi za kifedha zikiwemo benki za NMB, CRDB, NBC, EQUITY na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB,) ambazo zimetoa taarifa mbalimbali za program na huduma zinazotolewa ikiwemo masuala ya kilimo biashara na mitaji ya fedha.

Mweli amesema, kufanyika kwa mkutano huo nchini ni fursa katika kujitangaza kitaifa na kimataifa na kwenda agenda ya nchi ya kufanya kilimo cha biashara na kuleta tija kwa Taifa.

"Tunatarajia kupokea washiriki wapatao 3300 kutoka nje ya nchi ambao watakuja nchini kushiriki mkutano huu, tumejiandaa na kuwaandaa wafanyabishara kuelekea mkutano huu ambao utaota fursa nyingi za masoko, teknolojia na uwekezaji nchini....Tumeandaa maeneo maalum ya mazungumzo ya kibiashara na washiriki watakaokuja na hii ni pamoja na kubadilishana uzoefu pia vijana 130 kutoka nchini ambao ni wakulima watashiriki na kuonesha nini wanafanya na kujitangaza Kimataifa." Amesema.

Aidha amesema licha ya Serikali kuruhusu biashara ya chakula ndani na nje ya nchi watanzania lazima waweke akiba ya chakula ili kusaidia familia pindi shughuli za kilimo zinaposimama ili kuepukana na njaa.

Mweli amesema licha ya kuwepo kwa changamoto katika sekta ya kilimo bado kuna fursa kupitia benki mbalimbali ambazo zinafanya kazi kwa ukaribu za Serikali zikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB,) NMB, CRDB, NBC na Equity.

Pia Mkuu wa kitengo Cha Kilimo-Biashara wa benki ya EQUITY Teofora Madilu amesema, licha ya benki hiyo kutoa mikopo kwa  wakulima wadogo, wafanyabishara wadogo na kushirikiana kwa karibu na sekta ya kilimo wataendelea kushirikiana katika kutoa fursa za elimu na mikopo ili kuiboresha zaidi sekta hiyo.

"Mkutano huu ni fursa kubwa kwa Taifa tushirikiane ili kuipaisha sekta ya kilimo na kuvutia wawekezaji kwa kuwa rasilimali zipo za kutosha, tuendeleze malengo ya kuifanya Tanzania kuwa kapu la chakula Afrika na dunia kwa ujumla kama Rais anavyopambana kutangaza rasilimali zilizopo." Amesema.

Ameeleza kuwa Serikali kwa ushirikiana na wadau washirikiakaiane katika kutangaza fursa za uwekezaji hususani katika Kilimo cha umwagiliaji na zana za kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Kilimo- Biashara kutoka benki ya CRDB, Maregesi Shaban amesema benki hiyo imekuwa mdau mkubwa anayefanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha uwekezaji nchini unapaa kwa vya Kimataifa.

Amesema, benki hiyo kupitia taasisi tanzu iliyoanzishwa na benki hiyo wanatoa mafunzo ya kuendesha biashara kwa vijana na akina mama wenye mawazo bunifu pamoja na kuwapatia mikopo na hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa vijana waliopo katika vituo atamizi  katika sekta za kilimo na uvuvi kwa kuwapa elimu, mitaji na maeneo ya kafanyia shughuli hizo ili waweze kujiendesha kibiashara.

Kuelekea mkutano huo ameeleza kuwa; watashiriki kikamilifu kwa kukutana na wadau washiriki wa mkutano huo kwa kubadilishana uzoefu wa kiteknolojia ili kuhama kutoka uzalishaji wa kujikimu kwenda katika uzalishaji wa kibiashara, kutafuta fursa za masoko pamoja na kuendeleza uhusiano.

Amesema wamekuwa walishiriki katika kusaidia kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo kuwawezesha wakandarasi wakubwa wa reli ya kisasa ya SGR, ujenzi wa miundombinu ya barabara, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 3,  pamoja na miradi ya nishati ukiwemo mradi wa umeme wa mwalimu Nyerere.

Vilevile Mshauri wa idara ya kilimo, uvuvi na ufugaji kutoka benki ya NMB Isaac Msasu amesema kutokana na umuhimu wa sekta hizo benki hiyo kupitia Taasisi ya NMB Foundation waliunda idara hiyo ili kuwawezesha walengwa kuzalisha kwa tija katika maeneo yao.

Ameeleza, wamekuwa wakitoa mikopo ya muda mrefu hadi kufikia shilingi bilioni moja kwa mtu moja ili waweze kuwekeza katika teknolojia na kuongeza thamani ya mazao na kupitia mkutano huo watatafuta fursa zaidi zitakazoleta maendeleo zaidi ya kisekta kwa mtu mmoja na Taifa kwa ujumla.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa kongamano hilo litaleta tija kwa watanzania na Taifa kwa ujumla hususani katika kupata fursa ya masoko kimataifa pamoja na kubadilishana teknolojia. Leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa kongamano hilo ni fursa kwa watanzania katika kubidhaisha sekta ya Kilimo Kimataifa, Leo jijini Dar es Salaam.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...