WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za fedha nchini kuendelea kubuni huduma zinazolenga kutatua changamoto zinazowagusa wakulima huku akionyesha kuguswa zaidi na hatua ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kuwekeza nguvu zaidi kwenye utoaji wa mikopo ya zana za kilimo kwa wakulima nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa wito na pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Mwakangale mjini Mbeya. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa utoaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa zana za kilimo utasadia kuchochea mapinduzi ya kilimo kwa kuchochea kasi ya uzalishaji na ongezeko la mapato kwa wakulima.
‘’Siku zote serikali imekuwa ikisisitiza na kuziomba taasisi mbalimbali za kibenki kuongeza juhudi kwenye ubunifu wa huduma zake ili zije na huduma zinazoonekana kutatua kero za makundi mbalimbali kulingana na mahitaji yao mahususi. Na hii ndio sababu nawapongeza benki ya NBC ambapo kupitia mkakati wa NBC Shambani wanaweza kuwasaidia wakulima wengi kupata mikopo ya zana muhimu za kilimo…hongereni sana NBC,’’ alipongeza.
Awali akifafanua kuhusu mikopo hiyo Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa alisema kupitia ushirikiano na kampuni ya kuuza pembejeo za kilimo ya Agricom Africa benki hiyo tayari imefanikiwa kutoa mikopo ya zana za kilimo zenye thamani ya Sh bilioni 2.3 kwa wakulima mbalimbali nchini.
‘’Hatua yetu hii ni mwendelezo tu wa jitihada zetu nyingi tunazozielekeza kwenye sekta ya kilimo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua sekta ya kilimo nchini.’’ Alisema Urassa.
Zaidi, katika kuthibitisha dhamira hiyo benki hiyo mwishoni mwa wiki ilikabidhi mkopo wa trekta na jembe vyenye thamani ya Sh milioni 62.1 uliotolewa kwa Mkulima wa mpunga Evarist Msasi kutoka wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya zana hizo iliyofanyika kwenye viwanja hivyo, Urassa alibainisha kuwa tangu walipoingia ubia na kampuni Agricom, NBC imeshawezesha kuwapatia wakulima mikopo ya matrekta 20, mitambo ya uvunaji (combiner harvester) 15 na power tiller 10
“NBC itaendelea kuunga mkono kwa vitendo dhamira ya serikali inayolenga kufanikisha ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030’’ alibainisha Urassa huku akiwakaribisha wakulima kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo ya zana za kilimo sambamba na kufungua akaunti ya NBC Shambani.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona ambaye alikuwa mgeni rasmi aliipongeza NBC pamoja na Agricom Africa kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua sekta ya kilimo nchini.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanaondokana na kilimo cha mazoea ambacho hakina faida kwa pato la mtu mmoja mmoja huku akitumia fursa hiyo kuwasihi wakulima kuwekeza zaidi kwenye zana bora za kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom Alex Duffar ameishukuru NBC kwa kuendelea kuwa mbia mzuri huku akibainisha kuwa katika kipindi kifupi cha ushirikiano na benki hiyo kampuni hiyo imefanikiwa kuchochea mauzo yake mara 10 zaidi ya mwaka jana.
Akizungumza mara tu baada ya kukabidhiwa zana hizo, mkulima Evaristo Msasi aliishukuru benki ya NBC kwa kuwafungulia fursa ya mikopo hiyo yenye riba nafuu kwa wakulima huku pia akiahidi kutumia vema zana hizo ili kujinufaisha yeye na jamii yote inayomzunguka,
Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa ( wa tatu kulia) sambasamba na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom Alex Duffar (wa tatu kushoto) wakimkabidhi mfano wa ufunguo wa trekta mkulima wa mpunga Evarist Msasi kutoka wilayani Mbarali mkoani Mbeya ikiwa ni mkopo na benki ya NBC. Hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika kwenye kwenye Maonyesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika katika Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya leo. Wengine ni maofisa wa benki hiyo pamoja kampuni ya Agricom.
Mkulima wa mpunga Evarist Msasi kutoka wilayani Mbarali mkoani Mbeya (juu ya trekta) akijaribu ubora wa trekta alilokabidhiwa kwa mkopo na benki ya NB
Akizungumza mara tu baada ya kukabidhiwa zana hizo, mkulima Evaristo Msasi aliishukuru benki ya NBC kwa kuwafungulia fursa ya mikopo hiyo yenye riba nafuu kwa wakulima huku pia akiahidi kutumia vema zana hizo ili kujinufaisha yeye na jamii yote inayomzunguka
Hongera sana
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...