SERIKALI Imeeleza umuhimu wa kada ya Famasia nchini katika kukuza na kuimarisha sekta ya afya na kuahidi kuendelea kuthamini jitihada hizo kwa kuweka mazingira bora ya utendaji kazi pamoja na kutatua changamoto zinazoikabili.

Hayo yameeelezwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel katika siku ya Wafamasia duniani iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam na kutanguliwa na mkutano ulioratibiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC,) na kuwakutanisha watendaji mbalimbali wa sekta ya dawa wakiwemo wazalishaji, watoa mafunzo katika vyuo vya ngazi ya juu na kati, Wafamasia na wanafunzi wanaosomea kada hiyo.

Dkt. Mollel amesema, Wafamasia ni mhimili mkubwa katika kada ya afya na kuwataka wataalam hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

"Hakuna hospitali inayoweza kutoa huduma bila kuwepo kwa kada ya Famasi, tunathamini jitihada zenu muendelee kufanya kazi kwa bidii kama tunavyojua asilimia 53 hadi 58 ya mapato hospitalini hutegemea dawa.... Serikali kupitia Wizara tupo pamoja kwa kushirikiana na wadau katika kuhakikisha tunapata wawekezaji na fursa za mafunzo kwa wataalam wetu ili kuboresha huduma kwa wagonjwa." Amesema.

Akijibu changamoto zinazoikabili fani hiyo, Dkt. Mollel amefafanua kuwa;

"Wafamasia wanapoongeza elimu haitambuliki, wanaosoma miaka mitatu hadi nane malipo yanafanana hii inasababisha wataalam wasijiendeleze kielimu, hili limeshaanza kufanyika kazi katika bajeti ijayo mambo yatakuwa sawa.....Pia kuhusu uchache wa namba za ajira za famasi hili litaenda Bungeni lazima lipate ufumbuzi wa kiutekelezaji haiwezekani ajira za manesi ziwe 800 na Wafamasia ziwe 50 hii haitakidhi hospitali zetu kuanzia ngazi ya chini, tunalifualitia kwa ukaribu...Pia kuhusiana na suala la utofauti wa mitaala limepokelewa na Jumatatu tutakutana na Waziri wa Elimu kujadili hili ili kuwa na mitaala inayofanana." Amefafanua Naibu Waziri Mollel.

Vilevile Dkt. Mollel ameipongeza CSSC ambao ni wasimamizi wa Hospitali za Kanisa kwa kuandaa mkutano huo pamoja na kuendelea kutoa huduma na kuwataka kuendelea kuzisimia kwa kuwa zina mchango mkubwa katika sekta ya Afya na hiyo ni pamoja na kuandika mapendekezo kwa wadau kuhusu ufadhili wa bunifu na gunduzi zihusuzo kada ya Afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC,) Peter Maduki ameeleza kuwa katika kuadhimisha siku ya Wafamasia duniani wamekutana kumshukuru Mungu pamoja na kujipongeza kupitia shughuli wanazozifanya pamoja na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kada hiyo muhimu inayohusu Afya.

Amesema idadi ya Wafamasia kwa sasa ni takribani 3000 na hiyo ni kutokana na juhudi za Serikali katika kupanua wigo wa vyuo vya kutoa mafunzo pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika kuhakikisha wataalam hao wanapata mafunzo yanayokidhi mahitaji.

"Tunatambua jitihada za Serikali pamoja na taasisi mbalimbali katika kupunguza usugu wa dawa kwa jamii kupitia wataalam hawa na hii ni pamoja na jitihada za kuwaleta pamoja wadau wanaotoa huduma za dawa na kujadili mafanikio, changamoto na mapendekezo kuhusu kada hii." Ameeleza.

Akieleza changamoto zinazoikumba kada ya Ufamasia, Maduki ameeleza kuwa moja ya changamoto ni kukosekana kwa data za kuwatambua Wafamasia na kutambua idadi ya wataalam hao wanaohitajika katika kutoa huduma.

"Pia changamoto nyingine inayoikabili kada hii ni suala la mitaala ni vyema wataalam wakapata mafunzo yanayolingana katika vyuo vyote, Hata hivyo wataalam hawa bado wachache hawatoshelezi kwa mahitaji yaliyopo." Amesema.

Aidha, amewataka Wafamasia kushirikiana na kwa kufanya kazi ya kutoa huduma kwa kutumia rasilimali zilizopo na hiyo ni pamoja na kuboresha mawasilisho baina ya Wafamasia.

Katika mkutano huo jumuiya hiyo ilitoka na mapendekezo yaliyowasikishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC kwa Serikali kwa hatua zaidi za kiutekelezaji ambayo ni pamoja kuwepo kwa zana za kufundishia ili jamii iweze kuelewa namna ya kutumia dawa kwa usahihi ili kupunguza usugu wa dawa.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akizungumza wakati wa mkutano huo na kuwataka wataalam hao kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na kuahidi kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kutatua changamoto zinazoikabili kada hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.
Msajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth Shekilaghe akizungumza wakati wa mkutano huo na kuwataka wataalam hao kutumia fursa za mafunzo pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kada hiyo. Leo jijini Dar es Salaam.Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...