Na Mwandishi Wetu.

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), imefanikiwa kudhibiti ndege wasumbufu milioni 5 waharibifu wa mazao na kuokoa hekari 1,000 katika kata ya Kisangaji mkoani Manyara.

Aidha, TPHPA imesema ina mpango wa kuanzisha mfumo wa utabiri kutabiri ili kuweza kufahamu tatizo la mlipuko lilipo kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Gladman Mbukonyi Mtaalamu wa Kudhibiti Visumbufu vya Mimea TPHPA, wakati wa zoezi la kudhibiti ndege waharibifu wa zao la mpunga mkoani humo.

Mtaalam huyo amesema katika kata hiyo ya Kisangaji wameweza kuokoa hekari 1,000 ambazo zingeshambuliwa na visumbufu ndege.

"Hapa katika hii ya Kisangaji tumeweza kudhibiti ndege milioni 5 wasumbufu wa mimea ambao wana uwezo wa kuharibu tani 50 kwa siku moja,"amesema.
Mbukonyi amesema ndege hao wangeachwa wangeweza kuharibu zaidi ya hekari 1,000 kwa muda mchache hali ambayo ingekwamisha jitihada za wakulima.

Amesema mikakati yao TPHPA ni kuhakikisha mkulima anafurahia kushiriki katika kilimo, hivyo watatoa ushirikiano pale watakapohitajika.

Kaimu Meneja wa Usimamizi wa Visumbufu vya Mlipuko TPHPA, Godlove Kirimbo amesema katika kuhakikisha wanakabiliana na visumbufu hivyo wamenunua drone zakutambua vilipo visumbufu na kupuliza dawa ili visilite madhara kwa wakulima.


"TPHPA kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Umoja wa Ulaya (EU), tumenunua drone ambazo zinatambua vilipo visumbufu na kunyunyiza dawa, hivyo mazao ya wakulima yatakuwa salama, " amesema.
Kaimu Meneja huyo amesema pia wanatarajia kununua ndege mpya ambayo inasaidia kupambana na visumbufu hivyo.

Kirimbo amesema kubwa zaidi ambalo lipo kwenye mipango wa mamlaka ni kuanzisha mfumo wa utabiri ambao utawezesha wao kutambua na kufika kwa wakati kudhibiti visumbufu. Kaimu Meneja huyo amesema mfumo huo utashirikisha wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa kilimo, ili waweze kupata taarifa kwa wakati na kuchukua hatua stahiki.

"Natoa wito kwa wakulima kushirikiana na halmashauri katika kutoa taarifa ili tuweze kukabiliana na visumbufu," amesema.

Naye Kaimu Meneja wa TPHPA Kanda ya Kaskazini, Juma Mwinyimkuu amesema visumbufu vya mlipo vinachangia kupungua kwa tija ya uzalishaji kwa wakulima, hivyo watahakikisha wanavidhibiti ili kununua mkulima. Amesema TPHPA kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo zitahakikisha visumbufu vyovyote vinadhibitiwa ili kuongeza tija ya uzalishaji na kukuza uchumi.

"Jitihada zetu za kudhibiti visumbufu kama ndege, zinaenda kuifanya Tanzania kutekeleza Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) lengo namba moja la kuondoa umaskini na lengo namba la kuondoa njaa," amesema.

Mtaalam wa Viuatilifu na Afya ya Mimea Halmashauri ya Babati, Kanas Sulu amesema ili kuwadhibiti ndege hao wasumbufu wamekuwa wakiamka saa kumi alfajir, kwani kinyume na hapo wakulima wa mpunga wilayani hapo wangekosa mavuno.

Amesema operesheni hiyo ilitekelezwa na TPHPA itawezesha wakulima kupata mavuno ambayo yatawaingizia kipato wao na halmashauri.

Mwenyekiti wa kijiji cha Shaurimoyo, Florian Ngowi amesema tangu kijiji hicho kianzishwe hawajawahi kuona ndege ikifukuza ndege waharibifu wa mazao, hivyo wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwakumbuka wakulima.

Ngowi amesema wakulima wa mpunga na mazao mengine wamezoea kutumia udongo kufukuza visumbufu vya mazao, hivyo ujio wa ndege utawawezesha kujikita na shughuli zingine za kiuchumi. 


"Miaka ya nyuma ukulima unapaswa kukataa shamba muda wote, hivyo tunashindwa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi, ila ujio wa ndege hizi zinafukuza visumbufu kama ndege ni jambo jema," amesema.

Mwenyekiti huyo amesema ujio wa ndege utawezesha wakulima kuwa na afya nzuri na kusomesha watoto wao katika shule nzuri, kwani mavuno na kipato vitaongezeka.

Kwa upande wake Mkulima wa Mpunga, Mariam Gadiel amesema matumizi ya ndege za kufukuza na kuuwa ndege waharibifu umewapunguzia gharama katika kilimo.

Gadiel amesema awali walikuwa wanakodisha vijana kwa ajili ya kufukuza ndege, hivyo kulazimika kuwalipa fedha nyingi hadi kufikia wakati wa kuvuna.

"Tulikuwa tunashindwa kuwapikia watoto wetu, kwani muda wote tulikuwa tunatumia shambani, ila sasa tunarudi nyumbani kufanya kazi zingine, tunawashukuru TPHPA na serikali ya Raisi Samia kwa kutukumbuka wakulima, hasa sisi wakina mama, " amesema.











 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...