Na WILLIUM PAUL, DODOMA.

MBUNGE wa Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Anne Kilango Malecel amesema kuwa chama cha Mapinduzi katika jimbo hilo kilidhohofika kutokana na Jimbo hilo kuwa upinzani kwa kipindi cha miaka mitano 2015-2020.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo wakati wa semina maalum aliyoiandaa kwa Wenyeviti, Makatibu, Makatibu wenezi pamoja na Madiwani wa Chama cha Mapinduzi kata za jimbo hilo iliyofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa jijini Dodoma ambapo pia walipata fursa ya kujionea shughuli za Bunge zikiendelea.

Alisema kuwa, kutoka na jografia ya wilaya ya Same yenye majimbo mawili ya Same mashariki na Same magharibi viongozi wa Chama wilaya wanahitaji msaada kutoka kwa Mbunge ili kufika katika Jimbo la Same mashariki hivyo kutokana na Jimbo kuwa upinzani walikuwa wakikutana na changamoto kubwa kufika.

"Natambua chama chetu katika Jimbo letu kilizohofika sana na hii ni kutokana na Jimbo kuongozwa na upinzani sasa ndio kama tunaanza kukijenga upya chama na kwa kutambua hili nimeona niwalete viongozi wa Chama kata mje kutapa elimu ya jinsi ya kuongoza ili mkafanye shughuli zenu kwa ufanisi mkubwa kwa maslahi ya Chama" alisema Anne Kilango.

Mbunge huyo alisema kuwa, viongozi wa Chama katika Jimbo la Same mashariki wamedhamiria kuhakikisha chama kinashinda kuanzia uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani pamoja na uchaguzi mkuu wa 2025 ambapo kazi ya kuanza maandalizi ya ushindi zimeshaanza.

Anne Kilango alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa mafunzo aliiomba Ofisi na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa kutoa wakufunzi watakaotoa mada mbalimbali lengo likiwa ni kuwajengea uwezo viongozi hao katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akitoa mafunzo hayo, Katibu Msaidizi Mwandamizi Mkuu wa Sehemu ya Vikao na Maamuzi ya Chama Idara ya Oganaizesheni Taifa, Kajoro Vyohoroka aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanaingiza wanachama wapya kwani ndilo litakalopelekea chama kuendelea kushika Dola.

Vyohoroka alisema kuwa, ni wajibu wa kila Kiongozi ndani ya Chama kuweka mikakati ya kuongeza wanachama wapya pamoja na kuendelea kuwalinda na kuwaheshimu wale waliopo na kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

"Viongozi tunawajibu wa kuhakikisha tunaimarisha madaftari yetu ya wanachama kwenye matawi na kuwapa heshima mabalozi wetu kwani wao ndio wapo karibu zaidi na wapiga kura wetu na watatusaidia kuwapata wanachama wapya" alisema Vyohoroka.

Aidha Mkufunzi huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaonya Madiwani kuacha tabia ya kuwalipa ada za uanachama wanachama kipindi cha uchaguzi na badala yake kuwajengea misingi bora ya kila mwanachama kujilipia mwenyewe ada.

Katika hatua nyingine alitumia nafasi hiyo kuwasihi viongozi wa chama kuanzia kwenye matawi, shina, kata, wilaya na mkoa kuhamasisha wanachama wa CCM kujisajili kwenye mfumo wa kieletroniki.

Pia alisema kuwa, CCM ni daraja la kuwasemea na kuwasikiliza watu na kuwataka viongozi kuishi katika njia hiyo ili chama kiendelee kuaminiwa na wananchi na kuendelea kuwa kimbilio lao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...