Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kupitia Programu ya Serikali ya Shule Bora kwa ufadhili wa UKAID inaendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Wawezeshaji wa Vituo vya Utayari vilivyopo katika Halmashauri 11 za jiji la Tanga.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wawezeshaji waliopo katika vituo vya utayari kwa ajili ya kuwasaidia watoto kujenga utayari wa kuanza Darasa la Kwanza kwa mwaka 2024. Watoto hao wanaoandaliwa katika vituo hivyo ni wale waliokosa fursa ya kusoma madarasa ya awali kutokana na changamoto ya umbali au uwepo wa mazingira hatarishi kufika shuleni.

Akifungua mafunzo hayo katika Chuo cha Ualimu Korogwe jijini Tanga, Mratibu wa Programu ya Shule Bora kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bwana
Lawrence Sanga amewataka wawezeshaji hao kushiriki kikamilifu katika mafunzo watakayopewa ili waweze kuyafanyia kazi katika vituo vyao vya utayari.

“Serikali inaendelea kutoa nafasi ili watoto ambao hawajapata nafasi ya kujiunga na madarasa ya awali kupata fursa ya elimu hivyo ninyi kama wawezeshaji hakikisheni mnazingatia mafunzo na kuyaelewa vizuri "amesema Bwana Sanga.

Pia, amewashukuru wafadhili wa Programu ya Shule Bora kwa kuwezesha mafunzo kuendelea kufanyika.

Kwa upande wake Mratibu wa Shule bora TET, Bi. Mariam Japhet amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawasaidia wawezeshaji hao kujenga umahiri wa kuwaandaa watoto kuwa tayari kuanza shule.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tano kuanzia leo tarehe 11 -15/9/2023.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...