Na Janeth Raphael - Michuzitv Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais , Muungano na Mazingira, Dkt.Selemani Jafo amewaonya wanaosafirisha taka hatarishi nje ya nchi bila kibali hatua inayoisababishia Serikali mapato yanayotokana na tozo, ada na kodi zinazopaswa kulipwa.

Pia, amzielekeza Mamlaka za udhibiti zilizopo kwenye maeneo ya mipaka mbalimbali nchini kuhakikisha shehena yoyote ya taka hatarishi inayosafirishwa nje ya nchi au inayoingizwa nchini na kupitishwa kwenye mipaka ya nchi inakuwa na kibali kilichotolewa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira. 

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za usafirishaji wa chuma chakavu aina ya chuma dongo (Cast Iron) nje ya nchi licha ya kutokutolewa kwa kibali hicho tangu Machi hadi Septemba, 2023.

Akizungumza leo Septemba 22, 2023 jijini Dodoma, Waziri Jafo amesema kuwa suala hili husababisha kupungua kwa fursa za ajira kwenye viwanda vinavyotumia chuma chakavu aina ya chuma dongo kama malighafi ya kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nondo.

“Ikumbukwe kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo mkubwa katika suala la uwekezaji wa viwanda vya ndani kwa lengo la kuzalisha ajira na kukuza uchumi na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za chuma chakavu ikiwemo chuma dongo (Caste Iron) nje ya nchi kiholela na usiofuata utaratibu unaweza kusababisha upungufu wa malighafi kwenye viwanda vinavyotumia malighafi za aina hiyo hapa nchini kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo nondo na bomba za chuma,”.

“Upungufu wa malighafi unaweza kusababisha kupungua kwa ajira kwa vijana wanaofanya kazi katika viwanda vyetu vya ndani pamoja na kupanda kwa bei za bidhaa aina ya nondo na bomba za chuma ambazo zinatumika sana katika shughuli za ujenzi wa nyumba za wananchi, ujenzi wa majengo ya serikali na sekta binafsi, pamoja na ujenzi wa wamiundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, reli, madaraja, na mabwawa ya kuzalisha umeme,” amesema Dkt. Jafo. 

Hivyo, amewataka wananchi na wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya taka hatarishi nchini kuzingatia matakwa ya Kanuni Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za Mwaka, 2021 ikiwemo kuwa na kibali kilichotolewa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt Selemani Jafo akizungumza na wanahabari ( Hawapo pichani) Leo Jijini Dodoma


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...