Na Jane Edward, Arusha
Ripoti ya mauaji ya makusudi dhidi ya wanawake Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita imezinduliwa Rasmi Jijini Arusha ambapo wanawake 2,438 waliuawa.
Hayo yamebainishwa jijini Arusha mara baada ya uzinduzi huo uliofanyika katika wiki ya Asasi za Kiraia, Mkurugenzi wa kituo hicho Dr. Anna Henga amesema matokeo ya utafiti huo umehusisha pia jeshi la polisi kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ikionyesha wastani wa wanawake 492 waliuawa kila mwaka na wanawake 43 waliuawa kila mwezi katika kipindi hicho.
Dr. Henga amesema hadi kufikia Septemba 2022, tayari mauaji 472 ya wanawake yametokea ambayo ni sawa na wastani wa matukio 53 ya wanawake wanaouawa kwa mwezi kutoka wanawake 43 kuuawa kwa mwezi na kuongeza kusema kuwa "hii inaashiria wastani wa ongezeko la wanawake 10 zaidi wanaouawa kwa mwezi kutoka kwa wale waliuawa katika miaka mitano iliyopita"
Ametaja baadhi ya sababu zinazopelekea mauaji hayo kuwa ni wivu wa mapenzi, mila na desturi potofu, imani za kishirikina, ugomvi wa mali, elimu duni, mfumo dume pamoja na utegemezi wa kiuchumi.
Katika kushughulikia changamoto hiyo ripoti imetaja baadhi ya mapendekezo ya kisera na kiprogramu na kusema kuna haja ya kuwa na sheria ya kina kuhusu ukatili wa Kijinsia ambayo pia itakuwa inashughulikia mauaji ya wanawake, unyanyasaji wa nyumbani na ulinzi wa walionusurika na matukio hayo kuliko ilivyo hivi Sasa ambapo makosa hayo yanaangukia kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Pia ripoti hiyo imeiomba serikali kupitia Wizara ya Afya kutengeneza takwimu maalumu kuhusu masuala ya jinsia na mauaji ya wanawake na wasichana ili kufuatilia mienendo na kuelewa ukubwa wa tatizo kwa kuimarisha ufuatiliaji na uchunguzi wa mauaji ya wanawake.
Kamishna Msaidizi wa jeshi la polisi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi kwa Mtoto dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, Tulibake Kasongwa amesema serikali imeanzisha madawati ya Jinsia 420 katika vituo vya polisi nchini ili kukabiliana na Matukio kama hayo hali iliyopelekea mauaji ya wanawake kupungua Kwa asilimia mbili kutoka vifo 305 hadi 298 kati ya mwaka 2020 hadi 2023.
Nao baadhi ya viongozi wa dini Mchungaji Richard Hananja amewaataka wadau wa maendeleo nchini kuibua mijadala chanya itakayoweza kuleta utu na thamani ya mtu huku akizitaka Taasisi za dini kushirikisha wataalam wa sheria wakati wa kufungisha ndoa ili watoe elimu juu thamani ya mtu bila kuangalia jinsia yake.
Uzinduzi wa kitabu cha ripoti ya Mauaji ya makusudi dhidi ya Wanawake kikizinduliwa Rasmi Jijini Arusha katika Mkutano wa wiki ya Azaki.
Mchungaji Richard Hananja akizungumzia suala la ukatili mara baada ya Uzinduzi wa kitabu hicho.
Mjadala wa ukatili dhidi ya Wanawake ukiendelea jijini Arusha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...