Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) akiambatana na wajumbe, amefanya kikao na viongozi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Comrade Juma Zuberi Homera. Washiriki wengine wa Kikao hicho walikuwa ni Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tawala, Wenyeviti wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama na viongozi wengine katika Mkoa. Mkutano huo ni njia mojawapo ya kuimarisha agenda ya Kitaifa ya kuhakikisha kilimo kinaongeza mchango wake kwenye uchumi wa nchi.

Kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 18 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kililenga pamoja na mambo mengine kuweka mikakati ya kuhakikisha ruzuku inawafikia wakulima kwa wakati na karibu na maeneo yao sambamba na udhibiti wa uhalifu hasa katika kuvusha/ kutorosha mbolea nje ya nchi.

Dkt. Diallo amewaomba viongozi hao kushirikiana na TFRA kikamilifu katika kuhakikisha mbolea hizo zinawafikia wakulima mpaka ngazi ya kata na hivyo kuifanya dhana ya ruzuku kuleta maana kwa kupunguza adha ya wakulima kusafiri mwendo mrefu kufuata mbolea.

Aidha, Dkt. Diallo amesisitiza suala la usahihi wa taarifa na kueleza kuwa kumekuwa na tofauti ya taarifa kati ya zile zinazotolewa na mawakala wa mbolea na zile zinazopatikana katika ngazi za Kata na Wilaya na kuwataka watendaji kutumia taaluma zao vizuri katika kuhakikisha usahihi wa takwimu ili watendaji kufikisha pembejeo za kilimo zinazokidhi mahitaji halisi ya wakulima.

"Watu wanakusanyia taarifa (data) maofisini na zinapokusanywa kutoka ngazi ya kata zikawasilishwa wilaya hazifanyiwi Uhakiki, niwaombe sana muwe mnafanya verification ili kuepusha changamoto zinazotokana na taarifa zisizo sahihi" Dkt. Diallo ameongeza.

Pia Dkt. Diallo amezungumzia suala la utororoshwaji wa mbolea katika maeneo ya mipakani na kuwaomba viongozi kushiriki katika ulinzi na kuhakikisha mbolea zinawafikia walengwa na kutimiza nia ya Serikali ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa watanzania.

Pamoja na hayo, Dkt. Diallo amewaomba viongozi hao kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya vifaa vya kupimia afya ya udongo vilivyotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kujua afya ya udongo hivyo kuwawezesha kutumia mbolea sahihi kulingana na mahitaji ya udongo na mmea.

"Bila kujua afya ya udongo hakuna haja ya kutumia mbolea" Dkt. Diallo alikazia.

Katika kutatua changamoto ya umbali wa wakulima kufuata mbolea, Dkt. Diallo ameziomba Kamati za Pembejeo za Wilaya kushiriki kikamilifu katika kupanga bei ya mbolea kwa kuwasilisha mapendekezo ya bei kulingana na umbali wa kata ya mwisho kutoka makao makuu ya halmashauri ya wilaya husika.

Amesema ili kufanikisha hilo, amewashauri mawakala wa mbolea kuunda vyama vitakavyosaidia katika kutoa maoni kwenye vikao vya kamati za pembejeo za Wilaya na kuziwasilisha kwenye Mamlaka ili taarifa hizo zitumike wakati wa kupanga bei za mbolea na kueleza hali hiyo itasaidia kuongeza pato la taifa kwa kupitia kilimo.

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa Juma Homera amewataka viongozi hao kutilia maanani suala zima la usajili wa wakulima na kushauri vyombo vya habari vitumike katika kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kujisajili na kuhuisha taarifa zao kwa wale waliojisajili msimu uliopita wa kilimo na kubainisha hakuna mbolea itakayouzwa nje ya mfumo wa ruzuku.

Aidha, ameiomba Mamlaka kuhakikisha mbolea inafika kwa wakati, ikiwa inatosheleza mahitaji ya wakulima kabla ya msimu ili kufanya maandalizi ya msimu wa kilimo kwa wakati na hivyo kuongeza tija kwa wakulima.

Amesisitiza na kuwasihi maafisa ugani kusimamia suala la kupima afya ya udongo kutokana na umuhimu wake utakaowawezesha wakulima kujua aina ya mbolea inayopaswa kutumika na kuongeza uzalishaji ndani ya Mkoa.

 

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homeri (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo aliyepoambatana na baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo na menejimenti ya TFRA ofisini kwake kueleza dhumuni la kutemebelea mkoa huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha changamoto za kimfumo na uhaba wa mawakala wa mbolea vinatatuliwa kabla ya msimu kuanza.
 

Viongozi waandamizi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe.  Juma Homera (hayupo pichani), Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wakiwa katika kikao kilichoshirikisha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili kupanga mikakati ya kufikisha mbolea ya ruzuku ngazi ya Kata na kuwapunguzia umbali wa kufuata bidhaa hiyo wakulima.  Kikao kimefanyika  katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa tarehe 18 Oktoba, 2023
 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya,  Said Madito akizungumza na washiriki wa kikao kilichowahusisha viongozi waandamizi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,  Juma Homera (katikati), Wajumbe wa Bodi ya  wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi  Dkt. Anthony Diallo kilicholenga  kuhakikisha wakulima wananufaika na mbolea za ruzuku na kuongeza tija tarehe 18 Oktoba, 2023.
 

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, Dkt. Anthony Diallo akizungumza katika kikao na uongozi wa Mkoa wa Mbeya ili kuhakikisha wakulima wananufaika na mbolea za ruzuku wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Homera Juma Zuberi na katikati ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Said Madito
 

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homeri (kulia) akizungumza na washiriki wa kikao baina ya Viongozi Waandamizi wa Mkoa na wajumbe wa bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi,  Dkt. Anthony Diallo (kulia) kilicholenga kujadili namna bora ya kufikisha mbolea za ruzuku kwa wakulima kwa wakati na  kuhakikisha changamoto za kimfumo na uhaba wa mawakala wa mbolea vinatatuliwa kabla ya msimu kuanza. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Katibu Tawala wa Mkoa Said Madito

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...