Na Muhidin Amri, Kalambo
SERIKALI imetoa Sh.bilioni 1.4 kwa ajili ya kujenga soko la kisasa la kuuzia Samaki na dagaa katika Bandari ya Kasanga Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa.
Soko hilo litakasaidia kuongeza thamani ya Samaki na kudhibiti upotevu wa mapato unaofanywa na wafanyabiashara wanaosafirisha Samaki kwa njia ya panya kwenda nchi jirani ikiwemo Zambia na Kongo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kalambo Shafi Mpenda alisema,ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 95 na kwamba ujenzi wa soko la kisasa la Samaki la Kasanga umekuja baada ya soko la awali kuzingirwa na maji mwaka 2021 kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Aidha alisema,Halmashauri ya wilaya kupitia mapato yake ya ndani imenunua boti mbili za kisasa kwa ajili ya shughuli za doria kwenye ziwa Tanganyika ili kukomesha vitendo vya uvuvi haramu na kusaidia pale yanapotokea maafa kwenye ziwa.
Mpenda,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa moyo wa upendo kwa kuwakumbuka wavuvi wanaofanya shughuli zao katika ziwa Tanganyika na kutoa fedha ambazo zinakwenda kumaliza kilio cha muda mrefu cha wavuvi na wafanyabishara kukosa soko la kuuzia Samaki.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya uchumi, mipango na uratibu wa Halmashauri ya wilaya Kalambo Erasto Mwasanga alisema,soko la Samaki Kasanga litawasaidia wavuvi kuwa na mahali pazuri na uhakika kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
Alisema,soko hilo litakomesha vitendo vya kusafirisha Samaki kwa njia ya panya ambavyo vinasababisha serikali kushindwa kukusanya ushuru unaostahili na hivyo kuiokosesha mapato yake.
Aliongeza kuwa,litakuwa na vizimba vyenye uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara 100 kwa wakati mmoja,jokofu la kuhifadhia Samaki wabichi kabla ya kupelekwa kwenye masoko yaliyopo ndani na nje ya mkoa wa Rukwa.
Kwa mujibu wa Mwasanga,awali haikuwa rahisi kwa wavuvi na wafanyabiashara kusafirisha mazao ya Samaki kwenda kwenye miji mikubwa kutokana na kukosekana kwa soko lenye miundombinu ya kisasa.
Alisema,soko hilo litakapokamilika,wafanyabishara watasafirisha Samaki wabichi kwenda maeneo mengine kwa urahisi na amewataka wavuvi na jamii kutunza na kulinda miundombinu na kutumia fursa ya uwepo wa soko hilo kuongeza mazao ya Samaki, kwani serikali imetumia fedha nyingi katika kutekeleza mradi huo.
Wavuvi wa kata ya Kasanga na Samazi wilayani Kalambo,wameipongeza serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa soko hilo kwa kuwa litawaondolea usumbufu wa kusafirisha Samaki kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta masoko.
Martin Hondi alisema,uwepo wa soko hilo utawasaidia wavuvi kuuza Samaki kwenye soko lao badala ya kupeleka nchi jirani ya Zambia na Kongo ambako wanapata usumbufu na hata hasara kubwa kutokana na gharama za usafirishaji.
Adam Raymond,ameiomba serikali kumbana mkandarasi anayetekeleza mradi huo ili soko likamilike haraka na waweze kulitumia kuuza Samaki na bidhaa nyingine za uvuvi.
Msimamizi wa ujenzi wa soko la samaki la Kasanga wilayani Kalambo Albert Francis kushoto akitoa maelezo kwa baadhi ya wavuvi wa kijiji hicho kuhusu maendeleo ya ujenzi wa soko hilo,wa tatu kulia ni Mkuu wa idara ya uchumi, mipango na uratibu wa Halmashauri ya wilaya Kalambo Erasto Mwasanga.
Jengo la ofisi katika soko la samaki Kasanga Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa.
Sehemu ya jengo la soko la samaki na dagaa linalojengwa na Serikali katika kijiji cha Kasanga Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoani Rukwa likiwa hatua za mwisho kukamilika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...