Na Said Mwishehe, Michuzi TV
ASASI ya Agenda imeshauri Serikali kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukabiliana na changamoto ya uwepo wa madini ya risasi katika rangi ambayo madhara yake yameendelea kuleta athari katika jamii hasa kwa watoto.
Kwa mujibu wa Agenda katika kupunguza madini ya risasi katika rangi kuna kiwango maalum kinachotakiwa kutumika na Tanzania imeridhia utekelezaji wake, hivyo taasisi zote zinazohusika na utekelezaji huo zichukue hatua ili kupunguza madhara yatokanayo na madini ya risasi katika jamii.
Ushauri huo umetolewa jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya kupambana na madini ya risasi katika rangi ambayo hufanyika kila mwaka katika wiki ya tatu ya Oktoba.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisa Programu kutoka Agenda Dora Swai Kwa upande wake Dorah Swai amesema wamekuwa wakifanya uhamasishaji wa wananchi kupambana na madhara ya rangi zenye madini ya risasi.
“Tumekuwa tukiadhimisha hii wiki tangu ilipoanzishwa mwaka 2013 kwa hiyo hii ni mara ya 11 tunaadhimisha hii wiki na hatukuishia hapo huwa tunafanya tafiti ili kujua kama Tanzania nayo ina rangi yenye madini ya risasi.
“Na tukakuta ndio zipo zikiwemo rangi zinatoka nje ya nchi na zinazotengenezwa hapa nchini.Hivyo tunaitaka Serikali ishirikiane na wadau katika kuongeza nguvu kutekeleza kiwango ambacho kilitengenezwa mwaka 2017 kudhibiti madini ya risasi katika rangi yasizidi na kuleta madhara
“Kiwango hicho kipo hivyo tunaitaka Serikali iendelee kukitekeleze, tunajua taasisi za Serikali zinazotekeleza kiwango hicho zipo nyingi na kila mmoja akatekeleze kwa nafasi yake.Tunaamini haya madini ya risasi katika rangi yatatokomea kabisa,”amesema Swai.
Amefafanua madhara ya madini ya risasi inayoenda kwa watoto zaidi ilikuwa katika mafuta kama dizeli na petroli lakini hiyo imeshatolewa, hivyo ni wakati sasa wa kuondoa madini ya risasi katika rangi na isichukue muda mrefu kwani mchakato wake ulishaanza.
“Hapa nchini kwetu kuna hatua mbalimbali zilishaanza kufanyika basi tumalizie ili rangi zenye madini ya risasi ziishe kabisa nchi Tanzania.”
Kwa upande wake Ofisa Programu Mkuu wa Agenda Silvani Mng’anya amesema katika kuadhimisha wiki hiyo wameshirikiana na Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuiandaa lengo likiwa kukabiliana na madhara yatokanayo na madini ya risasi.
“Msisitizo mkubwa umekuwa katika rangi kwasababu ndio chanzo kikubwa cha watoto kukumbana na madhara ya madini ya risasi.Madhara yanayotokanayo na madini ya risasi husababisha watoto kutokuwa na uelewa wa kutunza kumbukumbu.Pia wakati mwingine husababisha uzezeta na wapo ambao wanapoteza maisha.
“Benki ya dunia imetoa takwimu kuonesha madhara yanayotokana na madini ya risasi pale yanaposababisha watoto kushindwa kuelewa na kutunza kumbukumbu.Madhara yake yamethaminishwa na kufikia kiasi cha dola za Marekani trilioni 1.4,”amesema.
Amesisitiza gharama kwa kiasi kikubwa ni katika nchi zinazoendelea hasa Bara la Afrika huku akifafanua hicho ni kiasi kikubwa hivyo kila mmoja achukue hatua ili kuokoa vizazi vyetu hasa kwa watoto vinginevyo changamoto ya watoto kutokuwa na uelewa wa mambo mbalimbali lakini kutunza kumbukumbu kuhusu yale wanayojifunza itaendelea kuongezeka.
Ameongeza kwa hiyo ni muhimu kuchukua hatua kama ilivyoelekezwa lakini kiwango kilichoelekezwa na Serikali ya Tanzania na duniani kwa ujumla ni kiasi cha sehemu 90 ya milioni alau kiasi hicho kikiwa kwenye rangi pengine hakitokani na nyongeza ya madini ya risasi katika rangi.
Amesema isipokuwa kutokana na malighafi pengine ndogondogo yaliyopo katika madini hayo, hivyo ni vizuri kuzikatingia hicho kiwango ambacho Tanzania imeridhia lakini kunakiwango cha makubaliano kwa nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla.
Awali Mratibu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Sumu chini ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Yohana Goshashy amesema nchi yetu imeendeela kuchukua hatua mbalimbali kuondoa bidhaa zenye madini hayo ya risasi akitolea mfano madini hayo yalikuwepo katika mafuta ya petroli na dizeli lakini sasa hakuna.
Amesema kwa mwaka huu kauli mbiu ya Shirika la Afya Duniani pamoja na wote ambao wanaungana katika kuadhimisha upunguzwaji wa madini ya risasi ni kuwa na watoto waliosalama dhidi ya madini ya risasi.
“Madini ya risasi yanaharibu mfumo wa fahamu, yanasababisha watoto kuathirika uwezo wao wa kufikiri na hivyo ufuatiliaji masomo huwa kidogo.Watu wengine madini hayo huathiri mfumo wa fahamu, uzazi pamoja na kuathiri mfumo mzima wa usafirishaji damu na moyo na matokeo yake mtu anaweza kupooza mwili.”
Hata hivyo amesema madhara hayatokei moja kwa moja ni ngumu kupata takwimu wangapi waanaathiriwa na madini ya risasi lakini WHO wana rekodi visa takriban milioni moja kila mwaka vya watu wanaofariki dunia kutokana na madhara yanayotokana na madini ya risasi.
Mratibu wa Kituo cha Taifa cha Udhibiti Sumu chini ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ndugu Yohana Goshashy(katikati) akifafanua jambo kuhusu madhara yatokanayo na madini ya risasi .Kushoto ni Ofisa Programu Mkuu wa Agenda Silvani Mng'anya na kulia ni Norah Swai ambaye ni Ofisa Programu kutoka Agenda.
Ofisa Programu Mkuu wa Asasi ya Agenda Silvani Mng'anya( kushoto) akielezea namna madini ya risasi katika rangi yanavyoleta madhara kwa jamii hasa watoto .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...