Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)kupitia Katibu Mkuu wake Jokate Mwegelo ametoa rai kwa jamii ya Watanzania hasa wazazi na walezi kusimamia misingi ya malezi bora kwa watoto ili kuwapa fursa ya kutimiza ndoto zao.
Kwa mujibu wa Jokate changamoto nyingi ambazo watoto wanazipitia na wakati mwingine kukatisha ndoto zao zinatokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kukosekana kwa malezi sahihi na bora kuanzia ngazi ya familia na jamii.
Jokate ameyasema hayo leo Novemba 17, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kuwatembelea wanafunzi wawili waliopata ujauzito lakini kutokana na ujasiri wao wameendelea na masomo na kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka huu.
Miongoni mwa wanafunzi hao alikuwa amejifungua siku tano zilizopita lakini aliamua kuacha kichanga chake ndani na kwenda kufanya mtihani wa kidato cha nne wakati mwingine akiwa na mtoto mwenye umri wa miezi miwili.
"Tuliposikia kuna watoto wamechukua fursa iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuendelea na shule baada ya kupata ujauzito tumeona tuje kuwatembelea.”
Pia amesema wamefika nyumbani kwa wanafunzi hao ili kuona mazingira ya nyumba wanayoishi sambamba na kuwapongeza kwa ujasiri wa kuendelea na masomo huku akisisitiza Rais Dk.Samia kwa kutambua changamoto wanazopitia watoto alitoa maelekezo yanayowezesha watoto kupata fursa ya kuendelea na masomo ili kutimiza ndoto zao.
Ameongeza watoto wengi wanaingia kwenye changamoto sio kwamba wametaka ila kuna mambo yanayochangia yakiwemo ya kurubuniwa na kukosa malezi sahihi kutoka kwa wazazi na changamoto za kiuchumi.
Aidha amewakumbusha wazazi kuhakikisha migogoro ndani ya nyumba isiwe sababu ya watoto wao kushindwa kutimiza ndoto zao.
“Serikali ya CCM inaendelea kupunguza vikwazo vya wazazi kushindwa kuwapeleka watoto shule kwa kuanzia utaratibu wa elimu bila malipo,”amesema.
Pia amesema bado kuna nafasi ya kuwezesha jamii kiuchumi ili wananchi wanufaike na makubwa ambayo Serikali yao inafanya huku akisisitiza UWT itahakikisha inakwenda kila sehemu kuona changamoto za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Pamoja na hayo Jokate amesema anatarajia kukutana na mawaziri wa Wizara nne ambazo moja kwa moja zinagusa maslahi ya wananchi.
Amezitaja Wizara hizo ni Wizara ya Afya, Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) pamoja na Wizara ya Fedha.
"Nitakaa na Wizara hizi na kupanga mikakati ya nini kifanyike ili tuwasaidie wananchi wetu wanufaike na mambo mazuri yanayofanywa na Serikali,”amesema na kueleza hatua ambazo Serikali inachukua katika kuwajengea ujasiri mabinti wa kike na mabinti hao wameonesha ujasiri mkubwa wa kupigania ndoto zao licha ya changomoto walizopitia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT,Jokate Mwegelo akizungumza na Vyombo vya Habari mara baada ya kutembelea Binti aliyeweza kufanya Mtihani mara baada ya kujifungua
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...