Na Muhidin Amri
Mbeya

WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) mkoa wa Mbeya,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kutumia zaidi ya Sh.bilioni 12 kutekeleza jumla ya miradi 46,kati ya hiyo miradi 27 ni ya kukamilishwa na miradi 19 ni mipya.

Meneja wa Ruwasa mkoani humo Mhandisi Hans Patrick alisema,lengo ni kuhakikisha wanafikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2025.

Hata hivyo alisema,kupitia bajeti ya mwaka ujao wa fedha wana uhakika kufikisha asilimia 88.5 ya utoaji wa huduma ya maji na hivyo kuvuka lengo la serikali kwa asilimia 3.


Aidha alisema,mwaka 2022/2023 walitengewa Sh.bilioni 8 lakini hadi kufikia mwezi Juni 2023 walipokea Sh.bilioni 13 zilizotumika kutekeleza miradi 49 ambayo inatoa huduma ya maji kwa wananchi wa mkoa huo.


Katika hatua nyingine Hans alisema, kabla Ruwasa haijaanza kazi mwaka 2019 hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya vijijini yanayohudumiwa na Ruwasa ilikuwa asilimia 59.1.


Hans alisema,mwitio wa watu kuingiza maji ya bomba kwenye nyumba zao ni mkubwa hasa baada ya kukamilika kwa miradi ya mingi ya maji katika vijiji mbalimbali ambavyo awali wananchi wake walitumia maji kutoka kwenye mito na visima vya asili.


Amewataka wananchi wa mkoa huo,kuhakikisha wanatunza na kulinda miradi ya maji sambamba na vyanzo vya maji kwa kuacha kukata miti na kufanya shughuli za kibinamu kwenye vyanzo ili miradi inayojengwa iweze kudumu kwa muda mrefu.


Naye meneja wa Ruwasa mkoa wa Songwe Mhandisi Charles Pambe alisema,kabla ya Ruwasa huduma ya maji katika mkoa huo ilikuwa asilimia 47 lakini katika kipindi cha miaka minne baada ya Ruwasa upatikanaji wa maji umefikia asilimia 78.8.


Pambe alisema,mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na wataalam wa Ruwasa mkoa wa Mbeya kukamilisha zaidi ya miradi viporo 20 ambayo ujenzi wake ulisua sua licha ya serikali kuwekeza fedha nyingi.


Kwa mujibu wa Pambe,wilaya ya Ileje upatikanaji wa maji kwa sasa ni asilimia 91 na kati ya vijiji vyote vya wilaya hiyo ni kijiji kimoja ambacho bado hakijapata maji ya bomba na katika wilaya ya Songwe upatikanaji wa maji ni asilimia 82 na vijiji viwili havijafikiwa na mradi wa maji.


Alitaja wilaya nyingine ni Mbozi ambayo upatikanaji wa maji ni asilia 73 na wilaya ya Momba upatikanaji wa maji umefikia asilimia 63 ambapo alisisitiza kuwa,ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji safi na salama katika wilaya hizo utavuka lengo la kitaifa la asilimia 85.


Pambe alisema,mwaka wa fedha 2022/2023 Ruwasa mkoa wa Songwe ilipokea Sh.bilioni 29 na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wametengewa zaidi ya Sh.bilioni 20 kati ya hizo Sh.bilioni 11 zimeshafika kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali.


Pia alieleza kuwa,wameanza kufunga mita za lipa kabla ya matumizi (Pre-paid) katika miradi yote inayoendelea kujengwa na zitafungwa kwenye taasisi za umma na kwenye nyumba za wananchi kwa lengo la kudhibiti na kuongeza mapato ya serikali.
MWISHO.

 

Tenki la kuhifadhi maji lililojengwa mkoani Mbeya kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
 

 Moja ya matenki lililojengwa katika mradi wa maji wa Shinji wilaya ya Ileje mkoani Songwe.
 

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ikukwa wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya wakichota maji ya bomba kwa mara ya kwanza tangu Uhuru kufuatia kukamilika kwa mradi wa maji uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),wa pili kushoto ni meneja wa Ruwasa mkoa wa Mbeya Mhandisi Patrick Hans.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...