Waongoza watalii nchini wametakiwa kuwa wazalendo wanapotekeleza majukumu yao ili kusaidia juhudi za Serikali za kuongeza idadi ya watalii na kukuza uchumi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Prof Jafari Kideghesho, wakati akifungua mafunzo ya waongoza watalii wa mlima yanayofanyika Chuoni hapo kwa muda wa wiki tatu.

Prof Kideghesho amesisitiza kuwa muongoza watalii ni mtu wa kwanza kukutana na wageni na ndiye anayekaa nao kwa muda mrefu. Hivyo ni lazima awe na nidhamu ya hali ya juu, mwaminifu, muwajibikaji, mkweli na zaidi awe mzalendo kwa nchi yake. Ameonya kuwa kitendo cha kukosa uzalendo na kuanza kusema maneno yoyote yanayochafua taswira ya nchi mbele ya wageni ni usaliti mkubwa kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kupunguza idadi ya watalii ambao wangependa kuja nchini na hivyo kushusha uchumi wa nchi na watu binafsi. "Waambie wageni maneno chanya kuhusu nchi yetu na usikubali kuiponda kwa vyovyote vile. Kuitangaza nchi vibaya ni sawa na kukata tawi la mti ulilolikalia, kwani watalii wasipokuja hata wewe ajira yako inakuwa hatarini". Alisisitiza Mkuu wa Chuo.

Naye Naibu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Wahabu Kimaro, amewataka washiriki wa mafunzo hayo wahakikishe kuwa wanatumia muda wa mafunzo hayo vizuri ili waweze kunufaika na kufikia matarajio yao na Taifa kwa ujumla kwa kuwa lengo ni kuona kuwa Sekta ya Utalii inapata watu sahihi watakaotoa huduma bora kukidhi idadi kubwa ya watalii inayotarajiwa kufuatia mikakati mbalimbali ya kitaifa iliyowekwa sambamba na kazi nzuri ya kuitangaza nchi iliyofanywa na Mheshimiwa Rais, Dr Samia Suluhu Hassan, kupitia Filamu ya Tanzania - The Royal Tour.

Awali, Meneja wa Kitengo cha Huduma za Kitaaluma Chuoni hapo, Dr Rehema Shoo, aliwahakikishia washiriki wa mafunzo hayo kuwa Mweka ni sehemu sahihi kwa ajili ya mafunzo hayo kutokana na kuwa na wataalamu wabobezi, miundombinu rafiki, vitendea kazi na zaidi mazingira mazuri ya kujifunzia. Jumla ya washiriki 60 wanahudhuria Mafunzo hayo yanayofanyika kwa wiki tatu, ambapo pamoja na nadharia, yatahusisha mazoezi kwa vitendo yatakayofanyika katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na maeneo mengine ya jirani.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...