Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amewataka Maafisa Ugani kutumia taaluma zao vizuri ili kusaidia kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinazalisha vya kutosha na kuiwezesha nchi kuwa kapu la Chakula Barani Afrika.

Prof. Shemdoe amesema hayo wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Ugani nchini (TSAEE) kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega unaofanyika jijini Dodoma kuanzia leo Novemba 20 hadi 21, 2023.

"Nyinyi ndio injini, hivyo katika Mkutano wenu huu jielekezeni katika kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ambayo imeweka kipaumbele katika kuhakikisha sekta hizi zinachangia katika upatikanaji wa chakula, lishe na kukuza kipato cha Wananchi ambao zaidi ya Asilimia 65 wanajishughulisha na Kilimo, Mifugo na Uvuvi", alisema Prof. Shemdoe

Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa Sekta hizo Serikali imekuwa ikiongeza bajeti kila mwaka lengo likiwa kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo kwa kuongeza tija kwenye uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na lishe; Kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na kuongeza mauzo ya bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ndani na nje ya nchi.

Aliendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi ambao wanaonesha dhamira ya dhati ya kuungana na serikali katika kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati kupitia shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Aidha, aliwataka Maafisa Ugani hao kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kwenye mradi wa kielelezo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT).

"Nyinyi ndio washauri wa kwanza katika programu ya BBT ambayo imelenga kuwainua vijana, utaalamu wenu utasaidia kutimiza malengo ya Rais, Dkt. Samia ya kuwainua vijana na kina mama hapa nchini", alibainisha

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Ugani(TSAEE), Prof. Catherine Msuya alizishukuru Wizara za kisekta kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Maafisa Ugani huku akiomba Wizara hizo ziendelea kukilea chama hicho kwa kukitengea bajeti ili chama hicho kiweze kujiendesha bila matatizo.

Halikadhalika, aliziomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kilimo na TAMISEMI kuboresha na kuweka mfumo mmoja ambapo utawawezeaha Maafisa Ugani hao kuwasiliana vyema tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna mifumo mingi tofautitofauti.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe akiongea na Maafisa Ugani (hawapo pichani) katika Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Ugani nchini (TSAEE) unaofanyika jijini Dodoma, Novemba 20, 2023.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akiondoka ukumbini muda mfupi baada ya kumaliza kufungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Ugani nchini (TSAEE) unaofanyika jijini Dodoma, Novemba 20, 2023. Anayemsindikiza ni Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Ugani nchini (TSAEE), Prof. Catherine Msuya (kulia).



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...