Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dk. Timothy Bende (kulia) akipokea msaada kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Sera, Ushawishi na Uraghabishi kutoka WaterAid, Christina Mhando (kulia)Na Mwandishi Wetu
KATIKA kuadhimisha siku ya choo duniani ambayo hufanyika Novemba 19 kila mwaka, Shirika la WaterAid Tanzania limetoa msaada wa vifaa vya usafi katika vituo viwili vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke.

Vituo vilivyopatiwa msaada kupitia kampeni yao ya “Choo safi, Hadhi Yangu” ni kituo kipya cha Mkondogwa kilichopo Chamanzi na Goroka klichopo Tuangoma.

Vifaa vya usafi vilivyotolewa ni pamoja na fagio, sabuni, vifaa vya kuhifadhia taka, mabuti, majaketi ang’avu na glavu ngumu.

Akizungumza wakati akitoa msaada huo, Mkuu wa Idara ya Sera, Ushawishi na Uraghabishi kutoka WaterAid, Christina Mhando amesema suala la vyoo ni suala la msingi, na wanaamini kuwa kila mahali huduma ya choo ni muhimu.

"Nichukue fursa hii kuipongeza serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani hivi karibuni takwimu za afya za mwaka 2022 (TDHS) zinaonyesha kuna ongezeko la vyoo bora kutoka asilimia 21 mwaka 2016 hadi asilimia 75 mwaka 2022...hiyo ni hatua nzuri Tanzania imefikia.

"Sisi kama WaterAid tunaendelea kuomba serikali mbali na uhamasishaji waweze kuelekeza rasilimali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kila kituo kiweze kuwa na vyoo bora," amesema Christina.

Kwa upande wa Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dk. Timothy Bende ameshukuru kwa msaada huo ambao umekwenda kwa vituo vya afya vipya.

"Tunawashukuru kwa kutoa sapoti kwenye vituo hivi viwili vipya ambavyo vimekamilika mwaka huu na vimeshaanza kutoa huduma. Tumeonelea ni jambo jema vituo hivi vichanga kuweza kupata vifaa hivi kwaajili ya kuboresha na kuimarisha masuala ya usafi," amesema Dk. Bende.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkondogwa, Dk. Amri Mkwinda amesema: "Tunashukuru kwa msaada huu pia tunapenda kutoa wito kwa mashirika mengine kuwa na moyo kama huu kwani bado tuna mahitaji mengi,".


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...