* Yapongeza ushirikiano wa Serikali na wadau wa michezo, TFF kupata fursa zaidi
SHIRIKISHO La Mpira barani Ulaya (UEFA,) limeeleza kuwa litaendelea kufadhili program ya Mpira Fursa inayotolewa na Taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO,) kupitia Vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi kote nchini na kunufaisha pia shule za Msingi zipatazo 110.
Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na mtaalam wa michezo kutoka UEFA Carine Nkoue katika kikao kilichowakutanisha na wadau mbalimbali wa soka wakiwemo KTO, Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF,) Baraza la Michezo Tanzania (BMT,) Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na TAMISEMI na kujadili mbinu za kuboresha zaidi soka la wanawake na wasichana.
Bi. Carine amesema jitihada zilizooneshwa na KTO zimeshawishi Shirikisho hilo na wataendelea kufadhili mradi huo ili kuendelea kukuza vipaji na kuwa na timu imara zitakazowakilisha Tanzania kimataifa.
"Project hii lazima iende mbele, ushirikiano huu ni wa kuigwa taasisi muhimu kama TFF, Wizara ya Elimu na Serikali kwa ujumla kushiriki katika miradi ya namna hii ni hatua kubwa inayohitaji usimamizi zaidi katika kuyafikia malengo." Amesema.
Amesema ushiriki wa TFF katika mradi huo ni kionjo tosha kwa kuwa Shirikisho hilo linatambua kucheza mpira ni zaidi ya burudani hivyo vijana watanufaika na ajira kupitia TFF na kuahidi kuisemea vyema TFF ambayo inatambulika na Shirikisho la Mpira Duniani (FIFA,) ili ipate fursa zaidi na kuboresha sekta ya michezo Tanzania.
Aidha amesema, siku ya jumapili watakabidhi vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo mipira 400 kutoka UEFA ikiwa ni sehemu ya kutambua jitihada za KTO kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau katika kukuza soka la wanawake na wasichana Tanzania.
Kwa upande wake Mratibu wa Michezo kutoka kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Yusuph Singo amesema ugeni huo wa UEFA ni jitihada za KTO kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kukuza soka la wanawake na wasichana Nchini kupitia Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi (FDC's,) ambapo Shule za Msingi zipatazo 110 pia zinanufaika na mradi huo wa Mpira Fursa.
Amesema watatumia fursa iliyotolewa na UEFA ya kuendeleza kudhamini program hiyo kwa kuhakikisha wanazifikia Shule nyingi zaidi ili kuzidi kutangaza Nchi kimataifa kupitia soka.
"KTO wamefanya kazi kubwa sana katika kutengeza timu za Mikoa pamoja na kutoa mafunzo kwa makocha na marefa kwa kushirikiana na TFF jitihada zao zinaonekana dhahiri na zinahitaji kuungwa mkono ili kuyafikia mafanikio makubwa zaidi." Amesema.
Pia Afisa wa Michezo kutoka Baraza la Michezo Tanzania (BMT,) Nicholas Mihayo ameeleza, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na KTO na mambo makubwa yanayofanywa na taasisi hiyo yanapaswa kutangazwa na kuungwa mkono na Serikali na wadau mbalimbali.
Mihayo ameishukuru na kuipongeza UEFA kwa ufadhili wa Fedha, mafunzo na vifaa vya michezo na jukumu la Serikali litaendelea kwa kuweka mazingira bora na yenye kuleta mafanikio makubwa kwa kuongeza timu zaidi katika mashindano ya kimataifa.
Amesema Serikali ipo tayari wakati wowote kwa maoni na ushauri pamoja na ushirikiano wa kuhakikisha soka la wanawake na wasichana linakua kimataifa.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO,) Maggid Mjengwa (kulia,) akimkabidhi zawadi ya jezi ya Tanzania Mtaalam wa michezo kutoka Shirikisho la Mpira Barani Ulaya (UEFA) kitengo cha UEFA Foundation For Children Taasisi maalum ya kuendeleza soka kwa watoto na vijana Carine Nkoue (Katikati,) mara baada ya kumaliza kikao hicho. Kushoto ni Afisa Michezo kutoka TAMISEMI Yusuph Singo. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Program wa Taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO,) Mia Mjengwa akiwasilisha mada ya utekelezaji wa program ya Mpira Fursa inayotolewa na Taasisi hiyo kwa Vyuo 54 Vya Maendeleo ya Wananchi (FDC's,) na kunufaisha shule za Msingi zipatazo 110. Leo jijini Dar es Salaam.
Mtaalam wa michezo kutoka Shirikisho la Mpira Barani Ulaya (UEFA) kitengo cha UEFA Foundation For Children Taasisi maalum ya kuendeleza soka kwa watoto na vijana Carine Nkoue (katikati waliokaa,) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa sekta ya michezo nchini wakiwemo TFF, BMT, TAMISEMI, KTO na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mara baada ya kukamilika kwa kikao hicho kilichofanyika Leo katika Ofisi ya KTO jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...